Wajue makocha waliowakosoa wachezaji wao hadharani

ty

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ruben Amorim, mkufunzi wa Manchester United
    • Author, Tom Mallows
    • Nafasi, BBC Sport
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Mkufunzi wa Manchester United, Ruben Amorim amegonga vichwa vya habari aliposema, ni bora kumuweka kama mchezaji wa akiba kocha wake wa makipa mwenye umri wa miaka 63, kuliko Marcus Rashford, kwa sababu hana juhudi.

Rashford hajacheza kwenye kikosi cha United kwa muda wa wiki sita. Amorim anasema mshambuliaji huyo wa Uingereza hafanyi vyema katika mazoezi.

Mustakabali wake ndani ya Old Trafford haujulikani. Kuna klabu za Ulaya zinazohusishwa na kutaka kumsajili mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27, kabla ya tarehe ya mwisho ya uhamisho wa wachezaji wiki ijayo.

Sio mara ya kwanza kwa kocha wa Ligi Kuu England kumkosoa hadharani mmoja wa wachezaji wake.

Harry Redknapp na Darren Bent

dc

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Darren Bent alifunga mabao 25 ​​katika mechi 79 akiwa na Tottenham kati ya 2007 na 2009.

Harry Redknapp alidai kuwa mke wake angefunga, pale Darren Bent alipokosa nafasi ya dakika za lala salama. Siku Tottenham ilipotoka sare ya 1-1 na Portsmouth Januari 2009.

Redknapp alisema: "Huwezi kupata nafasi nzuri zaidi ya kushinda goli kuliko ile uliyoipata. Mke wangu angeweza kufunga."

Licha ya kauli hiyo, Bent alibaki kwenye safu ya wachezaji wa Redknapp na alimaliza msimu wa 2008-09 kama mfungaji bora wa Tottenham akiwa na mabao 17, kabla ya kujiunga na Sunderland majira ya kiangazi.

Redknapp alitumia miaka mingine mitatu na nusu akiwa White Hart Lane (Tottenham) akiwasaidia kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa mwaka 2011, lakini alitimuliwa Juni 2012.

Harry Redknapp na Adel Taarabt

dx

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Adel Taarabt alitawazwa kuwa Mchezaji Bora baada ya kuisaidia QPR kutwaa ubingwa wa Championship msimu wa 2010-11.

Redknapp, wakati huo akiwa meneja wa QPR, hakusita kumkosoa Adel Taarabt alipoulizwa kwa nini kiungo huyo ameachwa nje ya kikosi kwenye mchezo dhidi ya Liverpool, Oktoba 2014.

"Siwezi kuwalinda watu ambao hawataki kukimbia na kufanya mazoezi, na wana uzito wa mawe matatu," alisema Redknapp.

"Alicheza katika mchezo wa timu ya kikosi cha pili juzi na ningeweza kukimbia zaidi ya alivyokimbia yeye. Siwezi kumchagua."

Taarabt ilijibu kwa kusema Redknapp alikuwa akitoa visingizio kutokana na matokeo mabaya ya timu hiyo, wakati huo timu ikiwa nafasi ya chini kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Kiungo huyo aliichezea klabu hiyo mechi tano tu, kabla ya kujiunga na Benfica msimu wa joto wa 2015.

QPR ilishuka daraja mwishoni mwa msimu wa 2014-15. Redknapp aliipandisha tena daraja timu hiyo msimu uliofuata kabla ya kung'atuka Januari 2015.

Jose Mourinho na Luke Shaw

d

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Manchester United ilimsajili Luke Shaw kutoka Southampton kwa pauni milioni 27 mwaka 2014 alipokuwa na umri wa miaka 18.

Jose Mourinho alimkosoa beki wa Uingereza, Luke Shaw wakati akiinoa Manchester United, akihoji kujitolea na utimamu wake.

Baada ya kuingia kama mchezaji wa akiba dhidi ya Everton Aprili 2017 Mourinho alisema beki huyo wa pembeni alitumia "mwili wake na ubongo wangu."

Aliongeza: "Alikuwa mbele yangu na nilikuwa nikimfanyia kila uamuzi."

Shaw bado yuko Old Trafford lakini ana jeraha, na amecheza mechi tatu tu msimu huu.

Mourinho alifutwa kazi Disemba 2018 baada ya kuuanza vibaya msimu huo.

Jose Mourinho na Tanguy Ndombele

v

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Tanguy Ndombele alikuwa mchezaji aliyevunja rekodi ya kununuliwa kwa pesa nyingi katika klabu ya Tottenham hadi Dominic Solanke alipojiunga kutoka Bournemouth majira ya joto yaliyopita.

Mourinho, alihamia Tottenham na kuwa meneja wa Tottenham, alimkosoa mchezaji aliyesajiliwa kwa pauni milioni 54, Tanguy Ndombele, Machi 2020.

Baada ya kiungo huyo kubadilishwa wakati wa mapumziko ya mchezo dhidi ya Burnley, Mourinho alisema: "Kipindi cha kwanza hatukuwa na safu ya kiungo. Yeye [Ndombele] amepata muda wa kutosha kupanda kiwango.

"Najua Ligi Kuu ni ngumu, na wachezaji wengine huchukua muda mrefu kuzoea ligi tofauti. Lakini mchezaji mwenye uwezo kama yeye, ni lazima atupe zaidi ya anachotupa sasa."

Hakukuwa na mwisho mwema kwa Mourinho wala Ndombele. Mourinho alitimuliwa Aprili 2021 baada ya kuiongoza kwa miezi 17, siku chache kabla ya fainali ya Kombe la Carabao dhidi ya Manchester City kwenye Uwanja wa Wembley.

Ndombele alipata tena nafasi katika timu wakati wa mechi za 2020-21, lakini alitumia misimu mitatu iliyofuata kwa mkopo kabla ya kuachiliwa kwa uhamisho wa bure Juni 2024.

Pep Guardiola na Kalvin Phillips

fv

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kalvin Phillips bado ana miaka mitatu na nusu kwenye mkataba wake Manchester City

Kocha wa Manchester City Pep Guardiola alidai Kalvin Phillips ni "mzito kupita kiasi" baada ya kurejea kutoka Kombe la Dunia la 2022 na ndio sababu iliyomfanya kuachwa nje ya kikosi kwa mechi ya raundi ya nne ya Kombe la Carabao dhidi ya Liverpool.

Phillips alisema maoni hayo "yaliharibu sana kujiamini kwake," huku Guardiola akiomba msamaha hadharani kwa kiungo huyo wa kati wa Uingereza.

Mchezaji huyo wa zamani wa Leeds aliichezea City mechi 27 kabla ya kujiunga na West Ham kwa mkopo Januari 2024. Kisha akahamia Ipswich kwa mkopo msimu uliopita.

Erik ten Hag na Jadon Sancho

df

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Jadon Sancho alianza msimu na Manchester United kabla ya kujiunga na Chelsea kwa mkopo

Kocha wa wakati huo wa Manchester United, Erik ten Hag hakumchezesha Jadon Sancho kwenye mechi dhidi ya Arsenal, Septemba 2023 kwa sababu aliamini winga huyo wa Uingereza hajafikia "kiwango" kinachohitajika mazoezini ili kujumuishwa.

Sancho alijibu kwa kusema, amefanywa "mbuzi wa kafara kwa muda mrefu."

Alilazimika kufanya mazoezi nje ya kikosi cha kwanza kabla ya kujiunga na klabu yake ya zamani ya Borussia Dortmund kwa mkopo mwezi Januari.

Ten Hag alifanya mazungumzo ya wazi na Sancho aliporejea United kutoka Borussia Dortmund, wakati wa mazoezi ya kujiandaa na msimu wa kiangazi mwaka 2024, lakini mchezaji huyo wa zamani wa Manchester City alijiunga na Chelsea kwa mkopo siku ya mwisho ya dirisha la uhamisho.

Ten Hag alifutwa kazi na Manchester United mwezi Oktoba huku klabu hiyo ikiwa nafasi ya 14 kwenye Ligi ya England, baada ya kushinda mechi tatu tu kati ya tisa za ufunguzi.

Ange Postecoglou na Timo Werner

rf

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ange Postecoglou alimsajili Timo Werner kwa mkopo kutoka RB Leipzig Januari 2024, na mkataba huo uliongezwa hadi mwisho wa msimu huu.

Kocha wa Tottenham, Ange Postecoglou alisema kiwango cha Timo Werner "hakikubaliki" baada ya kumtoa wakati wa mapumziko, katika mechi ya sare ya Ligi ya Europa dhidi ya Rangers mwezi Desemba.

"Tunahitaji kila mtu, akiwemo yeye kuchangia," alisema Postecoglou. "Nilitarajia kiwango kikubwa cha uchezaji kutoka kwa baadhi ya wachezaji waandamizi, na usiku wa leo haikuwa hivyo."

Mshambuliaji wa Ujerumani, Werner ameanza katika mechi mbili na mechi tano akitokea benchi tangu mchezo wa Rangers.

Postecoglou amesalia kwenye dimba la Tottenham lakini yuko chini ya shinikizo baada ya kufungwa mechi nane kati ya mechi 10 za Premier League.

Imetafsiriwa na Rashid Abdalla na kuhaririwa na Ambia Hirsi