Mfahamu nyota wa Misri Omar Marmoush, "mrithi wa Salah", ambaye anakaribia kujiunga na Manchester City

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Omar Marmoush
    • Author, Abdulsalam Hatamleh
    • Nafasi, BBC Arabic
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Manchester City wamefikia "makubaliano ya mazungumzo" na klabu ya Ujerumani Eintracht Frankfurt kumsajili mshambuliaji nyota Omar Marmoush katika kipindi hiki cha majira ya baridi kali, vyanzo kadhaa viliiambia BBC.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Misri mwenye umri wa miaka 25 amefunga mabao 20 katika mechi 26 katika mashindano yote akiwa na klabu hiyo ya Ujerumani tangu kuanza kwa msimu wa sasa wa soka.

"Makubaliano ya mazungumzo yameafikiwa kati ya klabu hizo mbili lakini mchakato wa uhamisho bado haujakamilika," duru hizo ziliiambia BBC.

Kutokana na mchezo wake mzuri , Marmoush alikua gumzo la kipindi cha uhamishaji wa msimu wa baridi ulioanza mwanzoni mwa Januari, huku kukiwa na juhudi za vilabu vya Ulaya kumpata.

Uhamisho wa Marmoush kwenda City, ambaye alijiunga na Frankfurt kwa uhamisho wa bila malipo, unakadiriwa kuwa karibu euro milioni 67, kulingana na gazeti la Uingereza la Daily Mail.

Wamisri wanatumai kuzaliwa kwa "Farao" mpya baada ya nyota wa Liverpool, Mohamed Salah

Safari iliyokaribia kuisha mapema

Marmoush alizaliwa Cairo mnamo Februari 1999, na alianza maisha yake ya soka katika klabu yake ya Akademi ya Wadi Degla Club na kuendelea na timu hiyo hadi 2017.

"Kipaji chake kiliibuka mapema na akaanza kupanda ngazi hadi timu ya vijana wemye umri mkubwa kwa sababu ya talanta yake," alisema Ali Abu Greisha, meneja wa sekta ya vijana wa Wadi Degla wakati huo.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mfaransa Patrice Carteron, kocha wa Wadi Degla wakati huo, aliona talanta ya Marmoush na kumpandisha kwenye kikosi cha kwanza mnamo 2016 alipokuwa na umri wa miaka 17.

Mkuu wa Klabu ya Wadi Degla, Hazem Khairat, aliambia BBC kwamba Marmoush amethibitisha ustadi wake tangu mechi yake ya kwanza baada ya kuitwa kwenye kikosi cha kwanza msimu wa 2015/2016, baada ya kuchangia pasi ya uhakika katika ushindi wa 3-2 wa timu yake. Al-Ittihad ya Alexandria katika michuano ya ligi.

Khairat, ambaye amekuwa akifanya kazi katika klabu ya Wadi Degla tangu 2007, alidokeza kwamba bao la kwanza la Marmoush akiwa na Wadi Degla lilikuwa dhidi ya Sharkia msimu wa 2016/2017, ambao ulimalizika kwa mabao mawili bila majibu, na katika msimu huo huo, chini ya uongozi wa kocha Ahmed Hossam Mido wakati huo.

Lakini kazi ya Marmoush ilikaribia kukoma mapema kwa sababu baba yake, ambaye pia ana uraia wa Canada, alitaka mwanawe azingatie zaidi masomo yake.

"Nilishangaa baba yake aliponiambia kwamba Marmoush atakosa mafunzo wakati wa mwaka wa shule kwa sababu ratiba ya mafunzo ilikinzana na siku yake ya shule," Abu Greisha, gwiji wa zamani wa Ismaily alisema. "Omar alipinga uamuzi huu, hivyo niliamua kwa makubaliano na baba yake na uongozi wa klabu kumpanga kocha wa kumfundisha peke yake ili tusipoteze kipaji hiki mapema.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Omar Marmoush

Akiwa na umri wa miaka 18, Marmoush ambaye ana uraia wa Canada, alihamia Ujerumani, ambapo awali aliichezea timu ya akiba ya Wolfsburg, ambayo aliendelea nayo hadi alipopanda kwenye kikosi cha kwanza mwanzoni mwa 2021, mwaka ambao alijiunga na timu ya taifa ya Misri kwa mara ya kwanza.

Mnamo Oktoba 2021, Mreno Carlos Queiroz alimjumuisha katika timu ya taifa ya Misri pamoja na nyota Salah na wachezaji wenzake, baada ya kushinda taji la mchezaji bora chipukizi katika Bundesliga kwa mwezi wa Septemba.

Wakati wake na Wolfsburg, Marmoush alitolewa kwa mkopo kwa St. Pauli, ambayo alicheza katika kitengo cha pili, na kisha Stuttgart.

Kisha akarejea Wolfsburg, ambapo alitumia msimu wa 2022-2023 kabla ya kujiunga na Frankfurt msimu wa joto wa 2023 baada ya mkataba wake na wa zamani kumalizika.

Takwimu za kuvutia macho

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Katika msimu wake wa pili na Frankfurt, Marmoush, ambaye anaweza kucheza katika nafasi kadhaa kwenye safu ya ushambuliaji, alifunga mabao 15 na kusaidia 9 katika mechi 17 za Ligi ya Ujerumani, na pia alifunga bao na kutoa pasi mbili za mabao kwenye Kombe, kabla ya timu yake kutolewa katika hatua ya kumi na sita.

Huko Uropa, alifunga mabao 4 na kutoa asisti 2 kwenye Ligi ya Europa, shindano la pili kwa ukubwa kwa bara katika kiwango cha vilabu, katika mechi 6.

Ingawa ni nusu tu ya msimu umepita, Marmoush tayari ameipita idadi yake ya mwaka jana alipofunga mabao 12 na kutoa asisti 6 katika mechi 29.

Kulingana na tovuti ya takwimu ya Opta, Marmoush amekuwa, wakati wa msimu huu, mchezaji wa kwanza katika historia ya Eintracht Frankfurt kufunga mabao 10 katika mechi tisa za kwanza kwenye Ligi ya Ujerumani.

Pia akawa mchezaji wa kwanza kufunga mabao 6 katika raundi tano za kwanza za Bundesliga, rekodi mpya kwa mchezaji kutoka Frankfurt. Alichaguliwa katika timu bora mara 4 katika raundi sita za kwanza.

Marmoush pia amekuwa mchezaji wa kwanza kutoka ligi tano bora za Ulaya kufunga bao kutoka kwa mpira wa adhabu wa moja kwa moja katika mechi tatu mfululizo, tangu Lionel Messi akiwa na Barcelona mnamo 2019.

Akiwa na bao lake la 13 kwenye ligi, Marmoush alikua mchezaji wa tatu kufunga idadi hii ya mabao katika kipindi cha kwanza cha msimu mmoja wa Bundesliga kwa Eintracht Frankfurt tangu 2010.

Wakati wa msimu huo, Marmoush aliungana na mwenzake Salah kwa kutoa pasi nyingi zaidi katika ligi tano bora za Ulaya, baada ya kila mmoja wao kutoa pasi 10.

Kuhamia klabu nyengine

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Marmoush na Salah katika timu ya taifa ya Misri

Baada ya takwimu zake za kushangaza, vilabu vya Uropa sasa vinamtazama Marmoush. Mchezaji huyo pia amelinganishwa na Mohamed Salah.

Hata hivyo, nyota huyo wa Liverpool hapo awali aliomba kutomlinganisha Marmoush naye, kwani hilo lingeongeza shinikizo kwake.

Salah alisema, "Omar Marmoush ni mmoja wa wachezaji wa Misri na Waarabu ambao walitatizika na kukumbana na hali ngumu Ulaya hadi kufikia kiwango chake cha sasa."

"Omar ana uwezo mkubwa na ni mchezaji muhimu kwa timu yake na timu ya taifa kwa sasa, lakini natumai tutakaa mbali na wazo la kulinganisha, kwa sababu litampa presha kila wakati. Usimlinganishe na mimi, usiseme yeye ni Mohamed Salah mpya, mwache aishi maisha yake ya soka, kulinganisha mchezaji mwanzoni mwa kazi yake na mwingine ambaye amepata mafanikio mengi kwa miaka mingi, ni jambo ambalo halimsaidii," aliongeza. .

Kwa mujibu wa tovuti ya "Coat Offside", Marmoush anaweza kuwa moja ya mikataba muhimu inayotarajiwa wakati wa majira ya baridi, huku kukiwa na hamu kutoka kwa zaidi ya klabu moja, kama vile Liverpool, Arsenal, Chelsea na Manchester City.

Marmoush anaweza kufidia uwezekano wa kuondoka kwa Salah kutoka Liverpool mwishoni mwa msimu huu. Pia, kudorora kwa matokeo ya City, bingwa mara nne wa Ligi Kuu England, yanaisukuma kuimarisha safu yake.

Gharama ya uhamisho wa Marmoush inakadiriwa kuwa karibu euro milioni 60, kwa mujibu wa tovuti ya "Transfer Market", ikibainisha kuwa anabanwa na mkataba na klabu yake ya sasa unaoendelea hadi 2027.

Afisa wa Klabu ya Wadi Degla, Hazem Khairat, alikadiria kwamba klabu ingenufaika kwa kumuuza mchezaji huyo kwa klabu nyingine yoyote katika siku zijazo kwa takriban 3% ya thamani ya jumla ya uhamisho wake kama "mchango wa mshikamano kwa mujibu wa sheria ya Shirikisho la Kimataifa la Chama cha Soka."

Wakala wa habari wa Marmoush, Ahmed Abdoun, alisema Oktoba mwaka jana, "Bundesliga ilikuwa lango la nyota wengi kuhamia ligi kuu, iwe England au Uhispania. Ofa zikifika, tutazijadili na klabu na kufanya uamuzi mwafaka kwa kila mtu," kulingana na Agence France-Presse

Imetafsiriwa na kuchapishwa na Seif Abdalla