Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Arsenal yaiondoa Madrid kwa aibu, yatinga nusu fainali ya UCL kukutana na PSG
Arsenal imetinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa kwa mara ya tatu katika historia ya klabu hiyo baada ya kuwachabanga Real Madrid kwa matokeo ya jumla ya 5-1, kufuatia ushindi wa 2-1 ugenini katika uwanja wa Santiago Bernabeu usiku wa Jumatano.
Kwa ubora wa Madrid, na historia yao kwenye michuano ya ligi ya mabingwa Ulaya, kuchapwa nyumbani na ugenini ni aibu.
Bukayo Saka aliifungia Arsenal bao la kuongoza kwa ustadi katika dakika ya 65, baada ya awali kukosa penati. Vinicius Junior aliisawazishia Madrid dakika mbili baadaye kwa makosa ya William Saliba, lakini Gabriel Martinelli alihakikishia ushindi Aersenal kwa bao la pili katika dakika za majeruhi za kipindi cha pili.
Katika nusu fainali, Arsenal itakutana na Paris Saint-Germain (PSG). PSG iliwatoa Liverpool kwa mikwaju ya penalti katika hatua ya 16 bora na kisha kuiondoa Aston Villa kwa jumla ya mabao 5-4 katika robo fainali, licha ya Villa kushinda mchezo wa marudiano kwa 3-2.
Katika robo fainali nyingine, Barcelona ilipita kwa mbinde dhidi ya Borussia Dortmund kwa jumla ya mabao 5-3, baada ya kupoteza mchezo wa marudiano kwa 3-1. Barcelona itakutana na Inter Milan katika nusu fainali nyingine. Inter ilifuzu kwa jumla ya mabao 4-3 dhidi ya Bayern Munich baada ya sare ya 2-2. Katika mchezo wa awali inter ilishinda 2-1
Ratiba Kamili ya Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa:
Arsenal vs Paris Saint-Germain
Barcelona vs Inter Milan
Michezo ya kwanza ya nusu fainali itachezwa Aprili 29-30, 2025, na michezo ya marudiano itapigwa Mei 6-7, 2025.