PSG 'inayotisha' yajenga ufalme wake?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Louis Enrique
Muda wa kusoma: Dakika 5

Paris St-Germain inaonekana kama timu inayojenga ufalme mpya baada ya kikosi cha Luis Enrique kuibomoa timu nyingine kubwa ya Ulaya - mara hii Real Madrid 4-0 - na kutinga fainali ya Kombe la Dunia la Vilabu.

Wafaransa hao waliwazaba Inter Milan 5-0 wiki tano na nusu zilizopita kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa - na wanaonyesha dalili chache za kuachia.

Ingawa wakosoaji wamelipuuzilia mbali Kombe la Dunia la Vilabu kuwa karibu na mashindano ya kirafiki, sivyo ilivyochezwa. Kombe hilo Iinachukuliwa kwa uzito kama mashindano yoyote na wachezaji.

PSG walilazwa na Botafogo ya Brazil, lakini wamezishinda Atletico na Real Madrid 4-0 katika michuano hiyo inayoendelea Marekani, pamoja na mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich 2-0 licha ya kumaliza mchezo na wachezaji tisa.

Timu zote hizi zimeshindwa kustahimili kasi ya PSG, pasi na shinikizo yao huku timu hiyo ikiendelea kusambaratisha timu yoyote katika njia yao.

Waliongoza 3-0 ndani ya dakika 24, shukrani kwa Fabian Ruiz aliyefunga mara mbili na Ousmane Dembele, kabla ya Goncalo Ramos kufunga zikiwa zimesalia dakika tatu.

Wafuatao ni Chelsea katika fainali itakayochezwa Jumapili huko New Jersey.

"Luis Enrique ameunda timu ya kutisha," alisema mchambuzi wa Dazn Andros Townsend.

Naye mshambuliaji wa zamani wa Real Madrid, Gareth Bale aliongeza: "Wanaonekana kama timu ambayo itakuwepo kwa muda mrefu.

"Ni wachanga sana, hawana huruma na wanataka kuaibisha kila timu."

Pia unaweza kusoma

Wamebadilika vipi?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Katika kipindi cha mwaka mmoja, PSG imekuwa timu ambayo watu wengi wasiopendelea upande wowote walidhani itapoteza kwenye Ligi ya Mabingwa - kwa timu bora zaidi ulimwenguni.

Nyota wawili wa 'PSG ya zamani' - ambao walikuwa na ubinafsi zaidi kuliko timu - cha kushangaza ni kwamba walikuwa upande usiofaa wa 4-0 huko Marekani.

Ni Inter Miami ya Lionel Messi katika hatua ya 16 bora na Real Madrid ya Kylian Mbappe katika mechi ya Jumatano ya upande mmoja ya hatua ya mtoano.

Tangu Mbappe, mfungaji bora wa muda wote wa PSG, alipoondoka majira ya kiangazi yaliyopita kwenda Madrid wakati mkataba wake ulipomalizika, Enrique amejenga sura mpya ya mashambulizi.

Dembele, Desire Doue na Khvicha Kvaratskhelia ni umeme. Wakati mwingine Bradley Barcola yuko ndani kusababisha matatizo zaidi.

Safu yao ya kiungo cha kati ina wachezaji wawili wa Ureno Joao Neves na Vitinha, na Mhispania Ruiz mwenye mabao mawili - hudhibiti mechi.

Kiungo wa kati wa zamani wa Chelsea John Obi Mikel alisema kwenye Dazn wakati wa mapumziko: "Wakati watatu katikati wanaamuru mchezo uchezwe hivyo, hakuna anayeweza kuwazuia. Limekuwa darasa kuu."

Mshambulizi wa zamani wa Newcastle Callum Wilson aliongeza: Mchezo wa PSG ni kama kutazama kama kutazama Fifa. Ajabu."

Na hiyo ni bila kutaja mabeki wa pembeni wa kushambulia bila kukoma Achraf Hakimi na Nuno Mendes, ambao pia ni sehemu kubwa ya jinsi PSG wanavyocheza.

Na wakiwa wameshinda Kombe la Ufaransa, Ligue 1 na Ligi ya Mabingwa, sasa wamebakiza mechi moja tu kabla ya kunyakua taji la nne kuu la 2025.

Chelsea watakuwa na kazi ya kuwazuia Jumapili. Wakirejea kwenye fainali ya Coupe de France, PSG wameshinda mechi zao tano za raundi ya mtoano kwa jumla ya mabao 18-0.

Luis Enrique sasa lazima achukuliwe kuwa mmoja wa makocha mashuhuri katika soka la dunia, baada ya kushinda Trebles akiwa na Barcelona na PSG.

"Ameweka kiwango," alisema Bale raia wa Wales. "Wanaongoza enzi mpya.

"Wameweka kiwango cha juu sana na kila mtu katika soka atakuwa akijaribu kuwaiga na kujaribu kuwazuia."

Wasiwasi pekee kwa PSG unaweza kuwa uchovu.

Jumapili itakuwa mechi yao ya 65 tangu kuanza kwa kampeni za 2024-25. Mwezi mmoja tu baada ya mchezo huo watamenyana na Tottenham kwenye Uefa Super Cup kuanza 2025-26.

Dembele afurahisha

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Je, Ousmane Dembele atashinda Ballon d'Or mwaka huu? Kuna uwezekano

Dembele hakika ametoka kwenye kivuli cha Mbappe msimu huu.

Mfaransa huyo mwenye umri wa miaka 28 amefunga mabao 35 na kutengeneza asisti 16 katika michezo 52 mnamo 2024-25, ikijumuisha mashindano haya.

Hadi kufikia sasa, msimu bora wa ufungaji wa Dembele ulikuwa 14 kwa Barcelona.

Mchezaji huyu mwenye kasi sasa ndiye anayepewa nafasi kubwa kushinda tuzo ya Ballon d'Or - jambo ambalo lingeonekana kutowezekana mwaka mmoja au miwili iliyopita.

"Ni mechi ya kwanza katika michuano hii ambayo tunaweza kumtumia [kuanza] Ousmane na nadhani amekuwa mchezaji wetu bora msimu huu," Luis Enrique alisema.

"Anastahili kushinda kila kitu kwa sababu anatoa kila kitu kwa klabu na amefanya hivyo msimu mzima."

Fowadi wa zamani wa England Wilson, 33, aliongeza: "Nambari za kushangaza kutoka kwa Dembele.

"Ikiwa atashinda Kombe la Dunia la Vilabu baada ya kushinda Treble, bila shaka anapaswa kushinda Ballon d'Or?"

Na sio nambari hizo tu zinazovutia.

"Yote huanza kutokana na kiwango cha mchezo wa Dembele - anawalazimisha wachezaji kufanya makosa," alisema Townsend wakati wa mapumziko, huku akitoa muhtasari wa mchezo mzuri wa PSG.

Alonso 'atajifunza kitu kutoka kwa kichapo hicho

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Baada ya mapumziko ya kiangazi, Xabi Alonso hatakuwa na muda mwingi wa kuwaandaa Real Madrid tayari kwa kampeni mpya ya La Liga

Tofauti na Luis Enrique, Xabi Alonso bado anajifahamisha kuhusu timu yake ya Real Madrid.

Mhispania huyo alichukua usukani mwishoni mwa msimu wa La Liga wakati Carlo Ancelotti alipoondoka kwenda Brazil - na bado ana kazi nyingi ya kufanya kulingana na ushahidi wa mechi hiyo.

Alonso amekuwa akifanya majaribio ya uundaji, akijaribu safu za nyuma za watu wanne na watano. Beki wa kulia wa Uingereza Trent Alexander-Arnold alikosa pambano hili kutokana na jeraha, hivyo kiungo Federico Valverde alicheza katika nafasi hiyo badala yake.

Na haikusaidia kwasababu washambuliaji wao hawakufanya bidii ya kutosha.

"Vinicius Jr na Mbappe hawakurudi nyuma kila walipopokonywa mpira na tatizo hilo ni kubwa katika mfumo huu," alisema Townsend.

"[Beki wa kushoto] Fran Garcia hana furaha, amekuwa hana usaidizi kabisa katika upande huo wa kushoto."

Alonso alikiri: "Wameijenga timu yao kwa miaka miwili na ndio tunaanza hivyo tutachukua muda, itabidi tujifunze kutoka leo, lakini hisia kwa sasa sio nzuri.

"Tunahitaji mapumziko ya kutosha. Huu si mwanzo wa mwaka ujao, huu ni mwisho wa msimu huu. Baada ya wiki tatu tu hapa nadhani tunaweza kujifunza . Tutajifunza kuanzia leo."

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Seif Abdalla