Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Wafungwa wa zamani wafichua walivyonyanyaswa na kuteswa katika gereza la Urusi
Wafungwa wa zamani wameelezea BBC jinsi walivyolawitiwa na kuteswa katika magereza ya Urusi. Picha zilizovuja za unyanyasaji zilisambazwa na mtu wa ndani mwaka jana, na sasa waathiriwa wameaimbia BBC kwa nini uyanyasaji huo hufanyika na namna wanavyopigania haki.
Onyo:Makala haya yana picha za kutisha na maelezo ya unyanyasaji wa kingono na vurugu.
Hospitali ya magereza ya Saratov, kusini-magharibi mwa Urusi, iligonga vichwa vya habari mwaka jana wakati video za unyanyasaji wa kutisha wa wafungwa zilipovujishwa kwa shirika la haki za binadamu na kuripotiwa na vyombo vya habari vya kimataifa.
Alexei Makarov alijua sifa ya gereza hilo kabla ya kuhamishiwa huko mnamo 2018 kama sehemu ya kifungo cha miaka sita kutokana na hatia kushambulia.
Wafungwa ambao wanapelekwa Saratov kutoka magereza mengine katika eneo hilo wamelalamika kwamba misingi ya matibabu ilibuniwa ili waweze kuteswa wakiwa nje ya milango iliyofungwa.
Magereza ya Urusi karibu yote hayana uangalizi wa kujitegemea, na hospitali za magereza - na sheria zao za karantini ya afya - hata kidogo.
Makarov alikuwa mgonjwa - aligunduliwa kuwa na maradhi ya kifua kikuu TB - na alitumai ataonewa huruma. Lakini anasema alinyanyaswa kingono mara mbili akiwa huko.
Waathiriwa na wataalamu wanasema unyanyasaji huo - ambao Makarov na wengine wamefanyiwa - mara zote umeidhinishwa na wakuu wa magereza, na hutumiwa kuwahadaa wafungwa, kuwatisha, au kuwalazimisha waungame makosa yao.
Uvujaji wa hali ya juu wa kanda za video za mateso zimeilazimu serikali ya Urusi kujibu kashfa ya mateso ya nchi hiyo.
Mateso yaliripotiwa katika 90% ya mikoa ya Urusi kati ya 2015 na 2019, kulingana na mradi huru wa vyombo vya habari vya Urusi unaofahamika kama Proekt.
Lakini mamlaka imekuwa ikijivuta kuchukua hatua. BBC imechambua maelfu ya hati za mahakama za kipindi hicho na kubaini kuwa wanachama 41 wa huduma ya magereza walipatikana na hatia katika kesi mbaya zaidi za udhalilishaji wafungwa.
Lakini karibu nusu yao walipewa tu hukumu zilizosimamishwa. BBC imezungumza na wafungwa wa zamani akiwemo Makarov kuhusu mateso waliyokumbana nayo katika mfumo wa jela nchini Urusi.
Mara ya kwanza Makarov aliteswa ilikuwa Februari 2020, anasema.
Alikataa kukiri njama iliyodhaniwa kuwa dhidi ya uongozi wa gereza na wanaume watatu walimfanyia unyanyasaji wa kijinsia mfululizo, anasema. "Kwa dakika 10 walinipiga, wakanirarua nguo.
Na kwa saa mbili zilizofuata walinibaka kila dakika wakati mwingine kwa kutumia mpini wa mop.
"Nilipozimia, walininyunyizia maji baridi na kunitupa tena kwenye meza."
Miezi miwili baadaye ilitokea tena. Alikuwa amelazimishwa kulipa rubles 50,000 (£ 735) kwa washambuliaji wake na anasema alibakwa katika jaribio la kumnyamazisha kuhusu suala hilo.
Makarov aliambia BBC kuteswa kwake gerezani kumerekodiwa. Wafungwa wanajua picha za kufedhehesha zinaweza kushirikiwa na gereza zima ikiwa hawatatii madai hayo.
Wabakaji walikuwa wafungwa wengine, ambao - Makarov na wengine wana hakika - walifuata maagizo ya wakuu wa magereza.
Muziki ungechezwa kwa sauti kubwa wakati wa vipindi vya mateso, Makarov anasema, ili kuficha mayowe.
Uvujaji wa picha za mwaka jana kutoka Saratov ulichapishwa kwa usaidizi wa mfungwa mwingine wa zamani katika gereza hilo.
Sergey Savelyev alifanikiwa kusafirisha picha za udhalilishaji na unyanyasaji dhidi ya makumi ya wafungwa.
Pia anaamini mateso hayo yameidhinishwa katika viwango vya juu kama sehemu ya mfumo uliopangwa.
Savelyev alipata picha hizo kwa sababu aliombwa kufanya kazi katika idara ya usalama ya gereza lenye wafanyakazi wafupi.
Alihitajika kufuatilia na kuorodhesha picha kutoka kwa kamera za mwilini ambazo kawaida huvaliwa na maafisa wa magereza.
Lakini aliiambia BBC kwamba wakati wa kutesa mfungwa huko Saratov, maafisa wangewafanya wafungwa wafanye kazi yao chafu - na kuwataka wavae kamera za mwili ili kurekodi kwa unyanyasaji huo.
"Ningepata maagizo [ya kutoa kamera za mwili] kutoka kwa mkuu wa usalama," anasema. Aliambiwa kisha kuhifadhi picha zilizorekodiwa za baadhi ya mashambulio haya ili kuonyesha kwa idara ya usalama, na mara kwa mara kuzihamisha kwenye gari ili ziweze kuonyeshwa kwa wafanyakazi wakuu zaidi.
Baada ya kugundua mambo ya kutisha yanayotokea nyuma ya milango iliyofungwa, alianza kunakili faili na kuzificha.
Katika baadhi ya video wanaume wanaotekeleza mateso hayo wanaonekana wakitumia pingu - vifaa, kama kamera za mwilini, ambazo hutolewa kwa wafanyakazi wa magereza pekee.
Savelyev anasema wafungwa wanaofanya unyanyasaji huo, kama sheria ni wale ambao wamepatikana na hatia ya uhalifu wa kutumia nguvu na kwa hivyo wanatumikia vifungo virefu.
Kwa hivyo, wana nia ya kujipendekeza kwa mamlaka ili kutendewa vyema, anasema. Wafungwa wakati mwingine hupewa jina la utani la "pressovschiki".
Wanapaswa kuwa na nia ya kufanya vyema katika kipindi hiki, wakitaka utawala uwe mwaminifu, ili waweze kula vizuri, kulala vizuri na kupata mapendeleo fulani,"
Savelyev anafafanua. Mwanaharakati Vladimir Osechkin ambaye shirika lake la Gulagu.net lilichapisha video zilizovuja, anabainisha itifaki ya kutisha iliyofuatwa na watesaji, iliyonaswa katika video moja mbayo inaashiria kuwa wana uelewa mkubwa wa kile wanachofanya.
"Wanapeana ishara, kutekeleza unyama wao kimya kimya, wanaelewana hata bila maneno kwa sababu wanafuata mfumo uliowekwa vizuri. [Mtu aliyenaswa kwenye kanda hiyo] anatoa ishara za jinsi kumweka sawa mwathiriwa kabla ya kumbaka."
Kufuatia uvujaji wa ushahidi wa Savelyev, pressovschiki sita walikamatwa, lakini walikana kuhusika.
Miezi miwili baadaye mkurugenzi wa hospitali ya gereza ya Saratov na naibu wake pia walikamatwa - wote walikanusha uhusiano wowote na unyanyasaji ulioonyeshwa kwenye video.
Rais wa Urusi Vladimir Putin alichukua nafasi ya mkuu wa huduma ya kitaifa ya magereza na akatangaza kwamba "hatua za kimfumo" zinahitajika ili kuleta mabadiliko.
Sheria ya nchi hiyo ilifanyiwa marekebisho mwezi uliopita ili kutoa adhabu kali kwa kutumia mateso kama njia ya kutumia vibaya mamlaka au kupata ushahidi.
Lakini wanaharakati wa haki za binadamu wanasisitiza kuwa utesaji kama kosa huru bado haujaidhinishwa.
Sio mara ya kwanza kwa Rais Putin kuahidi mabadiliko.
Alitoa ahadi kama hiyo, kufuatia uvujaji wa kwanza wa kushtua wa picha kama hizo, mnamo 2018, ambayo ilionyesha walinzi wakiwapiga vibaya katika gereza la Yaroslavl, kaskazini mwa Moscow.
Wafanyikazi kumi na moja wa gereza la Yaroslavl walipewa adhabu ndogo mnamo 2020 na wakubwa wao wawili waliachiliwa.
Wakili Yulia Chvanova, ambaye ni mtaalamu wa kuwakilisha waathiriwa wa mateso, anasema lengo la unyanyasaji wa kupangwa dhidi ya wafungwa ni ni mbinu inayotumiwa na mamlaka kuwashurutisha kukiri makosa, bila kujali hatia.
Matokeo yake ni kwamba, maafisa wanaohusika na uchunguza uhalifu ndio wachochezi wakuu wa mateso katika magereza ya za Urusi, anasema.
"Kukiri makosa [hupewa umuhimu] kwanza kabisa." Anajaribu kumtafutia fidia Anton Romashov mwenye umri wa miaka 22, ambaye aliteswa mwaka wa 2017 baada ya kukataa kukiri makosa ambayo hakufanya.
Romashov alikuwa amekamatwa kwa kupatikana na bangi lakini polisi walikuwa wakimshinikiza akubali kuhusika na biashara ya dawa za kulevya - kosa kubwa zaidi. Alipokataa kukiri makosa alizuiliwa kabla ya kufunguliw kesi huko Vladimir, magharibi mwa Urusi, mwishoni mwa 2016.
"Nilipelekwa katika [seli] nambari 26. Nilijua ni seli ya aina gani… kwa sababu nilisikia mayowe kutoka hapo, mayowe kwa siku nyingi."
Huko, wanaume wawili walikuwa wakimngojea. Anasema alitupwa sakafuni, mikono na miguu yake ikiwa imefungwa pamoja nyuma, kabla ya kupigwa kwa siku nzima.
Walipoishusha suruali yake chini, alisema atasaini chochote wanachotaka. Alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela, licha ya kuiambia mahakama kuwa alishurutishwa kukiri kosa hilo.
Uchunguzi kuhusu mienendo katika kituo cha kuzuilia wafungwa cha Vladimir hatimaye ulifanyika baada ya mfungwa mwingine kumuua mmoja wa waandishi wa habari wakitishia kumtesa.
Wafanyakazi wa magereza, walioombwa kutoa taarifa, walifichua kwamba wengi wao walijua kilichokuwa kikiendelea katika seli nambari 26 yenye sifa mbaya.
Mfanyakazi wa gereza hilo ambaye alikuwa akiendesha seli ya mateso alihukumiwa katika kesi ambayo Anton na wafungwa wengine wawili walitoa ushahidi.