Shinzo Abe: Waziri Mkuu wa zamani wa Japan auawa kwa kupigwa risasi katika hafla ya kampeni

Waziri mkuu wa zamani wa Japan Shinzo Abe amefariki dunia hospitalini baada ya kupigwa risasi kwenye hafla ya kampeni ya kisiasa, vinasema vyombo vya habari vya ndani.

Bw Abe alipigwa risasi mara mbili alipokuwa akitoa hotuba katika mji wa kusini wa Nara siku ya Ijumaa asubuhi.

Mara moja alianguka na kukimbizwa katika hospitali ya karibu. Picha zilizopigwa eneo la tukio zilimuonyesha akivuja damu.

Maafisa wa usalama katika eneo la tukio walimkabili mshambuliaji huyo, na mshukiwa mwenye umri wa miaka 41 sasa yuko chini ya ulinzi wa polisi.

Katika mkutano na waandishi wa habari wenye hisia kali hapo awali, waziri mkuu Fumio Kishida aliwaambia wanahabari kwamba Bw Abe yuko katika "hali mbaya sana".

“Kwa sasa madaktari wanafanya kila wawezalo,” alisema Bw Kishida ambaye alionekana kuzuia machozi, na kuongeza kwamba “anaomba kutoka moyoni mwake” ili Bw Abe apone.

Pia alilaani shambulizi hilo akisema: "Ni la kinyama na la nia mbaya na haliwezi kuvumiliwa."

Shirika la Kudhibiti Moto na Majanga lilithibitisha kuwa Abe alikuwa na jeraha la risasi upande wa kulia wa shingo yake, na pia alitokwa na damu chini ya ngozi chini ya sehemu ya kushoto ya kifua chake.

Haijulikani ikiwa risasi zote mbili zilimpata, au ikiwa risasi ilimpata shingoni na kutokea kwingine.

Shirika la utangazaji la taifa NHK lilisema Abe alikuwa "na fahamu " alipokuwa akisafirishwa hadi hospitali, akinukuu vyanzo vya polisi.

Lakini pia lilimnukuu mwanachama mkuu wa chama cha Abe akisema hali ya huyo mwenye umri wa miaka 67 ilikuwa ni "ya kusikitisha". Ndugu mdogo wa Bw Abe aliwaambia wanahabari kwamba Waziri Mkuu huyo wa zamani alikuwa akiongezewa damu.

Aliyekuwa gavana wa Tokyo Yoichi Masuzoe alikuwa amesema hapo awali kwenye ujumbe wa Twitter kwamba Bw Abe alikuwa katika hali ya mshtuko wa moyo. Neno hilo mara nyingi hutumika kabla ya kifo kuthibitishwa rasmi nchini Japani.

Walioshuhudia walisema walimwona mtu akiwa amebeba kile walichotaja kuwa bunduki kubwa na kumfyatulia risasi mara mbili Bw Abe kwa nyuma.

Maafisa wa usalama walimzuilia mshambuliaji huyo, ambaye hakujaribu kukimbia, na kunasa silaha yake ambayo iliripotiwa kuwa bunduki iliyotengenezwa kwa mkono.

Mshukiwa ametambuliwa kama mkazi wa Nara Tetsuya Yamagami. Ripoti za vyombo vya habari nchini humo zinasema kuwa anaaminika kuwa mwanachama wa zamani wa Kikosi cha Kujilinda cha Majini cha Japan, ambacho ni sawa na kikosi cha wanamaji.

Hotuba ya Bw Abe ilikuja kama sehemu ya kampeni kwa chama chake cha zamani, Liberal Democratic Party, wakati uchaguzi wa baraza la juu nchini Japan unatarajiwa kufanyika baadaye wiki hii.

Mawaziri kote nchini baadaye waliambiwa warudi Tokyo mara moja, kulingana na ripoti za ndani.

Katika mitandao ya kijamii ya Kijapani, lebo ya reli "Tunataka demokrasia, si vurugu" ilikuwa ikivuma, huku watumiaji wengi wa mitandao ya kijamii wakielezea hofu na kuchukizwa kwao na tukio hilo.