Kwanini ni vigumu kuzuia mali ya Warusi?

Chanzo cha picha, getty
Mvutano wa kisheria juu ya ni nani anayemiliki boti kubwa ya kifahari yaashiria ugumu wa kunyakua mali ya Urusi tangu vita vya Ukraine kuanza.
Wakati waandishi wa BBC walipochunguza kesi ya boti ya Alfa Nero ya pauni milioni 54, iliwapeleka kwa kampuni ya Uingereza ambayo sheria inamruhusu tajiri wa Urusi kudai kwamba boti hiyo kubwa si mali yake hata kidogo.
Wiki hii kesi inaendelea tena mjini Antigua. Ilianzishwa na binti ya bilionea wa Urusi Andrey Guryev kupinga kukamatwa kwa boti ya kifahari ya Alfa Nero.
Serikali ya kisiwa hicho inataka kuuza meli hiyo na kuchukua mapato yake. Hata ilibadilisha sheria kabla ya kuipiga mnada boti hiyo mnamo mwezi Juni mwaka jana.
Hatimaye ilinunuliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa zamani wa Google Eric Schmidt kwa £54m, lakini sasa amejiondoa kwenye zabuni huku kukiwa na pingamizi nyingi za kisheria, ikiwa ni pamoja na ile ya bintiye Bw Guryev.
Anadai kuwa yeye ndiye pekee mnufaika wa watu wazima wa amana inayomiliki boti, badala ya babake bilionea.
Kuchunguza pingamizi hiyo kuliifanya BBC kufichua baadhi ya mali zenye thamani ya £500m zilizounganishwa na bilionea huyo aliyewekewa vikwazo.
Pia ilisaidia kufichua jinsi miundo ya uaminifu inayosimamiwa kihalali na kampuni ya Uingereza kwa miaka mingi inamruhusu Bw Guryev kudai, kufikia wakati alipowekewa vikwazo, kwamba boti hiyo na mali za London ambazo tumetambua si zake hata kidogo.
Uhusiano na Ukraine
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Katika ziara kwenye Bandari ya kipekee ya Falmouth ya Antigua, mfanyakazi wa bandari yuko tayari kuzungumza kuhusu mengi yanayohusu boti ya Alfa Nero, lakini tunapouliza ni nani aliyekuwa akiimiliki, sauti yake inabadilika.
"Sijui," anasema, huku akitazama chini kwenye sitaha inayometa.
Kabla ya boti hiyo kukamatwa mwezi wa Aprili, serikali ya Marekani ilisema ni ya Bw Guryev, ambaye ilimwita "mshirika wa karibu anayejulikana" wa Vladimir Putin.
Hazina ya Marekani inasema Bw Guryev ni sehemu ya kundi la "wasomi wa Kremlin" ambao "huzalisha mapato makubwa kwa serikali ya Urusi".
Bw Guryev alipata utajiri wake kutoka PhosAgro, kampuni ya mbolea aliyoanzisha pamoja na mwenzake kufuatia kuanguka kwa Muungano wa Sovieti.
Kufikia wakati kampuni ya PhosAgro ilipoorodheshwa kwenye Soko la Hisa la London mnamo 2011, Bw Guryev alikuwa amenunua Witanhurst Estate, jumba lililochakaa la Georgia alilolibadilisha na kuwa mojawapo ya majengo ya gharama kubwa zaidi ya London, yanayokadiriwa kuwa na thamani ya £300m.
Majalada ya Nyumba kutoka kwa Makampuni yaliyowasilishwa Mei 2023 yanaonyesha kuwa jumba la Witanhurst, pamoja na Alfa Nero, imeunganishwa kwa familia ya Guryev kupitia anwani iliyoko Guernsey, eneo ambalo liko chini ya mamlaka ya Uingereza lakini sio sehemu ya Uingereza.
Na sio mali pekee ya thamani sana iliyounganishwa na anwani hii katika Visiwa vya Channel.
Luminosity ni mojawapo ya boti kubwa zaidi duniani ya hybrid, yenye urefu wa futi 353 (107.5m). Ina sehemu ambayo ndege aina ya helikopta hutua pamoja na kidimbwi cha kuogelea tofauti na jacuzzi, na wafanyakazi kadhaa.
Muda mfupi baada ya uvamizi wa Urusi kwa Ukraine kuanza, Boti ya Luminosity iliondoka kwenye bandari ya kaskazini mwa Italia hadi Montenegro ambayo haiko chini ya EU mnamo Machi 10.
Hiyo ilikuwa siku baada ya mtoto wa bwana Guryev kuwekewa vikwazo na EU.
Mkaguzi wa serikali alipopanda boti hiyo, waligundua kwamba boti hii kubwa pia iliunganishwa na anwani ile ile ya Guernsey.
'Sio mteja wetu'
Unaposafiri hadi kwenye anwani hiyo, unapata ofisi za msimamizi wa mali anayeitwa Opus Private.
Katika tovuti yake, kampuni hiyo ilisema ilisaidia "baadhi ya watu tajiri zaidi duniani kusimamia na kulinda mali zao".
Pamoja na idadi ya mali zingine, ikiwemo jumba la kifahari la penthouse la Pauni 50m London, tulibaini jumla ya mali ya thamani ya zaidi ya pauni milioni 500 za familia ya Guryev, zote zimeunganishwa na kampuni hii moja.
Tumeona pia hati zinazoonyesha uhusiano huo umekuwa ukiendelea kwa angalau muongo mmoja.
Huko Antigua, uhusiano huo na washiriki wengine wa familia ya Guryev unaendelea.
Nyaraka za mahakama ambazo tumeona zinaonyesha Opus Private ilihusika katika hatua ya kisheria ambayo ilishindwa kuzuia boti ya Alfa Nero kupigwa mnada hapo awali.
Ni muhimu kutambua kwamba ni halali kuendelea kufanya kazi kwa niaba ya mtu aliyewekewa vikwazo, kwa ruhusa ya serikali, na bintiye Bw Guryev hajawekewa vikwazo na Uingereza, EU au Marekani.
Nyaraka ya mahakama inaeleza kwa kina jinsi umiliki wa boti ya kifahari ilivyounganishwa katika dhamana, ambayo hakimu huko Antigua alipendekeza Bw Guryev bado ana uwezo wa kudhibiti.
Tunajua kumekuwa na mabadiliko katika wanufaika wa mdhamini, lakini hatuwezi kubainisha kwa kujitegemea wakati yalifanyika. Ikiwa ni baada ya kuwekewa vikwazo, itakuwa ni kinyume na sheria; kama ilikuwa hapo awali, haitakuwa hivyo.
Binti ya Bw Guryev na Opus walituambia ilifanyika kabla ya babake kuwekewa vikwazo.
Opus pia alisisitiza kuwa Bw Guryev hakuwa mteja wao kwa vile hakuwa mnufaika wa mdhamini tena.
Lakini kampuni hiyo inasema imefanya mamlaka ya Uingereza na Guernsey kufahamu kuhusu mali ya mdhamini inayozichukulia kuwa zilizozuiliwa kulingana na vikwazo vya Uingereza dhidi ya Bw Guryev.
Inasema inachukulia mali hizi kama zenye kuzuiliwa kwa sababu, wakati Bw Guryev si wanufaika wa mdhamini, anachukuliwa kuwa na "udhibiti" juu yake chini ya sheria ya vikwazo vya Uingereza.
Mtazamo tofauti sana Ukraine

Chanzo cha picha, bbc
Mali hizi zinafuatiliwa kwa karibu nchini Ukraine, ambapo gharama ya uharibifu wa vita inakadiriwa kuwa zaidi ya £300bn, na kupanda.
"Tumekuwa tukichukua kwa nguvu mali za watu wa Urusi," anasema Vlad Vlasiuk, mshauri wa vikwazo wa rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky.
Siyo tu kwamba Ukraine imewawekea vikwazo takriban watu na makampuni 9,000, imechukua hatua zaidi kuliko washirika wake wengi kutoka kuzuilia hadi kutwaa mali. Miongoni mwa waliowekewa vikwazo na Ukraine ni Bw Guryev, kijana wake, mkewe na bintiye.
"Tunafikiri kwamba Bw Putin anatumia sekta ya mbolea kwa silaha na kutishia dunia nzima katika suala la usalama wa chakula duniani. Hatutaki hilo lifanyike," Bw Vlasiuk anasema.
Tangu vikwazo vilipowekwa, Guryev na kijana wake wa kiume, wote wamejiuzulu nyadhifa zao katika kampuni ya PhosAgro, lakini familia inasalia kuwa washikadau wakuu.
Kampuni hiyo - inayofanya kazi kimataifa – imeweka rekodi katika mauzo yake tangu uvamizi huo, na Guryev na kujana wake wa kiume hata walikutana na Rais Putin mwezi Aprili kujadili sekta ya mbolea.











