Kwanini Sabasaba ni zaidi ya siku Afrika Mashariki?

Chanzo cha picha, eac
- Author, Na Yusuph Mazimu
- Akiripoti kutoka, BBC Dar es Salaam
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Kama kuna tarehe moja tu ambayo inaweza kuwakilisha uhuru, mapinduzi, demokrasia, lugha ya Afrika, na umoja wa kikanda, basi tarehe hiyo ni Julai 7 yaani Saba Saba.
Tarehe 7 Julai, inayojulikana sana kama Saba Saba, ni mojawapo ya tarehe muhimu zaidi katika historia ya Afrika Mashariki. Kwa mataifa kadhaa ya ukanda huu, Saba Saba ni alama ya harakati za kisiasa, mabadiliko ya kijamii, ujenzi wa taasisi za umoja wa kikanda.
Lakini Sabasaba pia utambulisho wa lugha ya Kiswahili kama kiungo cha kimaendeleo na utambulisho wa Waafrika.
Makala hii inaangazia maana tofauti tofauti na umuhimu wa ya tarehe hii katika nchi mbalimbali za Afrika Mashariki hasa Tanzania, Kenya, Uganda, pamoja na muktadha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Siku ya Kiswahili duniani.
Tanzania: Saba Saba ni Uhuru, ni biashara

Chanzo cha picha, Getty Images
Tarehe 7 Julai 1954, chama cha Tanganyika African National Union (TANU) kilianzishwa jijini Dar es Salaam kikiongozwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. TANU kilichukua nafasi ya chama kilichotangulia cha African Association, kikiwa na malengo ya wazi: kupigania uhuru kamili wa Tanganyika kutoka kwa Waingereza.
Kwa hiyo Watanzania, Saba Saba haikuwa tu siku ya kuzaliwa kwa chama bali ni siku ya kuamka kisiasa kwa taifa zima. Ndani ya miaka saba, TANU kilifanikiwa kuunganisha nguvu za wananchi na kufanikisha uhuru wa Tanganyika mnamo 9 Desemba 1961. Mwaka 1977 ikazaliwa CCM, baada ya TANU kuungana na chama cha ASP.
Kwa mantiki hiyo, Saba Saba ni kielelezo cha mwanzo wa safari ya kujitawala kwa taifa la Tanzania.
Kwa watanzania, Saba Saba pia imehusishwa na Maonesho ya biashara ya kimataifa, ishara ya maendeleo ya kiuchumi na ujamaa wa Mwalimu Nyerere.
Hata hivyo, kwa baadhi ya wanaharakati, maana ya Saba Saba imekuwa ikigeuka, kutoka siku ya sherehe hadi fursa ya kutafakari uhuru wa kweli wa kisiasa, haki za kiraia, na nafasi ya upinzani ndani ya mfumo wa vyama vingi ulioanza rasmi mwaka 1992.
Kenya - Saba saba ni siku ya mageuzi ya demokrasia

Chanzo cha picha, Kenyans
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mnamo tarehe 7 Julai 1990, Kenya ilishuhudia moja ya maandamano makubwa zaidi ya kupinga mfumo wa chama kimoja. Viongozi kama Kenneth Matiba, Charles Rubia na Jaramogi Oginga Odinga waliitisha mkutano katika uwanja wa Kamukunji jijini Nairobi kudai kurejeshwa kwa demokrasia ya vyama vingi.
Walijumuiika na wananachi wengine walioandamana kutaaka mfumo wa vyama vingi nchini humo, wakilalamikia ukandamizaji wa kisiasa wa utawala wa KANU chini ya Rais Daniel Arap Moi.
Maandamano hayo ya Saba Saba yalizimwa kwa nguvu kubwa na vyombo vya dola, yakiambatana na vifo, majeruhi na ukamataji wa wanaharakati.
Hata hivyo, kilio hicho kilisababisha presha kubwa ya kimataifa na ya ndani, na hatimaye Kenya ilikubali mfumo wa vyama vingi mwaka 1991.
Kwa Wakenya wengi, Saba Saba ni siku ya kuenzi mapambano ya kidemokrasia na uthubutu wa wananchi dhidi ya udikteta wa kisiasa. Ingawa madai kadhaa yanaonekana hayajafanikiwa kwa kiwango kinachotajwa na wapinzani ikiwemo maisha yasiyo magumu, angalau hali ya demokrasia iliyokuwepo sasa inatokana na jitihada zinazokumbukwa katika siku hii ya Sabasaba.
Uganda - Saba Saba ni mapinduzi ya kisiasa

Chanzo cha picha, Getty Images
Japo haina umaarufu sana kama ilivyo Kenya na Tanzania, nchini Uganda, Saba Saba pia inahusishwa na mabadiliko makubwa ya utawala. Tarehe 7 Julai 1985, kulifanyika mashambulizi makubwa zaidi ya kijeshi yaliyopelekea kundi la wanajeshi linaloongozwa na Tito Okello kupindua serikali ya Rais Milton Obote siku 20 baadaye (Julai 27, 1985). Wegi wanaikumbuka Julai 27 zaidi kwa sababu ndiko siku ya mapinduzi yaliyoonekana ya ghafla kwa siku hiyo..ingawa tukio mla Julai 7, 1985 lilijenga misingi ya mapinduzi hayo.
Ingawa utawala huo wa kijeshi haukudumu kwa muda mrefu, ulifungua njia kwa kuingia madarakani kwa Yoweri Museveni na chama chake cha NRM (National Resistance Movement) mnamo Januari 1986.
Hivyo, kwa Uganda, Saba Saba ina maana ya mabadiliko ya mfumo wa utawala, kutoka enzi ya Obote hadi enzi ya Museveni na chama chake cha NRM ambacho bado kiko madarakani hadi leo. Hata hivyo, tafsiri ya siku hiyo ni yenye mchanganyiko, kwani mabadiliko hayo hayakutokana na mapenzi ya wananchi moja kwa moja, bali nguvu ya kijeshi. Ingawa baadaye Museveni alishinda chaguzi kadhaa za kidemokrasia zinazomuweka madarakani hadi leo, akitangaza tena kugombea urais katika uchaguzi Mkuu ujao, wa Januari, 2026.
Kuzaliwa upya kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki

Chanzo cha picha, EAC
Tarehe 7 Julai 2000, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ilizaliwa upya baada ya kuvunjika mwaka 1977 kutokana na tofauti za kisiasa na kiuchumi kati ya wanachama wa awali ,Tanzania, Kenya, na Uganda. Uzinduzi wa EAC mpya ulifanyika mjini Arusha, Tanzania.
Saba Saba hii mpya iliwakilisha ahadi ya ushirikiano mpya wa kiuchumi, kijamii, na kisiasa. Hadi sasa, EAC imekua na kujumuisha nchi kama Rwanda, Burundi, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), na Sudan.
Maono yake ni kufanikisha soko la pamoja, sarafu moja, na hatimaye shirikisho la kisiasa.
Kwa hiyo, Saba Saba inaendelea kuishi kama ishara ya mshikamano wa kikanda si tu historia ya kitaifa, bali ndoto ya Umoja wa Afrika Mashariki.
Siku ya Kiswahili duniani
Mnamo Novemba 2021, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) liliitambua rasmi tarehe 7 Julai kuwa Siku ya Kiswahili duniani. Hii ilianza kuadhimishwa rasmi mwaka 2022.
Sababu kubwa ya kuchagua tarehe hii ni mchango mkubwa wa TANU na serikali ya Tanganyika (baadaye Tanzania) katika kukuza Kiswahili kama lugha ya ukombozi, mawasiliano ya umma, na lugha ya kitaifa.
Kiswahili pia kimekuwa lugha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Umoja wa Afrika, na kimepenya hadi Umoja wa Mataifa.
Leo hii, Kiswahili kimevuka mipaka ya Afrika Mashariki na kuzungumzwa na zaidi ya watu milioni 200 duniani.
Kutambuliwa kwake kimataifa katika tarehe hii kunaongeza uzito wa Saba Saba kama siku ya fahari ya utambulisho wa Waafrika.














