Maandamano ya Saba saba Kenya: Watu 10 wauwa na wengine 29 kujeruhiwa- Shirika la haki za binadamu Kenya

Barabara kuu za jiji la Nairobi na mitaa imefungwa siku nzima huku idadi kubwa ya polisi wakionekana kukabiliana na waandamanaji na kushika doria katika maeneo mbali mbali ya nchi.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma & Dinah Gahamanyi

  1. Na mpaka hapo ndito tunafikia mwisho wa matangazo haya ya mubashara kwa leo, shukran kwa kuwa nasi.

  2. Habari za hivi punde, Maandamano ya Saba saba Kenya: Watu 10 wauwa na wengine 29 wamejeruhiwa - Shirika la haki za binadamu Kenya

    Shirika la kutetea haki za binadamu nchini Kenya (KNCHR) limesema kuwa watu 10 wamefariki huku 29 wakijeruhiwa. Watu wawili wamekamatwa na 37 kukamtwa katika kaunti 17.

    Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, shirika hilo limesema limeshuhudia kuwekwa kwa vizuizi vya polisi vilivyovuruga matembezi ya watu hususan katika jiji la Nairobi. Vizuizi vingine viliwekwa kwenye kaunti za Kiambuu, Meru , Kisii, Nyeri , Nakuu na Embu, imesema taarifa ya KNCHR.

    Shirika hilo la haki za binadamu la Kenya limelaumu ukiukwaji wa polisi wa amri ya Mahakama Kuu inayowataka maafisa wote wanaohusika na udhibiti wa maandamano kuwa wamevalia sare ya polisi, huku likisema limeshuhudia maafisa wa polisi waliovalia sweta zilizofunika nyuso zao(hood), katika maeneo ya Kaunti za Nairobi, Kajiado na Nakuru na Eldoret.

    Jijini Nairobi shirika hilo linasema watu waliovalia sweta zenye kofia walionekana kushirikiana na polisi.

    Shirika hilo limelaani kushambuliwa kwa ofisi ya haki za binadamu jijini Nairobi na kushambuliwa kwa wafanyakazi wake na raia Jumapili waliokuwa wakiandaa maandamano.

    Limeitaka serikali kuacha unyanyasaji dhidi ya mashirika ya kiraia na watetezi wa haki za binadamu.

    Unaweza pia kusoma:

  3. Waziri wa Uchukuzi wa Urusi Roman Starovoit, ambaye aliondolewa kwenye wadhifa wake, amepatikana akiwa amefariki

    g

    Chanzo cha picha, Vladimir Smirnov/TASS

    Maelezo ya picha, Starovoit alikuwa na umri wa miaka 53.

    Roman Starovoit, ambaye aliondolewa katika wadhifa wake kama waziri wa uchukuzi leo amefariki dunia. Kulingana na habari za awali, alijiua, Kamati ya Uchunguzi ya Urusi ilisema.

    Mapema Jumatatu, Rais wa Urusi Vladimir Putin alitia saini amri ya kumfukuza Starovoit kutoka wadhifa wake kama mkuu wa Wizara ya Uchukuzi ya Urusi, ambayo alikuwa ameshikilia kwa zaidi ya mwaka mmoja. Kabla ya hapo, alikuwa amehudumu kama gavana wa eneo la Kursk kwa zaidi ya miaka mitano.

    Aleksey Smirnov aliteuliwa kaimu gavana baada ya Starovoyt; baadaye alishtakiwa kwa udanganyifu unaohusisha rubo bilioni 1 zilizotengwa kwa Shirika la Maendeleo la Mkoa wa Kursk kwa ajili ya ujenzi wa ngome kwenye mpaka na Ukraine.

    Unaweza pia kusoma:

  4. Waziri wa polisi wa Afrika Kusini ashutumiwa kwa uhusiano na magenge ya uhalifu

    g

    Chanzo cha picha, Gallo via Getty Images

    Maelezo ya picha, Waziri anayehusika na masuala ya polisi Senzo Mchunu ametupilia mbali madai hayo aliyoyataja kama ya kinyama

    Waziri wa polisi nchini Afrika Kusini Senzo Mchunu ameshutumiwa kwa kuwa na uhusiano na magenge ya wahalifu na kuingilia uchunguzi wa polisi kuhusu mauaji yaliyochochewa na siasa.

    Madai haya yalitolewa na mkuu wa polisi wa KwaZulu-Natal Nhlanhla Mkhwanazi katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumapili.

    Alisema Bw Mchunu alikuwa akipokea usaidizi wa kifedha kutoka kwa mfanyabiashara anayedaiwa kuwa fisadi ili kufadhili "juhudi zake za kisiasa".

    Bw Mchunu tangu wakati huo amekanusha kile anachosema ni "madai ya kipumbavu" huku Rais Cyril Ramaphosa akisema "yanatia wasi wasi mkubwa wa usalama wa taifa" na "yanapewa kipaumbele cha juu zaidi".

    Jenerali Mkhwanazi alielezea kwa kina mlolongo wa matukio anayodai yalisababisha kuvunjwa kwa jopo kazi lililoundwa mwaka wa 2018 kuchunguza mauaji ya wanasiasa, hususan KwaZulu-Natal.

  5. Habari za hivi punde, Maandamano ya saba saba Kenya: Raila ashindwa kufika katika uwanja alikotarajia kuuhutubia Umma

    Kiongozi mkongwe wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM), Raila Odinga amesema vizuizi vya polisi jijini ndio sababu iliyomfanya ashindwe kufika uwanja wa kihistoria wa Kamukunji kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 35 ya maandamano ya Sabasaba.

    Raila ambaye badala yake kwa sasa anahutubia kutoka katika hoteli moja jijini Nairobi , amekuwa akielezea historia yake na wanasiasa na wanaharakati wenzake katika juhudi za kupigania mfumo wa siasa ya vyama vingi.

    Ameelezea kuwa katika juhudi hizo alifungwa kwa miaka 6, na utawala wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Hayati Daniel Arap Moi.

    Amesema inasikitisha kuwa maadhimisho ya Saba Saba yamekuwa hayaadhimishwi mara kwa mara.

    Raila anahutubia huku Kenya ikikumbwa na makabiliano makubwa baina ya waandamanaji wa Gen Z na maafisa wa usalama katika uwanja wa Kamukunji jijini Nairobi.

    Kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga alikuwa amewahimiza Wakenya kukusanyika katika uwanja wa Kamukunji jijini Nairobi siku ya Jumatatu kuadhimisha kumbukumbu ya maandamano ya kihistoria ya Saba Saba.

    Unaweza pia kusoma:

  6. Tazama: Video ya droni inayoonyesha athari za mafuriko Texas yaliyowauwa watu 81

    Maelezo ya video, Picha za video zilizochukuliwa na droni zinaonyesha maafa ya mafuriko katika jiji la Georgetown, Texas

    Takriban watu 81 wamekufa na wengine kadhaa kupotea katika mafuriko huko Texas huku mvua zaidi ikiendelea kunyesha.

    Picha za video zilizochukuliwa na droni zinaonyesha maafa ya mafuriko katika jiji la Georgetown, Texas.

    Wengi wa walioaga dunia walikuwa katika Kaunti ya Kerr, ambapo kambi ya wasichana wa Kikristo iliyopo kando ya mto ilifurika, na kusababisha vifo vya watoto kadhaa na kuwaacha wengine wasijulikane walipo.

    Maeneo mengine yaliyorekodi vifo ni pamoja na Kaunti ya Travis, Kaunti ya Burnet, Kaunti ya Williamson, Kaunti ya Kendall na Kaunti ya Tom Green.

    Takwimu zinabadilika haraka huku waokoaji wakiendelea kutafuta waliotoweka, na maafisa wanasema idadi ya waliofariki ni hakika itaendelea kuongezeka. Miili mingi bado haijatambuliwa rasmi.

  7. Habari za hivi punde, Maandamano ya saba saba Kenya: Vurugu zatawala eneo analotarajia kufanya mkutano Raila

    h

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Kiongozi wa ODM, Raila Odinga, akiwa katika muungano wa Azimio La Umoja , alipokuwa akiwasili i kwenye mkutano wa hadhara kuhusu mswada wa fedha za serikali, katika viwanja vya Kamukunji jijini Nairobi, Kenya, 28 Juni 2023

    Kumekuwa na makabiliano makubwa baina ya waandamanaji wa Gen Z katika uwanja wa Kamukunji jijini Nairobi -mahala ambapo kiongozi mkongwe wa Orange Democratic Movement (ODM), Raila Odinga anatarajiwa kufanya mkutano leo.

    Kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga amewahimiza Wakenya kukusanyika katika uwanja wa Kamukunji jijini Nairobi siku ya Jumatatu kuadhimisha kumbukumbu ya maandamano ya kihistoria ya Saba Saba.

    Polisi wameonekana wakiwatupia vitoa machozi na maji vijana waliokuwa wamekusanyika kwenye Uwanja wa Kamukunji ambao walijibu kwa kuchoma moto mataili na kuwatupia mawe.

    Akihutubia wanahabari siku ya Jumapili, mwanasiasa huyo wa muda mrefu wa upinzani alisema itikadi za vuguvugu hilo bado hazijatimizwa.

    Odinga alisema nchi inaendelea kukabiliwa na masuala mengi yale yale ambayo yalisababisha maandamano ya kwanza ya Saba Saba mwaka 1990, ikiwa ni pamoja na matatizo ya kiuchumi na ukiukwaji wa haki za binadamu.

    Pia unaweza kusoma:

  8. Uchunguzi wa mauaji waanza baada ya kifo cha mwanasayansi mwenye asili ya Afrika

    h

    Chanzo cha picha, Police Scotland

    Maelezo ya picha, Dk Fortune Gomo alimaliza Shahada ya Uzamifu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Dundee mnamo 2022

    Mwanamume mmoja amefunguliwa mashtaka kuhusiana na kifo cha mwanasayansi aliyepatikana akiwa amejeruhiwa vibaya katika mtaa wa Dundee.

    Dk Fortune Gomo, 39, ambaye asili yake ni Zimbabwe, alitangazwa kufariki katika eneo la tukio kwenye Barabara ya Kusini mwendo wa saa mumi 12.12 Jumamosi.

    Mshukiwa huyo mwenye umri wa miaka 20 atafikishwa mbele ya Mahakama ya Dundee baadaye.

    Kufuatia uchunguzi wa maiti, Polisi wa Uskochi walisema kifo hicho kilikuwa kikichukuliwa kama mauaji.

    Dk Gomo, ambaye alifanya kazi katika idara ya Maji ya Uskochi alikuwa mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dundee.

    Profesa Nigel Seaton, mkuu wa muda na naibu-chansela, alisema chuo kikuu "kilishtushwa" na kifo cha kifo chake.

  9. Maandamano Kenya: Mamia wakosa nauli ya ziada kuweza kuingia jijini

    Mamia ya abiria walioingia jijini Nairobi usiku wa kuamkia leo, wamelazimika kusalia kwenye magari baada ya barabara kuu zinazoingia jijini kufungwa.

    Wengi wao hawawezi kulipa gharama ya ziada kwa ajili waendeshaji wa pikipiki kuwafikisha ndani ya jiji.

    Tazama hali ilivyo katika picha.

    .
    .
    .
    .
    .

    Soma zaidi:

  10. Maandamano Kenya: Milipuko ya mabomu ya kutoa machozi yasikika Nairobi huku wanaandamanaji waking’ang’ana kuingia jijini

    g

    Wakazi wa jiji la Nairobi wamekuwa wakisikiliza milio ya mabomu ya kutoa machozi ikilipuliwa tangu asubuhi kutoka barabara kuu ambako makundi ya vijana wamekuwa waking’ang’ana kulazimisha kupita ili kulifikia eneo la katikati ya jiji.

    Hali ya taharuki imetanda kote katika jiji kuu la Kenya nairobi, huku polisi wakikabiliana na waandanamanaji vijana wa Gen Z wanaotaka kuingia mjini humo kuelezea kero zao.

    Maandamano haya yanafanyika katika siku ya Saba Saba, inawakilisha tarehe 7 Julai, siku inayotumika kama ukumbusho mkubwa wa kujitolea kwa Wakenya katika mapambano ya demokrasia ya vyama vingi.

    Wafanyabiashara wamelazimika kufunga biashara zao yakiwemo maduka ili kuepuka wizi na uharibifu wa mali zao unaotawala kila mara maandamano yanapofanyika jijini.

    Kwa kiasi kikubwa polisi wameweza kudhibiti maandamano hayo kwa kuwazuia vijana wa Gen Z kuingia jijini.

    g

    Polisi wameweka vizuizi katika barabara zote zinazoingia jijini, kupiga doria kwa helikopta za kijeshi na kuzuia safari zote za kuelekea jijini, isipokuwa usafiri wa pikipiki.

    Baadhi yao wafanyabiashara kuchukua jukumu la kulinda mali zao dhidi ya majangili wanaoambata na wandamanaji na kuiba mali zao

    Awali Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Gilbert Masengeli alikanusha madai kwamba Wakenya wanazuiwa kuingia katikati ya jiji la Nairobi, akisema watu wanaendelea kwenda jijini bila vikwazo.

    Huduma ya Kitaifa ya Polisi imetoa wito kwa Wakenya kudumisha amani na kujizuia wakati wa siku ya Saba Saba hii leo 07/07/2025.

    Katika taarifa ya polisi kuhusu maandimisho ya Saba Saba iliyotolewa hapo jana, polisi ilitoa hakikisho la kujitolea kwao kulinda maisha na mali ya Wakenya wote, kudumisha amani, sheria, na utaratibu.

    Hali ya taharuki pia imetipotia katika baadhi ya miji mingine mikubwa nchini Kenya, huku usafiri ukidorora au kufungwa kabisa.

    Pia unaweza kusoma:

  11. Mbunge wa Nairobi asitisha mswada wenye utata wa Maandamano

    .

    Chanzo cha picha, Courtesy

    Maelezo ya picha, Mwakilishi wa Wanawake mjini Nairobi Esther Passaris

    Mwakilishi wa Wanawake katika mji wa Nairobi Esther Passaris ametangaza kuwa atasitisha uchapishaji wa Mswada tata wa Maandamano, Mswada wa Marekebisho ya Utaratibu wa Umma wa 2025.

    Akizungumza kwenye mtandao wa kijamii na kunukuliwa na gazeti la mtandaoni la The Citizen Kenya siku ya Jumatatu, mbunge huyo amesema kuwa kusitishwa huko kutafungua njia kwa mazungumzo ya kitaifa na ushirikishwaji wa umma kuhusu Mswada huo.

    "Huu ni mwaliko wa kuunda sheria kwa pamoja ambayo inalinda uhuru wa kikatiba huku tukihakikisha utulivu wa umma," aliandika.

    "Jamii yenye uadilifu haijengwi kwa nguvu au woga, bali kwa uwajibikaji wa pande zote kutoka kwa wananchi hadi maafisa wa serikali. Ni matumaini yangu kwamba mazungumzo haya yatabadilika kutoka makabiliano hadi ushirikiano."

    Hatua yake inajiri kama kutii wito wa Baraza la Kitaifa la Makanisa ya Kenya (NCCK) kuondoa Mswada huo kabla ya maandamano yaliyopangwa ya Saba Saba.

    Mswada huo unalenga kupiga marufuku mikusanyiko ya watu Bungeni na maeneo mengine yaliyohifadhiwa pamoja na kuweka mipaka ya maeneo ya mikusanyiko na maandamano ili kuzuia uharibifu wa mali.

  12. Israel yaanzisha mashambulizi katika maeneo lengwa ya Wahouthi huko Yemen

    .

    Chanzo cha picha, Mohammed Hamoud/Getty Images

    Israel inasema imeanzisha mashambulizi kwenye bandari tatu na kiwanda cha nguvu za umeme katika maeneo yanayodhibitiwa na Wahouthi ya Yemen.

    Waziri wa Ulinzi wa Israel Israel Katz alithibitisha wanacholenga ikiwa ni pamoja na meli ya kibiashara ya Galaxy.

    Meli hiyo, iliyotekwa nyara na kikundi cha waasi mnamo 2023, ilitumiwa kufuatilia vyombo vya baharini katika maji ya kimataifa, Israel ilisema.

    Baada ya mashambulizi ya Israel kwenye bandari za Hudaydah, Ras Isa na Saif, makombora mawili yalirushwa kutoka Yemen hadi Israel, kwa mujibu wa jeshi la Israel.

    Msemaji wa kundi la kijeshi la Houthi linaloungwa mkono na Iran alisema kufuatia mashambulizi hayo, walinzi wa anga wa kundi hilo walikabiliana na shambulio la Israel kwa kutumia "idadi kubwa ya makombora ya kutoka ardhini hadi angani yaliyotengenezwa nchini humo".

    Ving'ora vilisikika katika maeneo kadhaa ya Israel kujibu makombora hayo, huku jeshi likisema matokeo ya uvamizi huo yanachunguzwa.

    Vyombo vya habari vinavyoongozwa na Houthi nchini Yemen vilisema mashambulizi ya Israel yalishambulia Hudaydah, lakini hakuna maelezo zaidi yaliyotolewa kuhusu uharibifu au majeruhi.

    Soma zaidi:

  13. Fahamu historia ya Maandamano ya Saba Saba Kenya

    .

    Chanzo cha picha, Anadolu via Getty Images

    Maelezo ya picha, Polisi wakikabiliana na Waandamanaji Kenya

    Kila mwaka ifikiapo Julai 7, Kenya huadhimisha Saba Saba,kama siku iliyokita mizizi katika mapambano ya muda mrefu ya demokrasia .

    Kilichoanza mwaka wa 1990 kama maandamano ya kijasiri dhidi ya utawala wa chama kimoja wa rais wa awamu ya pili Kenya Rais Daniel Arap Moi kimekua na kuwa ishara yenye nguvu ya upinzani, uharakati wa raia, na mapambano yanayoendelea ya haki.

    Saba Saba, inawakilisha tarehe 7 Julai, na inatumika kama ukumbusho mkubwa wa kujitolea kwa Wakenya katika mapambano ya demokrasia ya vyama vingi.

    Historia ya Saba Saba

    • Mwaka 1990, Kenya ilikuwa ikifanya kazi chini ya mfumo wa chama kimoja ulioongozwa na hayati Rais Daniel Arap Moi kupitia cha kimoja cha KANU.
    • Upinzani wa kisiasa ulipigwa marufuku, na uhuru wa vyombo vya habari ukawekewa vikwazo vikali. Zaidi ya hayo, kuchanganyikiwa kwa umma kuliongezeka, kutokana na usimamizi mbaya wa kiuchumi na kutengwa kwa jamii fulani.
    • Mnamo Julai 7, 1990, viongozi wa upinzani Kenneth Matiba, Charles Rubia, na Jaramogi Oginga Odinga waliitisha mkutano katika uwanja wa Kamukunji jijini Nairobi kudai kurejeshwa kwa demokrasia ya vyama vingi.
    • Hata hivyo, serikali ilipiga marufuku mkutano huo, na waandamanaji walikaidi marufuku hiyo, ambayo ilisababisha machafuko makubwa katika jiji hilo.
    • Wakati wa maandamano hayo, polisi wa kutuliza ghasia waliwatawanya waandamanaji kwa nguvu, na kusababisha kukamatwa, kuwekwa kizuizini bila kesi na vifo miongoni mwa Wakenya wengi. Matukio ya siku hiyo yakawa hatua ya mabadiliko katika mapambano ya Kenya ya mageuzi ya kidemokrasia.
  14. Maandamano ya Saba Saba Kenya: Polisi wakanusha madai ya kufungwa kwa eneo la katikati ya jiji

    ..

    Chanzo cha picha, National Police Sservice NPS

    Maelezo ya picha, Naibu Inspekta Jenerali mkuu wa polisi Gilbert Masengeli

    Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi (DIG) Gilbert Masengeli amekanusha madai kwamba Wakenya wanazuiwa kuingia katikati ya jiji la Nairobi, akisema kuingia jijini kunasalia bila vikwazo.

    Akizungumza Jumatatu, Masengeli aliwataka wananchi kuzingatia sheria na kufanya maandamano yoyote kwa amani.

    "Kila mtu anaingia kazini bila masuala yoyote. Hakuna anayezuiwa kuingia," alisema.

    "Tunawahimiza kuhakikisha maandamano yao yanasalia kuwa ya amani."

    Licha ya hakikisho hilo, madereva wa magari ya Nairobi walikabiliwa na matatizo makubwa Jumatatu asubuhi huku polisi wakiweka vizuizi vingi kwenye njia kuu za kuingia na kutoka jijini.

    Vizuizi hivyo viliathiri magari ya kibinafsi na ya huduma za umma (PSVs), na kuwaacha wasafiri wengi wakikwama.

    Magari ya dharura pekee na yale ya serikali ndiyo yaliruhusiwa kupita.

    Biashara kadhaa kuu katikati ya jiji ziliwekewa milango ya chuma huku kukiwa na hofu ya uwezekano wa uporaji.

  15. Maandamano Kenya: Polisi waonya waandamanaji dhidi ya kuingia maeneo yaliyopigwa marufuku

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Huduma ya Kitaifa ya Polisi imetoa wito kwa Wakenya kudumisha amani na kujizuia wakati wa siku ya Saba Saba hii leo 07/07/2025.

    Katika taarifa ya polisi juu ya Saba Saba iliyotolewa hapo jana, polisi ilitoa hakikisho la kujitolea kwao kulinda maisha na mali ya Wakenya wote, kudumisha amani, sheria, na utaratibu.

    "Wakati katiba chini ya kifungu cha 37, inatoa haki kwa Wakenya kukusanyika kwa njia ya amani, kuandamana na kuwasilisha maombi, haki hii inafaa kutekelezwa chini ya sheria," Taarifa ilisema.

    Polisi walisema waandamanaji wadumishe amani na kwamba kubeba silaha za aina yoyote itachukuliwa kuwa ukiukaji wa moja kwa moja wa katiba.

    Pia, waandamanaji wameonywa dhidi ya kuingia au kujaribu kuingia katika vituo vya serikali vilivyolindwa au maeneo yaliyopigwa marufuku, wakisema ni ukiukaji wa Sheria ya Maeneo Yanayolindwa.

    "Uporaji, uharibifu wa aina yoyote wa mali, kuzuia barabara, au hata kuchochea vurugu chini ya maandamano hakutavumiliwa. Vitendo kama hivyo ni vya jinai na vitakabiliwa kisheria," Taarifa hiyo ilisema.

    Taarifa hiyo inawadia huku watu katika maeneo mbali mbali wakipanga kuandamana katika kumbukumbu ya Saba Saba.

    Jijini Nairobi hali tofauti imeshuhudiwa, wanaokwenda kazini wakipata shinda ya usafiri wa umma, magari yakizuiwa kuingia jijini huku maafisa wa usalama wakiendelea kushuhudiwa sehemu tofauti tofauti.

    Pia unaweza kusoma:

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Hali ilivyokuwa katika maandamano ya mwaka jana mwezi Julai
  16. Maandamano Kenya: Barabara kuu zote za kuingia Nairobi zafungwa

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Barabara zote za kuingia jiji Nairobi zimefungwa huku usalama ukimarishwa katika maeneo mbali mbali wakati ambapo maandamano yanatarajiwa siku hii ya kumbukumbu ya Saba Saba.

    Kuna vizuizi vilivyowekwa ambapo magari hayaruhusiwi kupita eneo hilo kuingia jijini na idadi kubwa ya polisi wa kushika doria inaendelea kushuhudiwa katika maeneo mbali mbali.

    Maeneo mengine kama vile daraja la Kangemi, mabasi hata yaliyotoka safari za mbali ama mfano yalioingia jijini asubuhi hii kutoka nchi jirani hayaruhusiwi kupita daraja hilo, hivyo, abiria wanalazimika kushuka eneo husika na kutembea kwa miguu kuingia mjini au kufikiria mbinu za kufika makwao.

    .

    Kuzuiwa kwa usafiri wa magari ya umma kuingia mjini, idadi ndogo tu ya usafiri ndio inayoshuhudiwa barabarani hasa pikipiki na tuktuk.

    Vile vile, biashara nyingi zimefungwa katika barabara mbalimbali za mjini kama vile Moi Avenue.

    Jana usiku, 06/07/2025, abiria waliachwa njia panda katika mji wa Mombasa baada ya serikali kusitisha usafiri wa SGR kwenye kituo cha Miritini.

    Hilo lilitokea baada ya polisi kufunga barabara ya Dongo Kundu kwa waliokuwa wakisafiri kutoka kaunti ya Kwale na baadhi kukosa usafiri wa SGR wa saa nane.

    Soma zaidi:

  17. Serikali Kenya yaonya waandamanaji watakaofanya vurugu

    .

    Chanzo cha picha, AFP

    Waziri wa Usalama nchini Kenya Kipchumba Murkomen ametoa wito wa kufanyika kwa maandamano ya amani kabla ya maandamano yaliyopagwa hii leo katika kumbukumbu ya Saba Saba.

    Akizungumza katika Kaunti ya Meru Jumapili, Murkomen ilielezea wasiwasi wake juu ya mwenendo wa hivi karibuni wa maandamano ya vurugu ambapo mali za umma kama vile vituo vya polisi na mahakama zimeteketezwa moto na kuwataka polisi kukabiliana na waandamanaji wenye vurugu.

    "Nimewaambia askari wetu wawe wapole kama njiwa, wawe wapole na wazuri kwa wananchi, lakini kama ni kupambana na majangili na wale ambao wanataka kuharibu mali ya umma, wale ambao wanataka kuua wananchi wengine au polisi, wawe wakali sana kuhakikisha amani inadumishwa," Murkomen alisema.

    Akizungumzia jinsi ambavyo mwenendo wa polisi umekuwa ukitia umma wasiwasi, Murkomen alisema hilo limechangiwa na machafuko ya waandamanaji ambayo yamekuwa yakishuhudiwa.

    "Wanasema polisi wamefanya hivi na vile. Lakini wale ambao wanasababisha matatizo na wale wanaotumia vurugu kufanya siasa ndio wanaoharibu nchi yetu," Waziri wa Usalama aliongeza.

    Murkomen aliwataka wale watakaojitokeza siku ya Jumatatu au nyingine yoyote kwa ajili ya maandamano, kufanya hivyo kwa amani.

    Waziri Murkomen aliwasihi polisi kufanya kazi yao kwa utaalamu na kuhakikisha maandamano hayo ni ya amani.

    "Ningependa kuwahakikishia Wakenya kwamba nchi yetu, wizara yetu, na serikali yetu ina nia nzuri ya kuhakikisha kuwa raia wanadumisha amani. Hatuna nia ya kumdhuru mtu yeyote. Kusudi letu ni kuhakikisha kuwa nchi yetu inasalia na amani," alisema Waziri Murkomen.

    Wakati huo huo, kuna kundi la wananchi lililojitokeza hapo jana 06/07/2025 katika eneo la Jeevanjee, wakisisitiza kufanyika kwa maandamano ya amani na kuzungumzia wahuni ambao wamekuwa wakishuhudiwa kuingilia na kuvuruga maandamano yaliyopangwa kwa kupora mali ya umma.

    Soma zaidi:

  18. Takriban watu 78 wamefariki dunia na wengine kutojulikana walipo katika mafuriko ya Texas

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Angalau watu 78 wamefariki dunia na wengine kadhaa hawajulikani walipo kufuatia mafuriko makubwa ya ghafla yaliyotokea Ijumaa katikati mwa jimbo la Texas.

    Idadi ya vifo inaonekana kuongezeka huku timu za uokoaji zikiendelea na shughuli za uokoaji.

    Kati ya vifo hivyo vilivyothibitishwa, 68, wakiwemo watoto 28, vilitokea katika Kaunti ya Kerr, ambapo kambi ya wasichana ya Kikristo iliyokuwa kando ya mto iliathirika vibaya.

    Wasichana kumi na mshauri mmoja kutoka Camp Mystic bado hawajulikani walipo. Maafisa wamesema idadi ya vifo bila shaka itaongezeka.

    Dhoruba zaidi inatarajiwa katika saa 24-48 zijazo katika eneo hilo, jambo ambalo linaweza kukwamisha timu za uokoaji ambazo tayari zinakabiliwa na nyoka wenye sumu wakati wanapochunguza matope na vifusi.

    Siku tatu baada ya mafuriko hayo, juhudi kubwa za utafutaji na uokoaji katika historia ya hivi karibuni ya Texas zilikuwa zikibadilika kuelekea operesheni ya kurejesha miili.

    Kati ya wale waliopatikana katika Kaunti ya Kerr, watu wazima 18 na watoto 10 bado hawajatambuliwa rasmi. Gavana wa Texas, Greg Abbott, alisema Jumapili kwamba mamlaka "haitasita " kuhakikisha kila mtu aliyepotea anapatikana.

    Pia unaweza kusoma:

  19. Madai ya Saba Saba hayajatimizwa Kenya, asema Raila

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga amewataka Wakenya kukusanyika katika uwanja wa Kamukunji mjini Nairobi leo Jumatatu 07/07/2025, katika kumbukumbu ya maandamano ya kihistoria ya Saba Saba.

    Akihutubia waandishi wa habari Jumapili, Odinga ambaye pia ni kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM), alisema madai ya Saba Saba bado hayajatimizwa.

    Odinga aliongeza kuwa Kenya bado inaendelea kukabiliana na mengi ya masuala yale yale yaliozua maandamano ya Saba Saba ya kwanza mnamo mwaka 1990, ikiwa ni pamoja na maisha kuwa magumu na ukiukwaji wa haki za binadamu

    "Hatujafikia kile Saba Saba alitaka", alisema. Ukiukaji wa haki za binadamu bado ni changamoto katika nchi, ukatili wa polisi upo, na uchumi haujakuwa kama tulivyotarajia. Saba Saba ilitakiwa kuwaleta watu pamoja kwa lengo moja: mabadiliko."

    Raila Odinga alisema yeye binafsi atakuwa katika uwanja wa Kamukunji, eneo lile lile ambapo wanaharakati wa demokrasia walikusanyika miaka 35 iliyopita kudai demokrasia ya vyama vingi dhidi ya utawala wa rais wa wakati huo Daniel Arap Moi.

    Wazo langu ni kutoa wito watu kwenda Kamukunji, mahali pa kwanza ambapo Saba Saba ilifanyika. Nitahudhuria Saba Saba huko Kamukunji kuwakumbuka wale waliouawa, "Odinga aliwaambia waandishi wa habari.

    Harakati ya Saba Saba, zilizopewa jina la tarehe 7 mwezi wa saba, zinafahamika katika historia ya kidemokrasia ya Kenya ambapo Wakenya waliingia mitaani wakidai demokrasia ya vyama vingi, na kusababisha kuondolewa kwa Sehemu ya 2A ya katiba.

    Kabla ya wakati huo, Kenya ilikuwa chini ya chama cha KANU {Kenyan African National Union} utawala wa Rais Moi.

    Hapo jana Jumapili, Baraza la Kitaifa la Makanisa nchini (NCCK) lilitoa wito kwa idara ya usalama kutotumia nguvu kupita kiasi dhidi ya Wakenya wakati maandamano hayo ya Saba Saba yanayotarajiwa kufanyika Jumatatu, Julai 7, 2025.

    Baraza hilo liliibua wasiwasi kuhusu mwenendo unaokua wa kile walichokitaja kama Serikali kuwanyima Wakenya haki ya kuandamana.

    NCCK Ililalamikia mauaji ya hivi majuzi ya waandamanaji na kauli iliyotolewa Waziri wa Mambo ya Ndani Kipchumba Murkomen ya kuwapiga risasi waandamanaji ikisema inatishia uhuru wa kujieleza nchini Kenya.

    Soma zaidi:

  20. Hujambo Msomaji wetu, ikiwa ni Jumatatu ya Saba Saba, karibu katika matangazo yetu mubashara tukikufahamisha yanayotokea Afrika Mashariki na Dunia nzima Ujumla. Mimi ni Asha Juma.