Mandamano ya saba saba Kenya: Makanisa yatoa wito kwa polisi kijidhibiti
Baraza la Kitaifa la Makanisa nchini (NCCK) limetoa wito kwa idara ya usalama kutotumia nguvu kupita kiasi dhidi ya Wakenya wakati maandamano ya Saba Saba yanayotarajiwa kufanyika Jumatatu, Julai 7, 2025.
Katika taarifa siku ya Jumapili, NCCK iliibua wasiwasi kuhusu mwenendo unaokua wa kile walichokitaja kama Serikali kuwanyima Wakenya haki ya kuandamana.
Ililalamikia mauaji ya hivi majuzi ya waandamanaji na kauli iliyotolewa Waziri wa Mambo ya Ndani Kipchumba Murkomen ya kuwapiga risasi waandamanaji ikisema inatishia uhuru wa kujieleza nchini Kenya.
Makanisa yanawaomba maafisa wa polisi kutekeleza wajibu wao kwamubu wa Sheria ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi na kutoa ulinzi kwa waandamanaji wote.
Chama cha NRM chamuidhinisha Museveni kugombea urais Uganda 2026
Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Yoweri Museveni ni mmoja wa marais waliosalia muda mrefu madarakani barani Afrika
Rais wa muda mrefu wa Uganda, Yoweri Museveni, 80, ametangazwa kuwa mgombea wa chama tawala katika uchaguzi wa rais mwaka ujao, na kumfungulia njia kuongeza kwa takriban miaka 40 madarakani
Katika hotuba ya kukubali hatua hiyo, Museveni alisema kuwa ameitikia wito huo na, ikiwa atachaguliwa, ataendelea na dhamira yake ya kuigeuza Uganda kuwa "nchi ya kipato cha kati".
Wakosoaji wa Museveni wanasema ametawala kwa mkono wa chuma tangu alipoingia mamlakani kama kiongozi wa waasi mwaka 1986.
Ameshinda kila uchaguzi uliofanyika tangu wakati huo, na katiba imefanyiwa marekebisho mara mbili ili kuondoa ukomo wa umri ili kumwezesha kusalia madarakani.
Msanii na mwanasiasa Bobi Wine anatarajiwa kuwa mpinzani mkuu wa Museveni katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Januari mwakani.
Wine aliiambia BBC mwezi Aprili kwamba atachuana na Museveni iwapo atateuliwa na chama chake, National Unity Platform, lakini ni kibarua "kigumu" kuwa mrengo wa upinzani kwa sababu ya kuongezeka kwa ukandamizaji wa serikali.
"Kuwa kambi ya upinzani nchini Uganda kunamaanisha kupachikwa jina la gaidi," alisema. Wine, ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi, alishindwa katika uchaguzi uliopita wa 2021 na Museveni kwa 35% hadi 59% katika uchaguzi iliokumbwa na madai ya wizi wa kura na ukandamizaji wa upinzani.
Mwanasiasa mwingine mashuhuri wa upinzani, Kizza Besigye, amekuwa kizuizini tangu Novemba baada ya kutuhumiwa kwa uhaini. Amekanusha mashtaka hayo akisema kukamatwa kwake kulichochewa kisiasa.
Tazama: Mafuriko mafuriko makubwa yalivyokumba mji wa Texas, Marekani
Maelezo ya video, Mafuriko makubwa yalivyokumba Georgetown, Texas
Operesheni kubwa ya uokoaji inaendelea katika jimbo la Texas nchini Marekani baada ya mafuriko kuwaua takriban watu 51, wakiwemo watoto 15.
Picha zilizonaswa na ndege zisizo na rubani zinaonyesha kiwango cha uharibifu uliosababishwa na mafuriko hayo katika mji wa Georgetown, baada ya Mto San Gabriel kuvunja kingo zake na kusomba majengo kwa kiasi.
Maelfu wajitokeza kumuenzi Dalai Lama
Chanzo cha picha, reu
Maelfu ya Wabudha wa Tibet wamejitokeza katika mji wa Himalaya wa Dharamshala siku ya Jumapili kusherehekea miaka 90 ya kuzaliwa kwa Dalai Lama.
Mvua kubwa iliyonyesha haikuvunja ari yao ya kumuenzi kiongozi huyo wa kiroho wa Tibet alionekana akiwa amevalia mavazi ya kitamaduni, akitabasamu akiwa katikati ya watawa wawili.
Mawaziri wa India, wafuasi wa muda mrefu akiwemo mwigizaji wa Hollywood Richard Gere na maelfu ya waumini walikusanyika kumuenzi kiongozi huyo anayeishi uhamishoni, anayetambuliwa kama mtetezi wa amani.
Chanzo cha picha, Reuters
Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock
Marekani yawarejesha wahamiaji Sudan Kusini baada ya makabiliano ya kisheria
Chanzo cha picha, Idara ya Usalama wa Taifa ya Marekani
Marekani imewatimua watu wanane nchini Sudan Kusini kufuatia mzozo wa kisheria uliopelekea watu hao kupelekwa Djibouti kwa wiki kadhaa.
Wanaume hao - waliopatikana na hatia ya uhalifu ikiwa ni pamoja na mauaji, unyanyasaji wa kijinsia na wizi - walikuwa wamemaliza au walikuwa karibu na kumaliza wa vifungo vyao gerezani.
Ni mmoja tu kati ya wanane hao anayetokea Sudan Kusini. Wengine ni raia wa Myanmar, Cuba, Vietnam, Laos na Mexico.
Maafisa wa Marekani wanasema baadhi yao wamekataliwa na mataifa yao.
Utawala wa Trump uko mbioni kuwapeleka wahamishaji wake hadi nchi ya tatu.
Imewapeleka wahamiaji katika mataifa ya El Salvador na Costa Rica.
Rwanda imethibitisha kujadiliana nayo huku mataifa ya Benin, Angola, Equatorial Guinea, Eswatini na Moldova zikitajwa katika ripoti za vyombo vya habari kama nchi zinazoweza kuwapokea wahamiaji wa Marekani.
Mafuriko Texas: Shughuli ya kuwatafuta manusura inaendelea
Chanzo cha picha, Getty Images
Mamia ya waokoaji wamepelekwa kuwatafuta watu waliotoweka katikati mwa Texas, baada ya mafuriko kuua watu 51, wakiwemo watoto 15.
Eneo lililoathiriwa zaidi ni Kaunti ya Kerr ambapo watu 43 wamefariki na ambapo watoto 27 wamesalia kutoweka katika kambi ya vijana wa Kikristo iliyoko kando ya Mto Guadalupe.
"Shughuli ya kuwatafuta waliotoweka itaendelea, hadi kila mtu apatikane," aliahidi Larry Leitha, afisa wa Kaunti ya Kerr.
Watu pia wamethibitishwa kufariki katika maeneo mengine ya jimbo, ikiwa ni pamoja na Kaunti ya Travis na Tom Green County.
Hali ya tahadhari imeendelea kudumishwa katika eneo la Texas.
Takriban 850 wameokolewa kufikia sasa.
Ayatollah Khamenei ajitokeza hadharani kwa mara ya kwanza
Chanzo cha picha, EPA
Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei amejitokeza hadharani kwa mara
ya kwanza tangu kuanza kwa mzozo wa Iran na Israel, kwa mujibu wa vyombo vya
habari vya serikali.
Picha za runinga ya
serikali zilimuonyesha akiwasalimia waumini kwenye msikiti siku ya Jumamosi kabla
ya tamasha la waumini wa Kishia linalofahamika kama Ashura.
Mara ya mwisho Khamenei kuoneka
ilikuwa katika hotuba iliyorekodiwa wakati wa mzozo na Israel, ulioanza tarehe
13 Juni na wakati ambapo makamanda wakuu wa Iran na wanasayansi wa nyuklia
waliuawa.
Israel ilifanya
mashambulizi ya kushtukiza katika maeneo ya nyuklia na ya kijeshi nchimi Iran.
Hatua ilisababisha makabiliano makali baada ya Iran kulipiza kisasi kwa
mashambulizi ya angani yaliyolenga Israel.
Wakati wa vita vya siku 12 na Israel, Khamenei
alionekana kwenye TV katika ujumbe wa video na kulikuwa na uvumi kwamba alikuwa
amejificha kwenye chumba chini ya ardhi.
Siku ya Jumamosi matangazo ya vyombo vya habari vya
Iran yalitawaliwa na mwonekano wa Khamenei, huku wafuasi wakionyesha kufurahia kumuona
kwenye televisheni.
Khamenei anaonekana akimgeukia kasisi mkuu Mahmoud
Karimi, akimhimiza "kuimba wimbo wa taifa, O Iran".
Wimbo huo wa uzalendo
ulipata umaarufu mkubwa wakati wa mzozo wa hivi majuzi na Israel.
Israel kutuma wapatanishi kwenye mazungumzo ya Gaza licha ya matakwa ya Hamas
Chanzo cha picha, reu
Israel imeamua kutuma ujumbe wake nchini Qatar leo Jumapili kwa mazungumzo
ya ana kwa ana na Hamas kuhusu pendekezo la hivi punde la kusitisha mapigano
Gaza na kuachiliwa kwa mateka.
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu inasema kuwa amekubali
mwaliko huo licha ya kile alichokitaja kuwa mabadiliko
"yasiyokubalika" ambayo Hamas ilitaka kufanya kwenye mpango
uliowasilishwa na wapatanishi kutoka Qatar, Marekani na Misri.
Siku ya Ijumaa usiku, Hamas ilisema imetoa "jibu chanya" kwa
pendekezo la kusitisha mapigano kwa siku 60 na kwamba iko tayari kwa
mazungumzo.
Hata hivyo, afisa wa Palestina alisema kundi hilo linataka kuhakikishiwa kwamba uhasama hautaanza tena ikiwa mazungumzo juu
ya mapatano ya kudumu hayataafikiwa.