Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, sheria inaruhusu waandamanaji kushtakiwa kwa ugaidi Kenya?
- Author, Laillah Mohammed
- Nafasi, BBC Swahili
- Akiripoti kutoka, Nairobi
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Mwanaharakati Boniface Mwangi ameponea shitaka la ugaidi ambalo lilimkabili tangu kukamatwa kwake mnamo Jumamosi Julai 19. Mwangi ambaye sasa ameachiwa huru kwa dhamana ya shilingi milioni moja za Kenya ambazo ni sawia na dola 7,750.
Mwangi amerejea nyumbani akisubiria kutajwa kwa kesi inayomkabili ya kumiliki risasi pasi kuwa na kibali rasmi ya kumiliki bunduki kw amujibu wa sheria za Kenya.
Na huku Mwangi akisubiri kuanza kisikilizwa kwa kesi dhidi yake, kuna washukiwa wengine kadhaa ambao pia wanazuiliwa kwa tuhuma za ugaidi, uhaini, mauaji, kuteketeza mali kwa kukusudia, ubakaji na dhuluma za kingono miongoni mwa mashtaka mengine.
Wabunge wawili: John Mukunji wa Manyatta na Jayne Kihara wa Naivasha wanakabiliwa na mashtaka ya kupanga na kufadhili ugaidi kwa kuwatuma vijana kuvamia vituo vya polisi na kuviteketeza katika maandamano ya Juni 25 na Julai 7.
Kwa mujibu wa katiba na sheria za Kenya, mtu binafsi au kundi la watu wanaweza kufunguliwa mashtaka ya ugaidi ikiwa makosa yao yamefikisha vigezo vifuatavyo.:
1. Kutekeleza kosa la ugaidi ambalo linahusisha ghasia ambazo zinatishia maisha ya watu, kuweka umma hatarini, kuharibu vibaya mali ya kibinafsi au ya umma, kutumia silaha au vilipuzi, au kurusha na kutumia kemikali hatari kwa umma kwa ajili ya kuwadhuru.
2. Kusaidia makundi ya kigaidi
3. Kuwahifadhi watu ambao wanapanga njama ya kutekeleza ugaidi
4. Kupanga na kufadhili tukio la kigaidi
5. Kumiliki kemikali za kibayolojia zenye uwezo wa kuwadhuru watu wengi.
Kwa misingi ya maelezo hayo ya sheria ya kuzuia ugaidi ulioanza kutumiwa mnamo Oktoba 26, 2012 baada ya kuidhinishwa na Bunge, makosa yaliyofanyika kwenye maandamano ya Juni 17, Juni 25 na Julai 7 mwaka huu yanaweza kuchukuliwa hatua chini ya sheria ya kanuni ya adhabu Yaani penal code ama sheria ya mpangilio wa mienendo ya umma Yaani public order act.
Wakili Charles Kanjama anasema kwamba ni sharti kwa upande wa mashtaka ya umma kuhusisha makosa yaliyotekelezwa na waliokamatwa na ugaidi huku kosa hilo likiwa wazi na kuoneysha kwa ufasaha kwamba tukio la kigaidi lilitekelezwa.
Baadhi ya mawakili wanahisi kwamba waundaji wa katiba ya Kenya ya 2010 na vile vile wabunge wanaojukumika na kuifanyia marekebisho katiba, hawakuwazia suala la maandamano kugeuka kuwa uwanja wa ghasia na makabiliano kati ya ''waandamanaji na polisi'' na kwamba pia taasisi za kiserikali huenda zikavamiwa kwa njia iliyoshuhudiwa na silaha kuibwa.
Akihutubia taifa baada ya maandamanos ua Juni 25, Waziri Kipchumba Murkomen alisema kwamba matukio ya jumatano hiyo yalikuwa yaliangaliw ana seikali kama jaribio la kuipenduwa serikali ya Rais William Ruto.
''Tutawakamata wote wanaopanga, kufadhili maandamano hayo na kufanya uharibofu wa mali ya kibinafsi na ya umma. Haiwezekani kwamba vituo vya polisi vinavamiwa na hata silaha kuibwa. Hatutakubali hilo kuendelea,'' alisema Murkomen katika kikao na waandishi wa habari.
Wakili Demas Kiprono ambaye ni Naibu Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Mawakili (ICJ), anasema kwamba kwa mtazamo wake upande wa mashtaka utakuwa na kibarua kigumu kuhakikisha kwamba walioshtakiwa kwa na ugaidi watapatikana na hatia.
''Sheria ya kuzuia ugaidi ilibuniwa na serikali kukabiliana na ugaidi ambao wakati huo ulikuw aumekithiri nchini. '' alisema Demas
Kundi la Al shabaab lilikuwa linatekeleza ugaidi kwa kutumia raia wa Kenya waliopata mafunzo ya itikadi kali. Kati ya 2011 na 2017 Kenya ilishuhudia matukio kadhaa ya kigaidi ndani ya nchi na kwenye maeneo ya mipakani.
Matukio ya kushambuliwa watalii wawili katika mji wa Kiunga ulipo kweeye mpaka wa Kenya na Somalia katika kaunti ya Lamu pwani ya Kenya, kulichangia vita vikubwa vya Kenya dhidi ya Ugaidi na kumfanya Rais Mwai Kibaki kuvituma vikosi vya jeshi la Kenya Somalia kupambana na Al Shabaab kwenye Operation Linda Nchi.
Katika matukio ya Ugaidi kwenye jumba la kibishara la Westgate mnamo 2013, chuo kikuu cha Garissa mnamo 2015, na katika jumba la kibishara la Dusit D 2 mnamo Januari 2017, washukiwa wakuu walikuwa raia wa Kenya, vijana waliokuwa wamepokea masomo ya chuo kikuu ambao walibadili misimamo au hata kubadili taifa kwa ajili ya kuendeleza misimamo ya itikadi kali dhidi ya raia wa Kenya.
Demas anasema kwa sababu Kenya sio mgeni kwa matukio ya kigaidi, basi ni rahisi kwa Wakenya kutambua ugaidi unapotokea na kwa kwamba kwa sasa sheria husika inatumiw avibaya na upande wa serikali.
Wakili Suiyanka Lempaa ambaye amekuwa msitari wa mbele kuwawakilisha baadhi ya washukiwa mahakamani anahisi kwamba, ''Hakuna kesi hapo. Hiyo ni njia ya serikali kuwanyamazisha wakosoaji na wanaitumia vibaya sheria hii.'' Aliiambia BBC.
Baadhi ya wanasheria wanahisi kwamba ni sharti kuwepo na uhusiano wa karibu kati ya washtakiwa na makundi au watu binafsi wenye kuwa na Azimio ya kutekeleza ugaidi. Na kwamba kosa hilo ambalo ni la jinai linaonekana wazi kwamba ugaidi umetekelezwa.
Wakili Charles Kanjama anatoa wito upande wa mashtaka kutathmini mashtaka hayo kabla ya kuwachukulia hatua washukiwa.
''Ni jambo la kusikitisha kwamba hili limefanyika, natuma mahakama itatafsiri vyema sheria ya kuzuia ugaidi na kutupilia mbali hizo kesi au kupendekeza mashtaka yanayofaa dhidi ya washukiwa hao,'' alisema Kanjama.
Ameendeelea kueleza kwamba katika baadhi ya kesi, ikiwa mtu binafsi amepanga kulemaza shughuli za uchumi wa taifa basi sheria zinafafanua wazi jinsi anavyostahili kuadhibiwa.
Imehaririwa na Ambia Hirsi