Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
David Maraga ndiye rais wanayemtaka vijana nchini Kenya?
- Author, Laillah Mohammed
- Nafasi, BBC Swahili
- Akiripoti kutoka, Nairobi
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Kama wewe ni mzoefu wa ''kudurusu'' kurasa za mitandao ya kijami kama wengi wanavyofanya siku hizi basi utakuwa umekutana na ujumbe wa aina hii, kwa mfano
#MaragaForPresident #Maraga2027 #RutoMustGo
Katika miezi miwili iliyopita, David Kenani Maraga, jaji mkuu mstaafu wa Kenya amejipatia umaarufu mitandaoni na hata mitaani ambapo vijana wanamuona kama sura mpya ya uongozi ambao wanahisi taifa linakosa.
Alipotangaza rasmi nia yake ya kuwania kiti cha Urais wa Kenya mnamo Juni 19, Maraga alieleza kwamba hali ya kisiasa na kiuchumi nchini humo imemlazimu kujitosa katika utumishi wa umma kwa mara nyingine na kuweka kando mipango mingine aliyokuwa nayo kwa sasa baada ya kustaafu.
"Uamuzi huu umefanywa kutokana na jinsi mambo yamekuwa yakifanyika nchini. Kuwaona vijana wetu wakihangaishwa jinsi wanavyofanyiwa kwa sasa ni jambo ambalo linanipa wasiwasi mkubwa," alisema Maraga.
Tamko hili lilinokena kuwa kama mwamko mpya kwa wengi ambao mara moja walionyesha hamu ya kumtaka kujitosa ulingoni na kupambana vikali kumrithi Rais wa sasa William Ruto kwenye uchaguzi wa 2027.
Katika ujumbe wao kwenye kurasa mbali mbali za mitandao ya kijami, vijana wemeonekana kumuunga mkono Maraga.
Harun Kimathi aliandika kwamba, "Sijali ikiwa nitasilia peke yangu, ila mimi na familia yangu tutampigia kura Maraga."
Carolyne Muthini naye akasema kwamba ,"Pindi tu Maraga alipotangaza kwamba atawania Urais, nilijawa na matumaini kwamba nchi yetu itapata mkombozi na kuokolewa hivi karibuni. Bila shaka nitampigia kura."
Juck Tumwa naye amesema kwamba," Jaji Mkuu, umeonyesha kwamba unafuata sheria za nchi na wewe ni mwaminifu na mtiifu wa katiba. Utaikomboa taifa hili. Endeleza mipang yako tutasimama na wewe."
Kwa sasa Maraga anasema kwamba anajiandaa kwa ajii ya kutengeneza ilani yake ya uchaguzi, ambayo ana amini itamuweka Mkenya wa kawaida katikati ya maono yake.
Ila kulingana na Dktari Peter Mwencha ambaye ni mhadhiri na mtaalamu wa uongozi na masuala ya kidiplomasia, Maraga anapaswa kuwa na ujumbe maalum atakaowapa raia ili kumuwezesha kuanza kuuza sera zake.
"Kwa kweli ni sura mpya ambayo taifa halijakuwa nalo hapo awali. Ni mgeni katika siasa na hana tabia ambazo zimeshuhudiwa awali na wanasiasa waliomtangulia. Lakini kwa sasa kilicho muhimu ni yeye kuwa na ujumbe utakaoafikiana na mahitaji ya wengi katika jamii na sio tu vijana na kuwa na suluhisho la kuboresha hali ya maisha ya wakenya," alisema Dkt Mwencha kwenye mahojiano na BBC.
Jaji Mkuu mstaafu Maraga ni nani?
David Kenani Maraga alihudumu kama Jaji Mkuu wa pili nchini Kenya chini ya katiba mpya iliyoasisiwa Agosti 2010. Aliteuliwa katika tume ya kusimamia idara ya mahakama (JSC) mwaka 2016 kufuatia kustaafu mapema kwa mtangulizi wake Willy Mutunga aliyehudumu katika wadhifa huo kwa miaka minne chini ya muongozo wa katiba mpya ya Kenya.
Kabla ya hapo Maraga ambaye alizaliwa Januari 12, katika kaunti ya Nyamira alihudumu kama Jaji wa Mahakama ya juu na ya rufaa kwa jumla ya miaka 13 ambapo alihudumu katika vituo mbali mbali nchini Kenya.
Japo alikuwa Jaji ambaye alipenda sana kufuata sheria na hakutaka kujihusisha na masuala ya ufisadi, alijikuta akipishana na watu kadhaa kutokana na maamuzi yake aliyoyatoa Mahakamani.
Tamko la aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta la ''We shall Revist'' lilionekana kuwa wimbi jeusi kwake Maraga hasa baada ya uamuzi wa Mahakama ya juu zaidi nchini Kenya mwezi Septemba 2017 kubatilisha ushindi wa Uhuru Kenyatta.
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa Barack Muluka anasema kwamba, ''wakati wa uamuzi huo uliokubaliana na ombi la upande wa NASA ulioongozwa na Raila Odinga kwamba kulikuwa na dosari kwenye usimamizi wa uchaguzi huo.
Na baada ya hapo, alionekana kukinzanana na uongozi wa nchi wakati huo na kuonekana mara kwa mara akilalamikia hatua zilizochukuliwa na serikali ya Kenyatta aliyotaja kama njia ya kuikata miguu Idara ya Mahakama.''
Maraga alilalamikia hatua ya kupunguzwa kwa bajeti ya Idara ya Mahakama huku pia akitaja hatua ya Rais Kenyatta kukataa kuidhinisha majina ya majaji sita walioteuliwa kuhudumu kwenye Mahakama ya rufaa kama ukiukwaji wa sheria.
Hata hivyo, Maraga alitumia kila fursa kuzungumzia kile alichohisi ni mambo kwenda mrama Serikalini na kukashifu bunge kwa kutofuata masuala ya kikatiba.
''Bunge limeshindwa kupitisha sheria ya kutozidi thuluthi mbili ya jinsia moja katika utumishi wa umma, na kwa vile kwa sasa bunge hilo halijatimiza matakwa hayo yaliyopendekezwa kwenye katiba, basi bunge linapaswa kuvunjwa,'' alisema Maraga mwaka wa 2019.
Bunge lilipinga hatua hiyo na mamlaka za nchi pia hazikuonekana kulipa kipaumbele suala hilo wakati huo, ambapo kulingana na Muluka, Maraga alitekeleza jukumu lake kikatiba.
''Alitoa maelezo yake kama mkuu wa Idara ya Mahakama ambayo ina jukumu la kutafsriri maelelezo ya katiba. Ila jukumu la kutekeleza pendekezo lake lilikuwa mikononi mwa uongozi wa nchi wakati huo. Alisimama wakati mwingi kwa msingi na mwamba wa katiba na hilo lilionekana kama kivutio kikubwa kwa wengi nchini Kenya kwamba ni kiongozi mwenye uadilifu,'' alisema Muluka.
Mtazamo wa Maraga wa sasa ni upi?
Akihojiwa kwenye vyombo vya habari nchini Kenya, katika siku chache zilizopita, Maraga amesisitiza kwamba yeye ndiye Suluhu ambayo taifa inahitaji kwa sasa.
Na japo anatetea hoja zake kwa misingi ya kupambana na ufisadi na kuboresha hali ya uchumi, kwa wengi ambao wanakabiliwa na mzigo mkubwa wa kodi zinazotozwa wafanyakazi, suala hilo ni jambo ambalo wangelipenda kulisikia kutoka kwake.
Daktari Mwencha anasema kwamba, 'Maraga anapaswa kuwa na ujumbe ambao atauuza kwa vijana na taifa zima kwa jumla. Ni sharti atambue kinachowabana raia na kisha kuuza sera zake zilizozingira suala hilo mara moja.'
Maraga mwenyewe amesema kwamba anafanya mazungumzo ya kina na wataalamu ambão watampa ushauri unaofaa kuweza kujiandaa vilivyo kwa kile ambacho wengi wanahisi ni mapambano makubwa katika maisha yake.
Muluka kwa mtazamo wake anasema kwamba , siasa za Kenya zimeshuhudia wanasiasa ambão ni wepesi kuahidi mambo, na rahisi kusahau pindi tu wanapoingia madarakani.
'Siasa za Kenya zina uchafu kiasi, kuna wale wanye kunawiri katika matusi, udanganyifu, kula rushwa, kulaghai mara nyingine na sio jambo ambalo Maraga analisimamia. Ni sura mpya ila anapaswa kutumia ujasiri wake zaidi katiak upande wa siasa kujiuza vyema kwa vijana,' alisema Muluka.
Vijana wenyewe wanahisi kwamba msimamo wake wa kusimama nao kwenye maandamano na kutetea haki za kimsingi za raia wote ni mwanzo mwema kwao.
Maraga alikuwa miongoni mwa kundi la mawakili wakuu waliofika Mahakamani wiki hii kusikiliza kesi inayowakabili watu 71 ambao wanakabiliwa na shitaka la ugaidi na uhaini kwa kuhusia kwenye ghasia zilizoshuhudiwa katika Taaisisi kadhaa za kiserikali mnamo Juni 25 na Julai 7 mwaka huu.
Don Kitheka alimpongeza Maraga akisema kwamba, 'Huyu hapa Rais wangu katika Mahakama ya kahawa akisimama kidete na vijana. Maraga anahitaji kupongezwa na kupata likes elfu moja.'
Maraga mwenyewe amewasuta wanao mkejeli kwa kuandaa vídeo na mwanamuziki mashuhuri nchini kenya mwenye jina la Charisma. Katika maandishi aliyoandika kwa kiingereza, maraga anaoenekana kuzungumza katika lugha wanayaoitambua vijana almaarufu Gen Z kwa kusema, 'Who said that I dont have charisma?' Kisha msaanii huyo anajitokeza na wawili hao wanacheka wakisalimiana.
Mara kwa mara amesisitiza kwamba, 'Watu wananiuliza ni kwanini, ninajotosa kwenye ulingo wa kisiasa nikiwa na umri huu? Nilipatwa na wasiwasi kwa kuwa ninaamini sote tukisusia kujitolea kuliongoza taifa, huenda tukakosa taifa ambalo watoto na wajukuu wetu watalirithi. Ninajitolea kujukumika binafsi kama Maraga, na nikipata fusra ya kuliongoza taifa, basi nitajitahidi.'
Kwa vijana hasa wanavyojieleza kwenye mitandao, wako tayari hata kuchanga ili kufadhili kampeni yake na kusimamama naye hadi watakapo hakikisha ameingia madarakani.
Lakini je, vijana watashiriki kwenye uchaguzi?
Katika miaka ya hapo awali, vijana wameonakana kususia kutekeleza wajibu huu waliokabidhiwa kisheria.
Mtaalaum Peter Mwencha anasisitiza kwmaba kuna haja ya vijana kujisajili kama wapiga kura na kujitokeza siku ya uchaguzi kwa ajili ya kumchagua kiongozi wanayemtaka.
Taifa kwa sasa liko katika hali ngumu, huku wengi wakihisi kwamba hali yao ya kiuchumi ni ngumu, japo Rais amesema kwamba tangu kuingia madarakani, mambo yamekuwa mazuri kiasi.
Lakini kwa vijana waliosoma na kupata viwango vya juu vya masomo, ukosefu wa ajira na hali ya kuhisi kwamba wanapoteza matumaini ni jambo ambalo linazidi kuwakera moyoni.
Kwa sababu hii, wamejitokeza kuandamana na kuikashifu serikali kwa kuendeleza sera ambazo wanahisi zinabana wengi. Hata hivyo, hatua hiyo imesababisha wengi kupotea, kuuawa, wengine wakikabiliwa na mashtaka Mahakamani na wakihisi kwamba uongozi wa sasa hauwasikilizi wao na kuwapa wanacho kihitaji.
Safari ya Maraga kulekea ikulu itajumuisha akina nani?
Barack Muluka anauliza hivi, 'Unaposimama kuwania uongozi wa nchi, wengi wanatazama kujuwa ni kina nani watasafiri na wewe katika azima yako?
Anahisi kwamba ni wakati mwafaka wa Maraga kuanza kutafuta ni wanasiasa wapi wenye mitazamo kama yake kwa ajili ya kuwa na kikosi kitakachotumika ipasavyo kama jeshi la kuwarai wananchi kumpigia kura Maraga kura 2027.
Kumuondoa Rais William Ruto haitakuwa kazi rahisi, ila wengi wanadhani ikiwa atajiandaa vyema basi huenda akawa na uwezo wa kupambana makabiliano haya.
Mwenda na Muluka wanaunga mkono maoni ya baadhi ya vijana kwamba wangependa Maraga aungane na Seneta wa Busia Okiya Okoiti Omutata kutengeneza timu itakayomuingiza Ikulu. Hii ni kwa sababu wengi wanahisi kwamba wawili hao wamekuwa watetezi wakubwa wa jamii na wana maadili yanaoana.
Kingine kinachotajwa ni ni vijana kutaka kujumuishwa kwenye meza ya uongozi na sio kutumika kwa njaa ya leo bila kujua hatma yao ya kesho.
Sera za Maraga za kimataifa ni zipi?
Huku wimbi la kumtaa Maraga kama kiongozi likivuma ndani ya nchi, wengi wangependa kujuwa mtazamo wake kidiplomasia ni upi. Ana sera zipi za kimataifa mbali na utetezi wa haki za kibinadamu – kama alivyoonyesha kwa kusimama na kiongozi wa chama kikuu cha upinzani Tanzania (CHADEMA) Tundu Lissu alipokuwa Mahakamani kuhudhuria kesi yake ya uhaini.
Ili kushawishi jamii ya kimataifa, itampasa Maraga kuwazia kwa undani sera yake na jinsi atakavyojiandaa kama mwanasiasa aliyetosha kubadili mkondo wa taifa ambao kwa sasa wengi wanahisi umekwenda kombo.
Lakini huku Maraga mwenyewe akilivalia njuga suala hilo, machapisho kama 'Maraga is my next President' yataendelea kushuhudiwa mitandaoni, huku wengi wakiwa na matumaini kwamba maneno hayo yataandamana na vitendo kwenye sanduku la kura.
Kwa sasa orodha ya wanaotaka kumuomdoa rais Ruto madarakani ifikiapo 2027 na kuhakikisha anahudumu kwa awamu moja kama Rais, Maraga ndiye anayeonakana kama asiye mwanasiasa ila atakuwana kibarua kigumu kutoka kwa kundi la upinzani linaojumuisha wanasiasa wakongwe kama Kalonzo Musyoka, Martha Karua, aliyekuwa naibu rais Rigath Gachagua na aliyekuwa waziri wa usalama wa ndani Fred Matiangi'.