PSG vs Real Madrid: Vita ya Ulaya iliyohamia kombe la dunia

Muda wa kusoma: Dakika 4

MetLife Stadium huko New Jersey, Marekani, itashuhudia pambano la kutikisa dunia usiku wa leo, wakati Paris Saint-Germain (PSG) wakivaana na Real Madrid katika nusu fainali ya pili ya kombe la dunia la klabu (FIFA Club World Cup).

Hii ni mechi inayokutanisha wababe wa soka la Ulaya, mabingwa wa sasa wa Klabu bingwa Ulaya (UEFA Champions League) PSG dhidi ya mabingwa wa mwaka uliopita Real Madrid.

Tayari Chelsea wametinga fainali baada ya kuifunga Fluminense kwa mabao 2-0, likiwemo bao la usajili wao mpya Pedro, hivyo mshindi wa pambano hili anakutana nao katika fainali inayosubiriwa kwa hamu kubwa.

Mbappe vs Dembele: Je, ndugu hawa wataamua mchezo?

Katika kitovu cha mvutano huu wa kisoka ni mastaa wawili wanaowakilisha taifa moja la Ufaransa, ni ndugu kwa taifa lakini sasa wakitazamana kama mahasimu, Kylian Mbappe na Ousmane Dembele.

Wawili hawa walishirikiana vyema wakiwa pamoja PSG kabla Mbappe hajahamia Real Madrid mwezi Juni 2024, na sasa wanakutana uso kwa uso kwenye jukwaa kubwa zaidi duniani la vilabu.

Mbappe, ambaye ameifungia Madrid mabao 44 katika mechi 58 msimu huu, aliihakikisha timu yake nafasi hii kwa bao la ajabu la 'bicycle kick' dhidi ya Borussia Dortmund katika dakika ya 94 kwenye robo fainali. Hilo lilikuwa tamati ya ushindi wa 3-2 kwa Madrid, katika marudio ya fainali ya UEFA ya msimu uliopita.

Kwa upande wa Dembele, maisha yamekuwa ya neema tangu kuondoka kwa Mbappe. Ameibuka kuwa nguzo kuu ya mashambulizi ya PSG, akifunga mabao 34 katika mechi 51, na kuiongoza timu hiyo kutwaa mataji manne makubwa msimu huu – ikiwa ni pamoja na Ligi ya mabingwa Ulaya. Dembele amesema:

"Najisikia vizuri sana. Huu ndio msimu bora kabisa katika maisha yangu ya soka. Nilijiunga na PSG kwa ajili ya nyakati kama hizi. Mwaka huu umekuwa wa kipekee, binafsi na kwa timu pia. Ni wa kushangaza. Lakini tunataka zaidi. Ukishajua ladha ya ushindi, unataka tena na tena."

Safari ya kufika nusu fainali

Real Madrid walianza kampeni yao kwa sare ya 1-1 dhidi ya Al Hilal huko Miami, kabla ya kuigaragaza Pachuca 3-1. Ushindi wa mwisho wa 3-0 dhidi ya RB Salzburg uliwapeleka hadi hatua ya 16 bora, ambapo waliibuka na ushindi mwembamba wa 1-0 dhidi ya Juventus.

Kisha wakailaza Borussia Dortmund 3-2 kwenye robo fainali, mechi iliyojaa mambo ya kustajabisha kisoka na ilihitimishwa na umahiri wa Mbappe kwa goli la dakika za mwisho.

PSG, kwa upande mwingine, walikua bora toka mapema kwa kuichapa Atletico Madrid 4-0 huko Los Angeles. Ingawa walipigwa 1-0 na Botafogo katika mechi ya pili, walirudi kwa nguvu dhidi ya Seattle na kushinda 2-0.

Hatua ya 16 bora waliitumia vuema kuilaza Inter Miami ya Lionel Messi kwa kipigo cha 4-0 kabla ya kuwaondoa Bayern Munich 2-0 kwa mchezo wa hadhi ya juu wa robo fainali.

Historia, rekodi na kauli za makocha

Real Madrid ni timu yenye historia nene kwenye michuano hii ya kombe la dunia la Klabu, wakiwa na mataji matano tayari, na wakisaka la sita. Mwaka jana walitwaa taji hilo kwa kuichapa Al Hilal 5-3.

Wanaongoza pia kwa jumla ya mabao na ushindi katika historia ya mashindano haya.

PSG kwa upande mwingine, wanatafuta taji hili kwa mara ya kwanza lakini wakishinda, wataweka historia kama klabu ya kwanza ya Ufaransa kutwaa mataji matano makubwa (quintuple) ndani ya msimu mmoja: Ligi kuu (Ligue 1), Coupe de France, Trophee des Champions, mabingwa Ulaya na kombe la dunia kwa vilabu. Ni Manchester City pekee waliowahi kufanya hivyo, mwaka 2023.

Dondoo Muhimu kabla ya Mchezo:

  • Mbappe: mabao 44, mechi 58
  • Dembele: mabao 34, mechi 51
  • PSG: mabao 12 katika mashindano haya, Real Madrid mabao 11
  • Uwanja: MetLife Stadium (New Jersey), uwezo wa watazamaji 82,500
  • Mshindi atakutana na Chelsea waliowafunga Fluminense 2-0

Kauli za Makocha kabla ya Mechi. Xabi Alonso, Kocha wa Real Madrid anasema:

"Mapambano ya kiufundi dhidi ya Luis Enrique yatakuwa mtihani mkubwa kwetu. Tutaandaa kikosi chetu kwa mtazamo chanya baada ya ushindi wa leo kwenye robo fainali."

Luis Enrique, Kocha wa PSG:

"Haitajalisha tunakutana na nani katika nusu fainali. Kinachojalisha ni kwamba tupo hapo na tunataka kufika fainali."

Kwa ufupi hii si mechi ya kawaida ni vita ya hadhi, historia na ukubwa. Vita ya Ulaya iliyohamia duniani. Ni Mbappe dhidi ya zamani zake, ni Dembele kutaka kutawala dunia, ni mabingwa wa kihistoria dhidi ya wanaotafuta urithi wa kudumu. MetLife itaamua nani atasonga kucheza fainali dhidi ya Chelsea Jumapili ya Julai 13, 2025?

Usiku huu, dunia ya soka inasimama.