Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ndoto za Arsenal mabingwa Ulaya zaota mbawa yachapwa na PSG
Ndoto ya Arsenal ya kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya imefikia kikomo baada ya kuchapwa kwa mabao 2-1 dhidi ya Paris Saint-Germain katika mechi ya marudiano ya nusu fainali iliyochezwa Parc des Princes usiku wa Mei 07.
Kikosi cha Mikel Arteta kilikuwa tayari nyuma kwa bao moja kwa bila kutokana na matokeo ya mechi ya kwanza ya nusu fainali. Licha ya kuanza kwa kasi katika mechi ya pili ya nusu fainali ugenini, walijikuta wakizidiwa kwa jumla ya mabao mawili pale Fabian Ruiz alipoifungia PSG bao la kwanza dakika ya 27.
Vitinha alikosa penalti, baada ya Myles Lewis-Skelly kunawa mpira mkononi katika eneo la hatari kufuatia uamuzi tata wa VAR, kabla ya Achraf Hakimi kufunga bao la pili katika dakika ya 72 na kuiondoa kabisa Arsenal kwenye mashindano.
Tofauti na mechi ya kwanza Emirates, Arsenal walianza kwa kasi ambapo mpira wa kichwa wa Declan Rice ulitoka nje karibu na goli la Gianluigi Donnarumma ndani ya dakika tatu.
PSG walipata penalti baada ya shuti la Hakimi kugonga mkono wa Lewis-Skelly, na mwamuzi Felix Zwayer aliitwa kwenda kuangalia VAR. Bila kusita, alitoa penalti ambayo ilionekana kuwa msumari wa. moto dhidi ya Arsenal.
Vitinha alikwenda kupiga mkwaju huo, lakini mlinda mlango David Raya aliokoa.
Hata hivyo, dakika tatu baadaye, Thomas Partey alishindwa kuondoa hatari na Hakimi akaifungia PSG bao la pili kwa shuti lililokwenda moja kwa moja kwenye kona ya chini ya goli.
Arsenal walipata mwanga kidogo walipofunga bao la kufutia machozi baada ya Leandro Trossard aliyemzidi ujanja Marquinhos, kabla ya kumpasia Bukayo Saka aliyemzunguka Donnarumma na kufunga.
Dakika 10 kabla ya mchezo kumalizika, pasi ya Riccardo Calafiori ilimkuta Saka akiwa peke yake na goli, lakini alipiga juu ya lango na hivyo kuzima matumaini yoyote ya Arsenal kupata kombe msimu huu.
PSG, ambao sasa wamezichapa timu tatu kutoka Ligi kuu ya England mfululizo: Liverpool, Aston Villa, na sasa Arsenal, watachuana na Inter Milan katika fainali itakayopigwa Mei 31, baada ya ushindi wa jumla wa mabao 3-1.
Arsenal walifika fainali ya Ligi ya Mabingwa mara moja tu, mwaka 2006, ambapo walifungwa na Barcelona jijini Paris. Mji mkuu wa Ufaransa umeendelea kuwa mahali pa majonzi kwa timu hiyo ya London Kaskazini.