Boeing 737 Max 9: Safari za ndege zasitishwa baada ya hitilafu kutokea

ndege

Chanzo cha picha, Reuters

Mashirika makubwa ya ndege nchini Marekani yamezuia makumi ya ndege za Boeing kuendelea na safari baada ya sehemu ya ndege kupasuka katikati ya safari ya Oregon.

Hatua hiyo imesababisha maelfu ya abiria kusitisha safari zao.

Mamlaka ya usafiri wa anga ya Marekani imesema ndege 171 aina ya Boeing 737 Max 9 lazima zizuiliwe kwa ajili ya ukaguzi baada ya sehemu ya ndege ya Alaska Airlines kuanguka siku ya Ijumaa.

Alaska imesema safari za ndege zinatarajiwa kutatizika hadi wiki ijayo.

Usitishwaji huo unaonekana kuathiri zaidi safari za ndege za nchini Marekani.

Hatua hii imechukuliwa baada ya mamlaka inayodhibiti safari za anga (FAA) kuagiza "ukaguzi wa haraka" wa 737 Max 9 duniani kote.

Ukaguzi unaohitajika utachukua takribani saa nne hadi nane kwa kila ndege, ilisema.

Wakala wa Usalama wa Anga wa Umoja wa Ulaya (EASA) unafuata muelekeo wa FAA, lakini mabadiliko ya safari za ndege katika bara hilo yanatarajiwa kuwa kidogo.

EASA imesema inaamini kuwa hakuna mashirika ya ndege ya Ulaya yanayotumia Max 9 zenye kwa umbo linalotajwa kwenya agizo hilo la FAA.

Mojawapo ya viwanja vya ndege vikubwa zaidi duniani, London Heathrow, imesema hakuna athari kwa safari za ndege.

Sehemu kubwa ya ndege zilizoathiriwa zinamilikiwa na mashirika ya ndege ya Marekani.

United Airlines imesimamisha ndege zake zote 79 za Max 9.

ndani

Alaska imesema imeahirisha safari 160 za ndege siku ya Jumamosi na kuathiri abiria takribani 23,000.

Mashirika mengine ya ndege ambayo pia hutumia ndege hizo yameziondoa kazini kwa muda.

Boeing ilisema inakaribisha uamuzi wa FAA, na kuongeza kuwa timu yake imekuwa na mawasiliano ya karibu na mdhibiti.

Wakati wa tukio la Ijumaa, ndege ya Alaska Airlines 1282 kutoka Portland, Oregon, hadi Ontario, California, ilifikia 16,000ft (4,876m) ilipoanza kushuka kwa dharura, kulingana na data za kufuatilia ndege.

Abiria waliokuwa ndani ya ndege hiyo walisema sehemu kubwa ya ganda la nje la ndege hiyo lilianguka chini muda mfupi baada ya kupaa.

n

Picha zinazoonekana katika vyombo vya habari zinaonesha anga nyakati za usiku na taa za Portland zikionekana pamoja na sehemu ya ndege iliyoathirika.

Abiria mmoja alisema sehemu hiyo ilikuwa "kama jokofu" huku mwingine akisema shati la mtoto lilipeperuka kwa upepo wakati ndege hiyo ilipotua kwa dharura.

Ndege hiyo, iliyokuwa na abiria na wafanyakazi 177, ilitua salama huko Portland. Alaska ilisema abiria kadhaa walijeruhiwa, lakini sio sana.

"Ninawahurumia wale waliokuwa kwenye ndege hii – nawaomba radhi sana kwa kile mlichokumbana nacho," Mkurugenzi Mtendaji wa Alaska Ben Minicucci alisema baada ya kampuni hiyo kujitolea kusitisha ndege zake 65 za 737 Max 9.

"Ninashukuru sana kwa muitikio wa marubani na wahudumu wetu wa ndege," aliongeza.

Alaska baadaye ilisema kwamba, kufikia Jumamosi alasiri, ilikuwa imesitisha safari 160 za ndege.

Shirika hilo la ndege lilisema Jumamosi kwamba ndege zake 18 za Max 9 ambazo ni karibu robo ya idadi ya zote zilifanyiwa ukaguzi wa ukarabati mkubwa na kurudishwa kufanya kazi, lakini kufuatia maagizo ya FAA hizo pia "zimeondolewa kutoa huduma."

"Tunawasiliana na FAA ili kubaini shida ni nini , ikiwa ukaguzi zaidi unahitajika kabla ya ndege hizi kurejeshwa kutoa huduma," Alaska ilisema katika taarifa.

Iliongeza: "Ndege iliyohusika katika ndege ya 1282 iliwasilishwa kwetu tarehe 31 Oktoba.

Hata hivyo ,United Airlines inasema imefanya ukaguzi uliohitajika na FAA kwenye baadhi ya ndege zake za 737 Max 9.

Na kuziondoa baadhi ya ndege zake kutoa huduma kulitarajiwa kusababisha kuahirishwa kwa takribani safari 60 siku ya Jumamosi, shirika hilo la ndege lilisema katika taarifa.

Shirika la ndege la Turkish Airlines limesitisha safari zake tano za 737 Max 9.

Imetafsiriwa na Esther Namuhisa na kuhaririwa na Maryam Dodo Abdalla