Tazama picha za Malkia Elizabeth II na matukio yake barani Afrika

Queen

Chanzo cha picha, Getty Images

Malkia Elizabeth II alitembelea zaidi ya nchi 20 za Kiafrika wakati wa utawala wake, ambayo ilishuhudia Dola ya Uingereza ikifika tamati na bara hilo kujpatia uhuru. Kiungo maalum kilicholiungaisha bara hilo na Uingereza ni kupitia Jumuiya ya Madola, ambayo Malkia aliongoza. Ulikuwa uhusiano wa karibu - na wakati mwingine mgumu - kati ya ufalme wa Uingereza na Afrika baada ya ukoloni.

Queen

Chanzo cha picha, Getty Images

Binti mfalme Elizabeth alitangaza kutoka kwenye bustani moja ya Jumba la Serikali huko Cape Town, Afrika Kusini katika siku yake ya kuzaliwa ya 21, akitolea maisha yake kwa ajili ya huduma ya Jumuiya ya Madola.

"Kila mahali nimetembea katika nchi hii nzuri ya Afrika Kusini ... wazazi wangu, dada yangu na mimi tumepokelewa kwa moyo na watu na kuhisi kuwa kama tuko nyumbani hapa, kana kwamba tumekuwa sehemu ya maisha yao na tumeishi nao katika maisha yetu,” alisema.

Queen

Chanzo cha picha, Getty Images

Binti mfalme Elizabeth akiwa na mumewe, Duke wa Edinburgh mwaka wa 1952, kwenye Hoteli ya Treetops nchini Kenya . Siku moja baada ya kupigwa picha hii, alipata taarifa kuhusu baba yake, Mfalme George VI, amefariki na kwamba anakwenda kuwa Malkia.

Queen

Chanzo cha picha, Getty Images

Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kati ya ziara mbili ambazo Malkia Elizabeth alifanya nchini Nigeria, mwaka wa 1956, wakati ilikuwa bado koloni la Uingereza. Malkia amepigwa picha hii akiwa na Chifu Oba Adenji-Adele II huko Lagos. Pia alitembelea Calabar, Enugu, Jos, Kaduna, Kano na Port Harcourt.

Queen

Chanzo cha picha, Getty Images

Malkia Elizabeth na Mwanamfalme Philip wakiwa katika picha ya pamoja na Mtawala Haile Selassie I wa Ethiopia mjini Addis Ababa, wakati wa ziara ya kiserikali mwaka 1965.

Mfalme huyo alikimbilia Uingereza kati ya 1936 na 1941 kufuatia uvamizi wa Italia katika nchi yake na kurejeshwa kwenye kiti cha mamlaka mwaka 1941 wakati wanajeshi wa Uingereza na Jumuiya ya Madola walipowashinda Waitalia.

Queen

Chanzo cha picha, Getty Images

Malkia Elizabeth na Rais wa Sudan El Tigani El-Mahi wakiwa kwenye gari la serikali kutoka Uwanja wa Ndege wa Khartoum, mwaka wa 1965. Ziara yake nchini Sudan ilijumuisha mashindano ya mbio za ngamia na safari ya kwenda kwenye eneo la ujenzi wa Bwawa la Roseires kwenye mto Blue Nile, ambalo lilikuwa linatarajiwa kukamilika mwaka uliofuata.

Queen

Chanzo cha picha, Getty Images

Malkia akiwa na Rais wa Tanzania Julius Nyerere mwanzoni mwa ziara ya kiserikali ya siku tatu mwaka 1979. Miaka kumi na minane nyuma, Mwalimu Nyerere aliiongoza iliyokuwa koloni la Uingereza, Tanganyika kupata uhuru, na kuwa waziri mkuu wake wa kwanza na baadaye rais wake wa kwanza.

Kwa miaka mingi, akawa ni mtu aliyetofautiana na Uingereza na Ulaya. Hata hivyo, serikali ya Uingereza ilimwona kama nguvu kuu ya kuleta utulivu katika eneo linalozidi kuwa na msukosuko.

Queen

Chanzo cha picha, Getty Images

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe alitunukiwa tuzo ya heshima na Malkia mwaka wa 1994. Lakini mvutano ulipozidi kukua kati ya Zimbabwe na serikali ya Uingereza kuhusu mpango wa rais wa mageuzi ya ardhi na madai ya ukiukaji wa haki za binadamu, Zimbabwe ilijiondoa katika Jumuiya ya Madola mwaka 2003. Bw Mugabe alivuliwa hadhi ya tuzo hiyo mwaka 2008.

Queen

Chanzo cha picha, Getty Images

Malkia Elizabeth anaonekana pichani akiwasili katika uwanja wa ndege wa Durban mwaka wa 1995. Alikuwa katika ziara rasmi ya siku sita nchini Afrika Kusini, ambayo ilishuhudia msimu bora wa mvua katika miaka 10, na kumpatia jina la utani la Motlalepula, ambalo linamaanisha "kuja na mvua".

Queen

Chanzo cha picha, Getty Images

Malkia na rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, walisemekana kuwa na urafiki wa karibu. Hata barua za Malkia kwenda kwa Rais Mandela zilisainiwa mwishoni kwa maneno "Rafiki yako wa dhati, Elizabeth R" na inaonekana akimtaja kama "Nelson", huku ikisemekana kuwa alimwita na yeye alimwita kwa kifupi "Elizabeth" ikiwa ni tofauti na itifaki ya kifalme.

Queen

Chanzo cha picha, Getty Images

Malkia alitembelea Nigeria kwa mara ya pili mwaka wa 2003. Nchi hiyo ilikuwa imesimamishwa kutoka Jumuiya ya Madola kutokana na ukiukwaji wa haki za binadamu wakati wa utawala wa kijeshi wa Sani Abacha mwaka 1995 na ilikubaliwa tena kurejeshewa uanachama wake mwaka 1999 baada ya kurudi kwa utawala wa kiraia.

Malkia na Rais Olusegun Obasanjo wanaonekana hapa kwenye ufunguzi rasmi wa mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola huko Abuja.

Queen

Chanzo cha picha, Getty Images

Katika safari yake ya mwisho barani Afrika, mwaka 2007, malkia huyo wa Uingereza aliyetawala kwa muda mrefu zaidi alikutana na mmoja wa marais waliokaa muda mrefu zaidi barani Afrika, Yoweri Museveni, ambaye amekuwa madarakani tangu 1986.

Huko nyuma aliwahi kuzuru Uganda mara moja- katika ziara yake ya kwanza ya kiserikali, kutembelea Afrika kama Malkia, mwaka 1954.