Ugomvi wa mke na mume walazimisha ndege inayoelekea Thailand kutua India

Chanzo cha picha, REUTERS
Ndege hiyo ilikuwa njiani kutoka Munich, Ujerumani kuelekea Bangkok, mji mkuu wa Thailand, ilitua katika Uwanja wa Ndege wa Indira Gandhi nchini India, wakati mzozo wa maneno kati ya mwanaume na mwanamke ulipozidi.
Maafisa wanasema ndege hiyo ilifika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Indira Gandhi siku ya Jumatano. Kwa mujibu wa maafisa wa usafiri wa anga wa Uwanja wa Ndege wa Delhi, sababu ya mgogoro kati ya mume na mke haijajulikana, lakini kutokana na mgogoro wao, ndege iliacha kwa muda kuendelea na safari.
Shirika la ndege la Lufthansa Airlines, lilisema katika taarifa yake - mume wa mwanamke huyo alitolewa nje ya ndege baada ya kutua India badala ya Bangkok. Shirika hilo pia lilisema, "mwanaume huyo aliomba msamaha.''

Chanzo cha picha, REUTERS
Inasemekana wafanyakazi wa ndege awali waliomba ruhusa ya kutua Pakistan, lakini baada ya kushindikana, rubani aliichukua ndege hadi Delhi. Abiria huyo alikabidhiwa kwa maafisa wa usalama wa Delhi.
Taarifa zinasema abiria waliokuwa wakigombana ni Mjerumani na mkewe mkaazi wa Thailand, na kwa mujibu wa gazeti la Indian Express, mwanamke huyo alilalamikia kwa wafanyakazi wa ndege kuhusu tabia zisizofaa za mumewe.
Katika ripoti ya shirika la habari la PTE, inaeleza mwanaume huyo, "kwanza alitupa chakula kinachotolewa kwenye ndege, kisha akajaribu kuchoma blanketi kwa kibiriti, na katika harakati hizo alimtukana mkewe.''
Kulingana na ripoti ya PT, mtu huyu alikataa kukubali maagizo ya wafanyakazi wa ndege. Ndipo alipotolewa katika ndege na kukabidhiwa kwa maafisa wa usalama.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












