Tunachofahamu kuhusu kikosi cha jeshi la Israel kitakachowekewa vikwazo na Marekani
By Alhareth Alhabashneh
BBC News Arabic

Chanzo cha picha, NAHAL HAREDI
Marekani inakusudia kuweka vikwazo kwa kikosi cha "Netzah Yehuda," moja ya vikosi vya jeshi la Israel, ambacho kilifanya operesheni nyingi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.
Hii ni mara ya kwanza (ikiwa vikwazo hivyo vitawekwa rasmi) kwa utawala wa Marekani kuweka vikwazo kwa kikosi cha jeshi la Israel kutokana na ukiukaji wa haki za binadamu.
Jeshi la Israel lilisema siku ya Jumapili "halifahamu vikwazo vyovyote vya Marekani" kwa kikosi cha Netzah Yehuda, na kuongeza kuwa kikosi chake "kinafanya kazi kwa mujibu wa sheria za kimataifa."
Iwapo Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani itaweka vikwazo kwa Kikosi cha Netzah Yehuda, itakuwa ni marufuku kupokea aina yoyote ya usaidizi wa kijeshi wa Marekani au mafunzo.
Majibu ya Viongozi wa Israel

Chanzo cha picha, Reuters
Taarifa hiyo kutoka Washington ilijibiwa kwa hasira na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu akisema, ''ikiwa kuna mtu anafikiri ataweka vikwazo kwa kikosi cha Jeshi la Israel, nitapambana navyo."
Waziri katika Baraza la Vita Benny Gantz alisema kuweka vikwazo ni "jambo la hatari," na kutoa wito kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Anthony Blinken, kutafakari upya jambo hilo.
Waziri wa Usalama wa Kitaifa wa Israel, Itamar Ben Gvir,, alitoa wito wa kushikiliwa fedha zote za Mamlaka ya Palestina zinazotumwa kupitia Israel ili kujibu vikwazo vilivyopendekezwa na Washington.
Ben Gvir anaamini vikwazo vitakavyowekwa ni kwa maslahi ya maadui wa Israel.
Waziri katika Baraza la Vita, Gadi Eisenkot, alisema kuweka vikwazo kwa kikosi hicho ni jambo baya na aliahidi kufanya kazi kuzuia uamuzi huo.
Waziri wa Fedha wa Israel Bezalel Smotrich alieleza hatua hiyo kama "wazimu kabisa na jaribio la kulazimisha taifa la Palestina."
Kiongozi wa upinzani wa Israel, Yair Lapid, alisema vikwazo dhidi ya Brigedia ya Netzah Yehuda ni kosa ambalo linapaswa kuepukwa.”
Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi cha Israel, Merav Michaeli, alitoa wito wa kuvunjwa kwa Brigedi ya Netzah Yehuda, akisema kikosi hicho "kinajulikana kwa tabia yake ya vurugu na rushwa kwa miaka mingi."
Brigedia ya Netzah Yehuda ni ipi?

Chanzo cha picha, BATTALION WEBSITE
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Jamii ya Wayahudi wa Haredi ilikataa kujiunga na jeshi la Israel, kwa sababu wanatumia wakati wao mwingi, kujifunza Torati na tafsiri za vitabu vya kidini.
Lakini baadae ilikubalika kuwaingiza jeshini baadhi ya vijana wa Kiharedi chini ya masharti maalumu wakati pia wakiendelea kufanya kazi ya kidini.
Nahal Haredi, shirika lisilo la serikali, lililoanza kufanya kazi mwaka 1999 - likiwa na wanachama wa Haredi, waliokuwa wakifanya kazi na Idara ya Usalama wa Jamii ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Israel ili kuwahudumia vijana wa Haredi.
Ushirikiano huu ulisababisha kuundwa kwa Kikosi cha Netzah Yehuda, ambapo maelfu ya askari wa Haredi kwa sasa wanahudumu katika maeneo mbalimbali ya Israel.
Mwaka 1999, kitengo cha kwanza cha askari 30 wa Haredi kiliundwa na kuitwa "Nahal Haredi," "Netzah Yehuda," au "Battalion 97," kutoka jina la shirika la kiraia ambalo lilikuwa na wazo la kuwaingiza vijana wa Haredi katika jeshi.
Mwaka 2019, gazeti la Kiebrania, Yedioth Ahronoth liliripoti kwamba jeshi la Israel liliamua kukihamisha kikosi cha Yehuda, kutoka Ramallah hadi Jenin.
Disemba 2022, Israel ilikihamisha kikosi hicho kutoka Ukingo wa Magharibi, ingawa jeshi lilikanusha kwamba lilimechukua hatua hiyo kutokana na tabia ya askari wa kikosi hicho, na tangu wakati huo kikosi hicho kimekuwa kikifanya kazi kaskazini.
Mapema mwaka 2024, kikosi hiki kilianza kupigana huko Gaza, kulingana na ripoti ya gazeti la Israel, the Jerusalem Post.
Hivi sasa, askari wapatao 1,000 wanafanya kazi chini ya amri ya Kikosi cha Netzah Yehuda. Askari wake hutumikia kwa miaka miwili na miezi minane katika jeshi la Israel.
Wanajeshi wa kikosi hicho hawaingiliani na wanajeshi wa kike, na wanapewa muda wa ziada wa maombi na masomo ya kidini, kulingana na Times of Israel.
Tatizo limeanzia wapi?

Chanzo cha picha, Getty Images
Wanachama wa Brigedi ya Netzah Yehuda walituhumiwa kumuuwa mzee mwenye uraia wa Palestina na Marekani, Omar Asaad (79), Januari 2022, baada ya kumkamata karibu na kizuizi cha ukaguzi.
Familia yake ilieleza kuwa askari hao walimfunga mikono yake, wakamziba na mdomo, na kumwacha chini, usiku kwenye baridi kali, saa chache baadaye alikutwa amekufa.
Baada ya kuchunguza tukio hilo, IDF ilitangaza kumekuwa na "kufeli kwa maadili ya askari hao na kutokea makosa katika uamuzi."
Kufuatia tukio hilo, kamanda wa kikosi cha Netzah Yehuda alikemewa, na makamanda wawili wa zamu waliondolewa, na uchunguzi wa jinai uliofunguliwa dhidi ya askari hao ukafungwa bila ya wao kufikishwa mahakamani.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilianza kuchunguza Kikosi cha Netzah Yehuda mwishoni mwa 2022 baada ya wanajeshi wake kuhusika katika matukio kadhaa ya unyanyasaji dhidi ya raia wa Palestina.
Mojawapo ikiwa ni kifo cha Asaad, kulingana na ripoti iliyochapishwa na gazeti la Haaretz.
Tangu kuanza kwa vita vya Israel katika Ukanda wa Gaza tarehe 7 Oktoba, Marekani imetoa vikwazo dhidi ya walowezi kadhaa kutokana na vitendo vya ukatili dhidi ya Wapalestina.
Sheria ya Leahy

Chanzo cha picha, Getty Images
Sheria ya Leahy inakataza Marekani kutoa usaidizi, ikiwa ni pamoja na mafunzo kwa vitengo vya usalama, kijeshi na polisi vya serikali mbalimbali za kigeni - ikiwa vitengo hivyo vimekiukaji haki za binadamu.
Msaada wa kigeni wa Marekani unaweza kuanza tena ikiwa wanachama waliohusika na ukiukaji huo watafikishwa mahakamani.
Sheria ya Leahy inatumika tu kwa "msaada unaotolewa kwa vitengo maalumu, na haiathiri kiwango cha msaada unaotolewa kwa taifa la kigeni."
Serikali ya Marekani inachukulia mateso, mauaji ya kiholela, kutoweka kwa nguvu, na ubakaji kuwa ni ukiukaji wa haki za binadamu, na sheria ya Leahy hutumika pindi uhalifu huu unapothibitishwa.
Sheria ya Leahy imepewa jina la mtu ambaye alitoa wazo la kuanzishwa kwake, ambaye ni Seneta Patrick Leahy, mwishoni mwa miaka ya 1990.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












