''Tower 22'': Ifahamu kambi ya kisiri ya jeshi la Marekani ilioshambuliwa Jordan

Chanzo cha picha, PLANET LABS/AP
Wanajeshi watatu wa Marekani waliuawa na makumi walijeruhiwa baada ya ndege isiyo na rubani kushambulia kituo cha kijeshi huko Jordan.
Kituo hicho cha Tower 22, kiko katika eneo la Al-Tanf ambalo ni muhimu kimkakati, ni sehemu ya kaskazini mashariki - ambapo mipaka ya nchi hiyo inakutana na Syria na Iraq.
Moja ya jukumu la kituo hicho ni kutoa usaidizi. Kuna wanajeshi 350 wa Jeshi la Marekani na Jeshi la anga kwenye kituo hicho.
Kituo hicho kiko karibu na makao makuu ya jeshi katika kambi ya Al-Tanf, ambayo iko upande wa Syria wa mpaka wa Jordan.
Al-Tanf ilikuwa muhimu katika vita dhidi ya ISIS na ilichukua jukumu kama sehemu ya mkakati wa Marekani kudhibiti makundi yanayoungwa mkono na Iran nchini Syria.
Vikosi vya Marekani huko Jordan

Chanzo cha picha, US DEPARTMENT OF DEFENSE
Jeshi la Jordan ni mojawapo ya wanufaika wakubwa wa mfumo wa Marekani wa ufadhili wa kijeshi.
Ufalme huo una mamia ya wakufunzi wa Kimarekani na ni mmoja wa washirika wachache wa kikanda ambao hupokea mafunzo ya kutoka vikosi vya Marekani.
Tangu kuanza kwa mzozo wa Syria mwaka 2011, Washington imetumia mamilioni ya dola kusaidia Jordan kuanzisha mfumo wa ufuatiliaji unaojulikana kama Mpango wa Usalama wa Mipaka ili kukomesha uingiaji wa wanamgambo kutoka Syria na Iraq, kulingana na shirika la habari la Reuters.
Haijulikani ni aina gani ya silaha zilizowekwa kwenye kituo hicho na pia haijulikani ni ulinzi gani wa anga unaotumika.
Idara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon), ilisema katika taarifa yake kwamba shambulio hilo lilisababisha vifo vya wanajeshi watatu wa Marekani na idadi ya waliojeruhiwa iliongezeka hadi 34.
Pentagon ilisema shambulio hilo lilikuwa "la moja kwa moja la ndege zisizo na rubani kwenye kituo kilicho kaskazini mashariki mwa Jordan karibu na mpaka wa Syria."
Kwa upande mwingine, serikali ya Jordan imelaani shambulizi hilo, karibu na kambi ya Al-Tanf.
Idara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon, ilisema shambulio hilo lilitokea "kwenye kituo cha kijeshi cha Tower 22, ambacho kipo karibu na kambi kuu ya kijeshi ya Al-Tanf.
Taarifa iliyotolewa na Pentagon ilieleza "takriban wanajeshi 350 wa Jeshi la Merekani, waliowekwa kwenye kituo hicho."















