Uchaguzi wa Chadema: Lissu aibuka kidedea, Mbowe ampongeza

Lissu na Mbowe

Chanzo cha picha, Chadema

Muda wa kusoma: Dakika 5

Tundu Lissu amechukua usukani wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Chadema.

Lissu amemng'oa madarakani Freeman Mbowe ambaye amekiongoza chama hicho kama mwenyekiti kwa miongo miwili.

Mbowe amekuwa wa kwanza kukiri kushindwa na kumpongeza Lissu kupitia mtandao wa X.

Timu ya kampeni ya Lissu pia imetumia mtandao wa X kutangaza ushindi wake.

Matokeo rasmi ya uchaguzi huo uliofanyika Jumanne usiku yanaonesha kuwa Lissu amepata 51.5% ya kura zote dhidi ya 48.3% alizozipata Mbowe.

Mara baada ya wagombea wakuu Mbowe na timu ya kampeni ya Lissu kutuma salamu za matokeo kupitia mtandao wa X, wakala wa Lissu kwenye uchaguzi huo na aliyekuwa Mbunge wa Arusha Godbless Lema aliwaambia waandishi wa Habari kuwa Chadema ndiyo imeshinda.

"Chama kimeonesha demokrasia iliyokomaa… huu ulikuwa uchaguzi huru n awa haki kabisa, na umerushwa mubashara na vyombo vya habari. Watu wote wameliona hilo," amesema Lema.

Soma pia:

Lissu ampongeza Mbowe

Mwenyekiti mpya wa Chadema Tundu Lissu baada ya kutangazwa mshindi amesema chama hicho kimeweka kiwango cha dhahabu cha demokrasia ya ndani na kuvitaka vyama vingine vya siasa nchini humoi kuiga mfano wao.

Kissu amesema uchaguzi huo ulikuwa wa wazi, huru na haki bila mizengwe japo amekiri kuwa kulikuwa na misuguano na kasoro za hapa na pale.

"Tumefanya jambo ambalo halijawahi kufanywa toka chama chetu kianzishwe… tumeweka kiwango cha dhahabu – tunawaambia vyama vingine kama vinaweza viige," ameeleza Lissu.

Lissu pia alitumia hotuba yake hiyo ya kwanza kama mwenyekiti kumshukuru mtangulizi wake Freeman Mbowe akisema alichukua kjiti cha uongozi wa chama hicho wakiwa na wabunge watano na katika uongozi wake amekifanya kuwa chama kikuu cha upinzani Tanzania.

Lissu pia amesema Mbowe ndiye aliyefanikisha uchaguzi wa jana na leo kuwa huru na haki na anastahili pongezi. "Historia ya chama chetu itakapoandikwa, watatambua huu mchango wako mkubwa uliotoa."

Mwenyekiti huyo mpya amesema Mbowe hajastaafu na ataendelea kuwa mjumbe wa kudumu wa kamati kuu ya chama hicho kama ambavyo katiba ya Chadema inavyoainisha.

Mbowe 'amuagiza' Lissu kutibu majeraha

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Freeman Mbowe, mwenyekiti wa Chadema anayemaliza muda wake baada ya kushindwa katika uchaguzi na Tundu Lissu amesema mchakato wa uchaguzi huo umekiacha chama hicho na majeraha.

Mbowe amesema japo uchaguzi umefanyika katika misingi ya uhuru, haki na uwazi kama ambavyo aliahidi awali lakini amesema mchakato wa kampeni umeacha majeraha na amemtaka Lissu na viongozi wengine waliochaguliwa kuleta maridhiano ndani ya chama.

"Mimi niliahidi kuwa kama ningeshinda ningeliunda kamati ya ukweli na maridhiano ili watu wazungumze na kutibu majeraha yaliyoletwa na kampeni … sasa kama mnaniheshimu kama baba, basi nawaagiza Lissu na viongozi wenzako wapya mlete maridhiano baada ya majeraha yaliyoletwa na kampeni," amesema.

Mbowe pia amewataka viongozi wapya kusimama na katiba ya chama hicho na kujizui kuwa na kiburi.

Kuhusu mustakabali wake kisiasa, Mbowe amesema anachukua likizo na ataendelea kujikita katika kufanya biashara zake na kuendelea kukishauri chama. "Nimepewa likizo ya lazima, na nitaenda kwenye biashara zangu nitafute pesa ana nitaendelea kutoa ushauri kwa chama…Nashukuru nimepewa likizo hii kidemokrasia na katika mfumo ambao nimeujenga mwenyewe… kuna watu waliniambia nijitoe kwenye uchaguzi nitaadhirika, nikawaambia nitafia demokrasia."

Kampeni kali

Mbowe na Lissu

Chanzo cha picha, Chadema

Kumalizika kwa uchaguzi huu kunahitimisha takribani kipindi cha mwezi mmoja cha kampeni kali kati mwenyekiti Mbowe anayeondoka madarakani dhidi ya makamu wake, Lissu. Lissu aliendesha kampeni zake akijielekeza kwenye kuleta mabadiliko ya namna Chadema inavypendesha shughuli zake za kisiasa.

Anamtuhumu Mbowe akidai amebadilika mno tangu alipotoka gerezani alikokuwa ameshkiliwa kwa miezi 8 akikabiliwa kesi ya Ugaidi.

Pia anamtuhumu Mbowe kwa kupokea fedha kutoka kwa watu walio karibu na serikali, japo hakuwahi kutoa ushahidi wowote.

Mbowe alikuwa akisema kuwa bado ana kazi ya kufanya kukiimarisha zaidi chama huku akimwita Lissu muongo anayewachafua watu bila ushahidi

Hata hivyo, wawili hao waliuambia mkutano mkuu wa chama wakati wa kuomba kura kuwa watabakia ndani ya chama bila ugomvi, bila kujali matokeo ya uchaguzi.

Lakini wafuatiliaji wa masuala ya siasa za Tanzania wanasema kuna hatari ya Chadema kudhoofika na kugawanyika kutokana na tuhuma ambazo viongozi hao wawili walitupiana wakati wa kapeni za uchaguzi.

Tundu Lissu ni nani?

Tundu Lissu ni mwanasheria maarufu nchini Tanzania, na aliwahi kuwa Rais wa chama cha wanasheria Tanganyika(TLS), mwaka 2020 aligombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chadema na kushindwa na mgombea wa chama tawala John Magufuli, aliyefariki dunia Machi 2021.

Lissu aliyenusurika kifo Septemba 2017 baada ya kushambuliwa kwa risasi mjini Dodoma, ni maarufu kwa siasa za mapambano na ''ulimi mkali'' hali ambayo mara imemuweka katika mabishano makali na wanasiasa wezake hususan wa chama tawala. Amekuwa akisema alipopigwa risasi alikuwa ''nusu mfu''

Kuanzia mwaka 2010 Lissu alikuwa mbunge wa Singida Mashariki na alijipatia umaarufu kwa michango yake bungeni hususan ya kuikosoa serikali ya Rais Jakaya Kikwete na baadaye Hayati Rais John Pombe Magufuli.

Lissu ni msomi wa kiwango cha shahada ya umahiri aliyoipata nchini Uingereza katika Chuo Kikuu cha Warwick kati ya mwaka 1995 na1996. Kabla ya hapo alipata shahada ya kwanza ya sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alikohitimu mwaka 1994.

Maisha yake yamekuwa zaidi katika harakati za kutetea haki za binadamu na kutoa msaada wa kisheria kwa watu wenye mahitaji lakini wana uwezo mdogo wa kifedha. Aliwahi pia kuwa mwenyekiti wa chama wanasheria za Mazingira Tanzania (LIT) katika miaka ya 1990.

Lissu mpambanaji

Lissu

Chanzo cha picha, Chadema

Jambo moja ambalo utalipata kuhusu Tundu Lissu kutoka kwa watu wake wa karibu ni kwamba ni mtu ambaye siku zote hakuwahi kuwa mpole au mwenye kufanya mambo yake kimyakimya.

Hadithi za matukio yake akiwa mwanafunzi katika shule za Ilboru (shule ya wanafunzi wenye vipaji maalumu kiakili) na baadaye Umbwe, zinamuelezea kama mwanafunzi mtundu, mahiri katika mijadala na ambaye uwezo wake kitaaluma darasani haukuwahi kutetereka kutokana na matukio yake mengi ya nje ya madarasa.

Lissu ana nguvu kubwa mbili za kuzaliwa ambazo hakuna shule inayoweza kumfundisha mtu; ujasiri na umahiri wa kuzungumza. Kwa Lissu, vyote viwili amejaliwa kuwa navyo tangu utotoni na katika maisha yake ya utu uzima -kama mwanaharakati na mwanasiasa, amevitumia vitu hivyo kwa ufanisi mkubwa.

Ni ujasiri wake ndiyo uliompa umaarufu kwa kupambana kama mwanaharakati dhidi ya vyombo vya dola vya utawala wa Mkapa vilivyomweka jela, kumpiga na kujaribu kumnyamazisha kwa mbinu 2 tofauti.

Ni ujasiri wake ndiyo uliompambanua na wanasiasa wengine katika miaka ya mwanzo ya utawala wa Rais John Magufuli. Watanzania, kwa ujumla, ni wenye woga dhidi ya mamlaka na yeye alijipambanua kwa kuikosoa serikali hadharani; hata katika wakati ilipoonekana ni hatari kufanya hivyo.

Tofauti kubwa; baina ya Lissu na wanasiasa wengine ilikuwa kwenye uwezo wake wa kujieleza. Mbunge huyu wa zamani wa Singida Mashariki ana uwezo wa kujenga hoja na kuzieleza vizuri - kipaji kilichoungwa tangu enzi zake akiwa mwanafunzi wa Ilboru.

Pia unaweza kusoma:

Imehaririwa na Athuman Mtulya