Maandamano Tanzania: Askofu Gwajima, makada wa Chadema wasakwa na polisi

Jeshi la polisi nchini Tanzania limetangaza msako mkali wa kuwatafuta watu wanaowatuhumu kwa kupanga kuratibu na kutekeleza maandamano ya vurugu ya Uchaguzi wa Oktoba 29, 2025 katika mikoa mbalimbali nchini humo.
Katika taarifa iliyotolewa usiku wa kuamkia leo, polisi imewataja watu 10 wengi wao wakiwa wanasiasa wa chama Kikuu cha upinzani Chadema.
Miongoni mwa wanaotafutwa ni aliyekuwa mbunge wa Kawe na Mkuu wa Makanisa ya Ufufuo na Uzima Askofu Josephat Gwajima. Gwajima ni moja ya wakosoaji Wakuu wa serikali ya Rais Samia Suluhu Hassana.
Polisi wanamsaka Askofu Maxmillian Machumu ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Makanisa Ufufuo na Uzima na kiongozi wa Chadema mkoani Simiyu.
Wengine wanaotafutwa ni viongozi waandamizi wanane wa Chadema wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Chama hicho John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu Amani Golugwa, msemaji wa chama Brenda Rupia na mwenyekiti wa baraza la vijana Deogratius Mahinyila.
Makada wengine wanaosakwa ni Godbless Lema, Boniface Jacob, Award Kalonga na mwanaharakati Hilda Newton.
''Jeshi la Polisi linawataka kujisalimisha katika vituo vya polisi mara moja''ilieleza taarifa hiyo.
Katika hatua nyingine Polisi imeeleza hatua za kisheria kwa wanaotuhiwa kwa uhalifu ambao wamekwisha kamatwa zinaendelea kote nchini Tanzania na kwamba tarehe 7 Novemba 2025 baadhi wamefikishwa mahakamani.

Chanzo cha picha, Reuters
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
''Tunapenda kujulisha umma kuwa waendelee na shughuli zao bila hofu yoyote,na watoe taarifa mara moja wanapoona dalili yoyote ya uhalifu ama uvunjifu wa amani mahali popote pale ili hatua kwa mujibu wa sheria ziweze kuchukuliwa.''
Kwa mujibu wa polisi
Katika maandamano yaliyodumu kwa siku tatu kuanzia Oktoba 29, 2025 siku ya uchaguzi, watu kadhaa wamepoteza maisha huku mali za umma na binafsi zikahariwa.
Waandamanaji walikuwa wakitaka mabadiliko mbalimbali ikiwemo mifumo ya uchaguzi na usimamizi wa haki lakini mamlaka nchini Tanzania si adai maandamano hayo yalikuwa kinyume cha sheria na yaligubikwa na ghasia na uharibifu.
Bado taarifa rasmi haijatolewa kuhusu tathmini ya madhara yaliyotokea kutokana na maandamano hayo makubwa zaidi kuwahi kutokea kuhusu uchaguzi tangu nchi hiyo ipate uhuru miongo ya sita iliyopita.
Duru mbalimbali za ndani na nje ya Tanzania ikiwemo wapinzani, wanaharakati na wanadiplomasia zinaeleza kuwa mamia ya watu wameuawa na vyombo vya usalama ikiwemo polisi. Serikali ya Tanzania imekanusha madai hayo.
Maandamano hayo yaliyoanzia jijini Dar es Salaam na kusambaa katika maeneo mengine ikiwemo majiji ya Arusha, Mwanza, Mbeya, na Dodoma, na maeneo ya mikoa mingine yamesababisha uharibifu mkubwa wa miundo mbinu ya umma na binafsi, ikiwemo vituo vya Polisi, ofisi za umma zikiwemo za chama tawala (CCM), vituo vya mafuta na maduka kadhaa.















