Maandamano Tanzania: 'Nilikimbia kivyangu na mume wangu kivyake'

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 2

''Nilipatwa na hofu kuu kushuhudia mtoto wa jirani alitumwa kwenda kununua maji alikutana na risasi akafa'' kwakweli hali haikuwa nzuri ikabidi tukimbie.. Watoto niliwaacha tu nilipoona hali imekuwa mbaya, anaeleza Atuganile Mwaki sio majina yake halisi.

Baadhi ya raia wa Tanzania kutoka nyanda za juu kusini mwa nchi hiyo wamesimulia namna walivyolazimika kukimbilia nchi jirani ili kunusuru maisha yao kufuatia machafuko yaliyoibuka baada ya maandamano ya siku ya uchaguzi.

Maandamano hayo, yaliyoanza Oktoba 29, 2025, yameathiri maeneo mbalimbali nchini, na kusababisha vifo vya mamia ya watu.

Hali hiyo imeibua hisia za wasiwasi miongoni mwa wananchi waliokuwa wakitaka mabadiliko katika mifumo ya uchaguzi, usimamizi wa haki, na utawala wa kidemokrasia.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

''Nilikimbilia mpakani nikaingia nchi jirani tunalala stendi ya mabasi hapa Mpika kuna wafanyavbiashara wengi usiku na mchana tuko salama hapa kuliko nyumbani''

Atuganile Mwaki mama na mke anasema amewaacha watoto wake nyumbani Tanzania baada ya kushuhudia watu waliokuwa na silaha walionekana wakiingia majumbani na kufyatua risasi au kuwapa kipigo.

''Ninasubiri kukitulia kidogo nitarejea kwani watoto niliwaacha baada ya kuona watu wazima wakilengwa zaidi,''alisema Mwaki.

Kwa mujibu wa mashuhuda, wananchi wamekuwa wakikimbia maeneo yao, huku wengine wakiwa na hofu kubwa kutokana na vurugu zilizoambatana na maandamano hayo.

Malafyale Moses ambaye sio majina yake halisi ni mfanya biashara kutoka Iringa ambaye ameeleza kuwa safari yake mkoani Mbeya kuchukua mzigo ilibadilika na kukimbilia nchi jirani ili kupata hifadhi salama.

Kilichomuogopesha zaidi ni wanaume kuonekana kulengwa zaidi na washambuliaji jambo lililofanya kuacha mali zake na kuvuka mpaka wa Tanzania.

Mimi nilipita mto Songwe nikakimbilia Malawi na baadae kuvuka hadi Lusaka,nitakaa huku kwa mwezi mzima.

'Ni kweli serikali imesema hali ni shwari turejee lakini kwa mimi na maono yangu siamini hadi pale nitakapojiridhisha mwenyewe ndipo nitarejea nyumbani'

Maelezo ya sauti, Maandamano Tanzania: 'Nilikimbia kivyangu na mume wangu kivyake'
.

Chanzo cha picha, Getty Images

Uchaguzi wa mwaka 2025 umejikita katika masuala ya kisiasa, haki za binadamu, na mapambano ya kidemokrasia, lakini kwa wengi, vurugu za baada ya uchaguzi zimekuwa ni kipimo kigumu cha uvumilivu na matumaini ya mustakabali wa kisiasa nchini Tanzania.

Mnamo Novemba tarehe 4, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Nchini Tanzania (THBUB) imesema itaanzisha uchunguzi wa kina kufuatia maandamano yalioshuhudiwa wakati wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025, na kusababisha uharibifu wa mali na vifo vya raia.

Rais Samia Suluhu alitangazwa mshindi katika uchaguzi wa Tarehe 29 Oktoba 2025, lakini Chama cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA ambacho kiongozi wake Tundu Lissu anazuiliwa jela kwa tuhuma za uhaini, kilipinga matokeo hayo na kudai kuwa uchaguzi huo ni kejeli kwa demokrasia.