Operesheni ya kumuokoa chura mkubwa zaidi duniani

Cedric Fogwan amemshikilia mmoja wa vyura wa goliath aliyevunja rekodi

Chanzo cha picha, JEANNE D'ARC PETNGA

Cedrick Fogwan alipokutana kwa mara ya kwanza na chura wa goliath alivutiwa na ukubwa wake.

Alikua hadi ukubwa wa paka, ndiye chura mkubwa zaidi ulimwenguni.

Karibu kama kushika mtoto (wa binadamu), anasema, akiwa amemshughulikia mmoja katika misheni ya uokoaji.

Mhifadhi huyo wa Cameroon alivutiwa sana kiasi kwamba alianzisha mradi wa kupigania mustakabali wa viumbe vilivyo hatarini kutoweka.

"Nilipogundua spishi hii ni ya kipekee, kubwa zaidi ulimwenguni, nilisema hili ni jambo ambalo hatuwezi kupata mahali pengine kwa urahisi na nilijivunia," anasema.

"Watu katika eneo hilo wanasema wamebarikiwa kuwa na kitu kama hicho; wanakiambatanisha na thamani ya kitamaduni."

 Vyura wa Goliath wanaweza kuwa wakubwa kama paka wa kufugwa, wakiwa na urefu wa hadi 32cm na uzani wa zaidi ya kilo 3.25

Chanzo cha picha, CEDRICK FOGWAN

Kwa miongo kadhaa, chura wa goliath amekuwa akiwindwa kupita kiasi kwa ajili ya chakula na biashara ya wanyama vipenzi nchini Cameroon na Guinea ya Ikweta.

Makazi yake kando ya mito na vijito yanaharibiwa haraka na chura huyo sasa ameainishwa kuwa yuko hatarini kutoweka kwenye Orodha rasmi ya wanyama wanaotoweka.

Chura huyo hajulikani sana na sayansi na hata nchini Cameroon wenyeji wengi hawajui thamani yake kwa mfumo wa ikolojia, kama vile kuwinda wadudu wanaoharibu mazao

Chura huishi kando ya vijito

Chanzo cha picha, JEANNE D'ARC PETNGA

Timu ya uhifadhi inafanya kazi kuwashawishi wawindaji kuwa wanasayansi raia, kurekodi kuonekana kwa chura badala ya kumtumia kama chakula.

Pia wanafanya kazi na vikundi vya wenyeji kusaidia kuanzisha ufugaji wa konokono ili kutoa chanzo mbadala cha chakula.

Kazi ya uhifadhi inaanza kuzaa matunda, huku chura wa goliath akirejea kwenye mito mipya katika Hifadhi ya Mlima Nlonako.

Simu kutoka kwa mwindaji haramu wa zamani kuripoti kuwa chura alikuwa amekamatwa na jirani ilikuwa hatua ya mabadiliko. Cedric aliweza kumuokoa chura huyo na kumrudisha porini.

"Ninaamini tunaweza kuwa nayo milele na tunaweza kuendelea kujivunia," anasema.

Mradi wa kuokoa chura wa goliath unaungwa mkono na Mpango wa Uongozi wa Uhifadhi (CLP) unaoendeshwa na Fauna & Flora International, BirdLife International na Jumuiya ya Kuhifadhi Wanyamapori.