Wazee wachapwa viboko katika Makao ya Wazee ya PCEA Thogoto Kenya

.

Chanzo cha picha, BBC Africa Eye

Wakazi walio katika mazingira magumu katika makao ya wazee karibu na mji mkuu Kenya, Nairobi wamekuwa wakinyanyaswa na kutelekezwa, uchunguzi wa BBC Africa Eye umefichua.

Upigaji picha wa siri unaonyesha wafanyikazi wakiwatesa wakazi, wakitupa chakula moja kwa moja kwenye meza bila sahani yoyote, na kuwaacha bila matibabu.

"Mchape katika makalio. Mpige," mfanyikazi mmoja anamsihi mfanyakazi mwenzake aliyeshika fimbo, katika Kanisa la Presbyterian Church of East Africa (PCEA) Thogoto Care Home for the Aged, takriban kilomita 20 (maili 12) magharibi mwa Nairobi.

Picha za siri zinaonyesha kwamba muda mfupi kabla, wafanyakazi watatu waliovalia sare za rangi ya zambarau, wanamzingira mwanamke mzee karibu na lango la chuma lililozungukwa na mabati pembezoni mwa bustani ya nyumba hiyo.

"Ulikuwa unaelekea wapi upande huo?" anauliza mmoja wa wafanyakazi. "Uliitwa ukakataa kurudi."

Ajuza huyo aliyevalia kofia, anaonekana kuchanganyikiwa na kuogopa.

"Oh, tafadhali nisamehe," anasema.

"Sasa inabidi tukuchape," anasema mmoja wa wafanyakazi.

Mfanyikazi mmoja anaonekana akimchapa mwanamke huyo mzee kwenye makalio yake kwa kutumia fimbo ya mbao.

Maelezo ya video, Africa Eye: Wazee wanavyonyanyaswa katika Makao ya Wazee Kenya

Huu ni mfano mmoja tu wa ushahidi wa unyanyasaji uliofichuliwa katika uchunguzi wa BBC Africa Eye.

Nyumba ya kuwatunza wazee hao ilianzishwa na Chama cha Wanawake cha kanisa la ndani la PCEA lakini sasa inajitegemea. Ni nyumbani kwa takriban wanawake 50 wazee na wanaume.

Katika muongo uliopita, idadi ya nyumba za wazee inaripotiwa kuongezeka mara tatu zaidi jijini Nairobi. Wengi hawatozi kodi na hutegemea makanisa ya ndani au michango.

Katika miaka 30 ijayo idadi ya wazee barani Afrika inakadiriwa kuongezeka mara tatu kutoka milioni 75 hadi milioni 235, kulingana na ripoti ya Ofisi ya Sensa ya Marekani ya 2020.

Ukuaji wake utakuwa wa haraka zaidi kuliko katika eneo lingine lolote la ulimwengu, na kufanya uwezekano wa kuwapeleka waliozeeka kwenye makao ya kuwatunza kuwa jambo halisi kwa idadi kubwa ya familia zonazoongezeka.

.
Maelezo ya picha, Msimamizi wa nyumba hiyo anasema nyumba hiyo inaongozwa na kanuni za Kikristo
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mwaka 2020, kituo cha utangazaji cha Kenya, Ebru Television, kilirekodi filamu ndani ya nyumba ya wazee ya Thogoto Care Home. Meneja, Jane Gaturu, aliwasilisha taswira ya sehemu salama, ambapo wakazi walikuwa wamelishwa vyema na kutunzwa.

BBC Africa Eye ilipata ripoti zinazotia wasiwasi kwamba haikuwa hivyo. Wanahabari wawili wa siri waliajiriwa katika nyumba hiyo na walitumia wiki 14 kupiga filamu kwa siri ndani ya kituo hicho.

Pamoja na picha za wafanyikazi wakimpiga mwanamke mzee kwa fimbo, walirekodi wafanyikazi wakikiri kuwadhulumu wakaazi wengine.

"Wakati mwingine lazima utumie nguvu," anasema mfanyakazi, akiwa ameketi nje wakati wa mapumziko ya chai.

“Hata walezi walio na upole hujikuta wakiwa wakali kwa wateja,” anasema.

Wanaendelea kuelezea kuhusu mzee mmoja ambaye "kila mara hupigwa viboko".

"Tunampiga na hilo ndilo linalomtuliza. Maana akikasirika anaweza kukupiga hata na jiwe," anasema.

Waandishi wa habari walirekodi mifano zaidi ya kupuuzwa na kutendewa vibaya, pamoja na kuachwa bila kutibiwa hali zao za kiafya. Mzee mmoja alikuwa na tatizo kubwa la ngozi.

"Ninasikia maumivu. Sana, sana. Nahisi kama ninaungua," anasikika akisema kwenye picha hiyo, akijaribu kumwonyesha ripota wa siri shingo yake. Anadai wafanyikazi wa nyuma hiyo hawatampeleka hospitali kutibiwa.

Uzito wa hali ya ngozi yake ni vigumu kubainisha katika picha za siri, lakini ripota huyo wa siri anasema alikuwa akivuja damu vibaya sana.

"Alitoa pesa kwa Jane [Gaturu, meneja wa nyumba hiyo] ili ampeleke hospitali," ripota anasema.

"Hakupelekwa hospitali. Na alipomuuliza Jane, Jane alimkasirikia sana. Na hata akamwambia: 'Nyumba yako iko karibu na kona, na watu wako wamekata tamaa. Unadhani nitaweza kukusaidia?''

"Alikuwa akiniambia: 'Tunasubiri kifo','' mwandishi anakumbuka.

Ilichukua karibu wiki sita kwa mtu huyo kuona daktari, na pesa zilizotolewa na familia yake.

..
Maelezo ya picha, Mwanamume huyo anasikika kwenye video akisema anahisi kama "anachomwa" na moto

Katika picha zilizopigwa na ripota wa siri, ngozi yake iliobadilika na juwa nyeupe imetapakaa katika mwili wake wote kuanzia kiunoni hadi juu ya shingo yake. Haijulikani ni hali gani .

Bi Gaturu alikataa kuzungumzia iwapo alipewa pesa za matibabu kisha hakufanya lolote.

Miongozo ya serikali inasema nyumba za wazee zinapaswa kutoa huduma za matibabu kwa wakaazi.

“Mimi binafsi nilikuwa na uchungu nilipowaona wakiteseka na siwezi kujizuia,” anasema mwandishi huyo wa siri.

"Nilikuwa nalia sana. Mara nyingi nilikuwa nikienda chooni. Ninazima kamera yangu na kulia."

Mmoja wa waandishi wa habari alimpiga picha mwanamke mzee akitumia mikono yake kula chakula kilichoachwa moja kwa moja kwenye meza bila sahani kwa sababu hakuweza kujilisha kwa kijiko.

Mfanyikazi wa zamani wa utunzaji alisema walishuhudia matukio kama hayo, akielezea jinsi wafanyikazi walimwambia asiwasaidia wazee hao kula chakula.

"Waliniambia nisiwasaidie leo kwa sababu hakuna mtu ambaye angewasaidia kesho," anasema.

Ripota wa siri alirekodi mazungumzo kwa siri na mfanyakazi kuhusu wafanyakazi kutowalisha wakazi walio katika mazingira magumu.

"Unadhani atakuwa wa kwanza kufa kwa njaa hapa?" mfanyakazi anamwambia.

"Wengi wamekufa kwa njaa hapa. [Walezi] wanawanyima chakula cha mchana, kuwanyima chakula cha jioni, yote kwa sababu hawataki kupata muda wa kuja kuwalisha."

.
Maelezo ya picha, ''Iwapo tutamkuta mtu yeyote akiwanyanyasa, kuwalemaza wazee hawa, ninakuhakikishia adhabu inayostahili itatolewa kwa yeyote anayefanya hivyo", afisa wa serikali anayesimamia nyumba za wazee Joseph Motari

Chakula kingi katika nyumba hiyo ni cha msaada, na mara tatu waandishi wa habari waliojificha waliona chakula kikipakiwa kwenye gari la afisa mkuu wa makaazi hayo.

Ripota wa siri pia aliulizwa kama angependa kuchukua chakula cha wakazi kutoka kwenye kituo hicho, lakini alikataa.

Mlezi wa zamani wa nyumba hiyo alidai chakula kilikuwa kikiibiwa na wafanyakazi.

"Kulikuwa na chakula ingi lakini kilikuwa kikiibiwa. Wanapakia chakula kwa gari. Wanapakia gari kwa chakula kingi kiasi kwamba gari linainama," anasema.

BBC Africa Eye ilionyesha baadhi ya rekodi za siri kwa Joseph Motari, katibu mkuu wa ulinzi wa jamii na masuala ya wazee - afisa wa serikali ya Kenya anayehusika na huduma za wazee.

"Iwapo tutakuta mtu yeyote anawanyanyasa, kuwatia vilema wazee hawa, niwahakikishie adhabu inayostahili itatolewa kwa atakayefanya hivyo," alisema.

"Tutafanya ukaguzi wa papo hapo kwenye nyumba mbalimbali za kibinafsi na kuona kama zinakidhi viwango ambavyo wanapaswa kuwa navyo. Tuko tayari kuchukua hatua dhidi ya nyumba za wazee za kibinafsi zinazowanyanyasa," aliongeza.

Tulimwelezea Bi Gaturu madai hayo.

"Nyumba nhii i shirika lisilo la faida linaloendeshwa kwa hiari ambalo lilitegemea kabisa michango kutoka kwa watu wema," alisema.

Aliongeza kuwa nyumba hiyo haina timu ya wataalamu wa matibabu na inategemea wengine kutoa huduma ya matibabu, "lakini madai kwamba hawakuwajali wakaazi ambao walihitaji matibabu ni uwongo na nia mbaya".

"Wakazi wanaotatizika kula hupewa usaidizi na yeyote anayeonekana kubeba chakula kutoka nyumbani anapaswa kufukuzwa kazi.

"Nyumba na wasimamizi haiungi mkono aina yoyote ya ukatili au unyanyasaji dhidi ya wazee. Wafanyikazi wamekuwa waathiriwa wa kushambuliwa na wakaazi.

"Nyumba kila mara huzingatia sheria na husalia kuongozwa na kanuni za dini ya Kikristo ambayo ndio chanzo chake," Bi Gaturu alisema.