Kundi la Wagner: Vyombo vya habari vya serikali ya Urusi vyamshambulia Prigozhin

Kituo cha Televisheni kinachodhibitiwa na serikali ya Urusi kimeanza kampeni inayoonekana kumkashifu kiongozi wa kundi la Wagner Yevgeny Prigozhin baada ya kushindwa kwa uasi wake mwishoni mwa mwezi Juni.

Vyombo vikuu vya habari vilionyesha picha zilizodaiwa kupigwa wakati wa msako katika nyumba yake ya kifahari nje ya mji wa St Petersburg, vikihoji kwamba utajiri wake.

Pia viliangazia uhalifu wake wa zamani na kuashiria kwamba alikuwa akiongozwa na uchoyo, lakini havikutaja ukosoaji wa mara kwa mara wa Prigozhin wa jeshi la Urusi na jinsi linavyoendesha vita huko Ukraine.

Hii ni mara ya kwanza kwa chombo cha habari cha serikali kuripoti kuhusu Prigozhin na maisha yake ya kibinafsi na maelezo mabaya kuhusu wasifu wake.

Hadi hivi majuzi, Runinga ya Urusi ingeonyesha picha nzuri ya kundi la mamluki la Wagner, ambalo limepigana pamoja na jeshi la Urusi wakati wa uvamizi wake nchini Ukraine.

Picha zinazosemekana kuwa ni za ndani ya nyumba ya Prigozhin zilionekana kwenye mtandao unaoendeshwa na serikali Rossiya 1 tarehe 5 Julai.

"Wacha tuangalie jinsi mpiganaji huyu alivyoishi, mtu ambaye ana hatia mbili za uhalifu na ambaye aliendelea kudai kuwa kila mtu alikuwa mwizi," alisema mchambuzi kwenye kipindi cha mazungumzo cha 60 Minutes.

"Hebu tuangalie jnyumba ya kifahari iliyojengwa kwa ajili ya mwanaharakati huyu dhidi ya rushwa na uhalifu," Eduard Petrov alisema kwa kejeli.

Picha hizo zilionyesha rundo la pesa taslimu, silaha mbalimbali, mambo ya ndani ya nyumba hiyo ya kupendeza na bustani kubwa - ikiwa na helikopta iliyoegeshwa, aina mbalimbali za wigi na pasipoti feki zenye majina tofauti ambazo ni dhahiri zimetolewa kwa Prigozhin.

Baadaye, picha kama hizo zilionyeshwa kama sehemu ya taarifa kuu ya habari ya jioni ya kituo, mojawapo maarufu zaidi nchini Urusi. Pia iliangazia dhahabu na "pakiti zinazotiliwa shaka za poda nyeupe", ambayo Rossiya 1 aliashiria huenda ni dawa haramu.

Pia ilingazia kwa muda mrefu juu ya uhalifu wa zamani wa Prigozhin.

Alihukumiwa mara kwanza na makosa ya jinai mwaka 1979, akiwa na umri wa miaka 18 tu, na kupewa kifungo cha miaka miwili na nusu kwa wizi. Miaka miwili baadaye, alihukumiwa kifungo cha miaka 13 jela kwa makosa ya wizi, alitumikia jela miaka tisa.

"Wanasema kwamba ni uzoefu aliyopokea kutoka kwa wahalifu sugu alipokuwa gerezani ndio ulimsaidia kutembea kutoka kwa muuzaji wa mbwa hadi kuwa kiongozi mwenye mamlaka ," mwandishi wa Rossiya 1 alicheka, akirejelea jukumu la zamani la Prigozhin kama mtunzi wa Kremlin.

Jukumu hili pia lilimpatia jina la utani "mpishi wa Kremlin".

Moja ya picha zilizoonyeshwa na TV ya serikali ya Urusi ilionyesha nyundo yenye maandishi "Tumia wakati wa mazungumzo muhimu". Hii inaonekana kuashiria mauaji ya kikatili kwa kutumia nyundo ya mkuu wa Wagner aliyetuhumiwa kwa usaliti mnamo Novemba 2022.

Jioni hiyo hiyo, Channel One ya runinga ya serikali ilipendekeza kwamba Yevgeny Prigozhin alihusishwa na ujasusi wa Magharibi, ambao sasa " ulikuwa na aibu sana" kukubali kuhusika katika uasi wake dhahiri.

NTV, mojawapo ya vituo vitatu vya runinga maarufu zaidi nchini Urusi, ilisema kwamba alikuwa akiongozwa na pupa na uhalifu wa zamani.

"Kilichotokea kina mizizi dhahiri katika utu wake, masilahi ya biashara na maisha yake ya zamani yaliyozongwa na uhalifu," ilisema. Kuhusu utajiri unaodaiwa wa Prigozhin, "kupigania ukweli kunagharimu pesa nyingi", NTV ilisema.

Hadi miezi kadhaa baada ya kuanza kwa vita kamili vya Urusi dhidi ya Ukraine, maafisa, vyombo vya habari na vitengo vya mawasiliano ya Prigozhin vilikanusha uwepo wa kundi la Wagner.

Kwa kipindi cha muda baadaye, TV ya serikali ilisherehekea kuhusika kwa Wagner katika "operesheni maalum ya kijeshi" nchini Ukraine.

Taarifa kuhusu Wagner zilikuwa zimetoweka kwenye vyombo vya habari vya serikali wakati Prigozhin alipoanza "maandamano ya haki", akiapa kuwaadhibu makamanda wa kijeshi wa Urusi ambao aliwashutumu kwa uzembe.

Prigozhin mwenyewe, ambaye amekuwa kimya kabisa kwenye mitandao ya kijamii baada ya uasi wake dhidi ya Urusi hajatoa kauli yoyote kuhusiana na picha hizo.

Lakini kituo kimoja kilichohusishwa na Wagner kilisema kuwa haikuwa kawaida kwa mfanyabiashara tajiri kama Prigozhin kumiliki nyumba ya bei ghali: "Ni nini cha kushaza hapa, basi?" iliuliza.

Baada ya kukanusha kuwa kulikuwa na uhusiano wowote kati ya Wagner na serikali, Rais Vladimir Putin - akizungumza muda mfupi baada ya maasi ya Prigozhin kushindwa - alisema serikali ilifadhili kikamilifu shughuli za jeshi hilo la kibinafsi, ikitumia hadi dola bilioni moja kati ya Mei 2022 na Mei 2023.