Bakhmut: Mji wa Ukraine ambapo Urusi bado inasonga mbele kijeshi

Na, Jonathan Beale

BBC News, Bakhmut

Takriban miezi minane baada ya Urusi kuvamia Ukraine, vikosi vyake bado vinang’ang’ana huku Ukraine ikiwa imesonga mbele kijeshi na kurejesha maeneo ya mashariki na kusini iliyokuwa imeyateka.

Katika eneo la mashariki la Donbas, mji wa Bakhmut bado unalengwa na Urusi, hata hivyo, wanajeshi wake wanapiga hatua.

Jiji linashuhudia makombora ya kila wakati, mchana na usiku.

Hali hii imekuwa ikiendelea kwa wiki kadhaa sasa.

Wengi wa raia 70,000 wa Bakhmut tayari wametoroka mji huo.

Waliobaki wengi wao ni wazee.

Wanaishi bila maji wala umeme.

Kulikuwa na foleni ndogo kutokana na hali ya kuondoka mji hivi karibuni, huku watu waliojitolea wakiwa bado wanaendesha basi dogo ndani na nje ya jiji kwa ujasiri.

Olena, ambaye ana umri wa karibu miaka 70, alikuwa miongoni mwa wale waliokuwa wakisubiri kuondoka.

"Watu wamechoka," alisema, wakati shambulio lingine likitikisa jiji.

Kila mtu huchukua hatua tofauti, alisema - wengine hutafuta sigara, au kitu cha kutafuna, wakati wengine hukaa tu na kulia.

Maisha yalikuwa magumu sana, alisema, akilazimika kupika chakula sehemu ya nje na kuchota maji kwa kutumia ndoo.

"Namlaani aliyeanzisha vita hivi. Ninamlaani mara 100," alisema.

Alipopanda basi alishika mikono yake kwa shukrani na hatimaye kuondoka.

Huko Bakhmut, Urusi inajaribu sana kubadilisha simulizi ya vita hivi.

Ni moja wapo ya maeneo machache ambayo haijasalimu amri.

Maendeleo yake hapa kivita yamekuwa ya polepole na ya gharama kubwa, lakini vikosi vya Urusi vimekuwa vikipata mafanikio.

Huenda wakati mmoja kulikuwa na mantiki kwa mtazamo wa Urusi katika kukamata mji wa Bakhmut.

Katika majira ya joto awali kabisa ilikuwa imeteka miji ya karibu ya Severodonetsk na Lysychansk.

Bakhmut ilikusudiwa kuwa mji utakaofuata, kwa matarajio kwamba vikosi vya Urusi vingeelekea Kramatorsk na Sloviansk.

Lakini hiyo ilikuwa kabla ya Ukraine kuzindua mashambulizi yake ya kushtukiza katika mashariki na kusini.

Vikosi vya Urusi vimerudishwa nyuma zaidi kaskazini.

Miji ya Kramatorsk na Sloviansk haiko tena katika maeneo ya makombora ya Kirusi, kama ilivyokuwa mnamo Julai.

Urusi kwa kiasi kikubwa imelazimika kubadilika kutoka kuwa mshambuliaji hadi jeshi la kujihami.

Kanali Serhiy Cherevatyi, msemaji wa Kamandi ya Mashariki ya Ukraine, bado ana shaka kwamba Warusi wana idadi au vifaa vya kuchukua Bakhmut - ambayo anasema sasa ni mkusanyiko wa juhudi zake za kijeshi.

Wakati huo huo, alisema, Urusi inajaribu kujenga ulinzi mpya kaskazini zaidi karibu na miji ya Svatove na Kremenna - ambapo njia kuu za usambazaji pia sasa zinatishiwa na Ukraine.

Kanali Cherevatyi aliniambia mengi sasa inategemea ni vikosi vingapi vya ziada ambavyo Urusi inaweza kuhamasisha na ubora wa wanajeshi hao wa akiba.

"Hadi kufikia sasa tunaona kwamba ubora wao ni duni na hawana silaha za kutosha. "

Nilikutana na kanali katika uwanja ambapo vifaru vya Kirusi viliharibiwa na magari ya kivita karibu na jiji lililokombolewa hivi karibuni la Lyman.

Ni taswira ya jeshi la Urusi Ukraine inataka kuonyesha ulimwengu - bado inazuia ufikiaji kwa waandishi wa habari ambao wanataka kwenda vitani.

Kanali Cherevatyi alidai Urusi hivi majuzi imekuwa ikituma vifaru vya zamani vya T62, vilivyotengenezwa miaka ya 1960, vitani kwa sababu silaha zake nyingi za kisasa zilikuwa zimeharibiwa.

Mwezi uliopita Rais Putin alitangaza kuwa anataka usajili wa wanajeshi 300,000 kwa ajili ya vita, na Urusi sasa inasema lengo hili litafikiwa ndani ya wiki mbili.

Lakini juhudi za kukamata mji wa Bahkmut zimeongozwa na mwanakandarasi binafsi wa kijeshi, kundi la mamluki la Wagner, kundi la kijasusi la kijeshi la Uingereza linaamini.

Kundi hilo la mamluki limekuwa likipigana nchini Ukraine tangu mwaka 2014, na mwezi uliopita video iliibuka ikimuonyesha kiongozi wake akisajili wanajeshi katika gereza la Urusi.

"Ni aidha makampuni binafsi ya kijeshi na wafungwa, au watoto wenu - kuamua mwenyewe," aliwaambia Warusi.

Bado inawezekana kwamba vikosi vya Urusi vinaweza kukamata mji wa Bakhmut.

"Lakini nini basi?

"Tulipotoka Lysychansk tuliwachosha adui," Kanali Cherevatyi alisema.

Matarajio yake ni kwamba Bakhmut anaweza kufanya vivyo hivyo.

"Kuhusu kuongezeka kwa kasi ya mashambulizi ya makombora ya masafa marefu ya Urusi, anasema athari pekee itakuwa motisha zaidi kwa Ukraine: "Tuliwashinda vitani, na muhimu zaidi walichobakisha ni makombora.