Ni masuala gani yaliyo kwenye Azimio la Dar es Salaam la Marais wa Afrika kuhusu umeme?

    • Author, Alfred Lasteck
  • Muda wa kusoma: Dakika 3

Viongozi wa nchi na serikali za Afrika wameafiki Azimio la Dar es Salaam yaani 'Dar es Salaam Energy Declaration' linalolenga kuhakikisha upatikanaji wa umeme kwa watu milioni 300 barani Afrika ifikapo mwaka 2030.

Maafikiano hayo yalifikiwa katika Mkutano wa Nishati wa 'Mission 300 'ulifanyika kwa siku mbili nchini Tanzania, ukihudhuriwa na wakuu wa nchi 24 za Afrika, mawaziri wa nishati na fedha, pamoja na viongozi wa taasisi za kifedha na nishati za kimataifa, ambapo jumla ya viongozi 2,600 walishiriki.

Azimio la Dar es Salaam limepewa kipaumbele kama hatua muhimu ya kushughulikia changamoto kubwa za nishati zinazozuia maendeleo ya bara la Afrika.

Miongoni mwa mambo mengine yaliyomo kwenye azimio hili ni kila nchi kushiriki katika kugharamia upatikanaji wa umeme na kuimarisha uwezo wa utekelezaji wa miradi ya umeme kwa wakati.

Usawa wa jinsia katika upatikanaji wa nishati

Azimio linasisitiza usawa wa kijinsia katika kuongeza upatikanaji wa nishati, hasa kwa wanawake na wafanyakazi, ili kuimarisha mustakabali wa nishati endelevu.

Pia azimio linatoa msisitizo mkubwa kuhusu umuhimu wa kuunganisha nishati kati ya nchi za Afrika, kutumia vyanzo vya nishati jadidifu kama vile jua, upepo, umeme wa maji, nishati ya joto la ardhi, na mchanganyiko wa nishati ili kuwa na mifumo imara ya nishati.

Viongozi hao pia walihimiza ushiriki mkubwa wa sekta binafsi, ubunifu, na kuweka mazingira bora ya kisheria ili kuhamasisha maendeleo, kuboresha miundombinu na kufanikisha mageuzi ya nishati kote Afrika.

Waunda Tume ya kufuatilia masuala ya umeme Afrika

Kwa kuongezea, siku ya jana viongozi hao walikubaliana kuanzisha Tume ya Umoja wa Afrika itakayoratibu na kufuatilia utekelezaji wa azimio hilo, kwa lengo la kutokomeza tatizo la umeme na kuimarisha uchumi katika nchi za Afrika.

Aidha, watahakikisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia, kutumia nishati mbadala, na kupunguza madhara ya uharibifu wa mazingira.

Viongozi hao pia walikubaliana kuongeza ufanisi wa miundombinu ya uzalishaji, upitishaji, na usambazaji wa nishati kwa gharama shindani, huku wakifanya kazi pamoja katika kukuza mifumo ya ununuzi shindani na wazi.

Sekta binafsi kubeba ukuaji nishati Afrika

Wakuu hao wa nchi walikubaliana kuvutia mitaji kutoka sekta binafsi na kuhakikisha fedha zinazohitajika kwa ajili ya miradi ya mabadiliko ya nishati zinapatikana.

Azimio hili pia linatoa wito wa utekelezaji wa mipango wiliyoafikiwa ikiwa na malengo ya muda mrefu ya kupata fedha kwa ajili ya miradi ya nishati safi.

Sehemu ya azimio hilo linasema: "Lengo letu ni kufikia watu milioni 300, na tunapendekeza hatua madhubuti na ushirikiano wa kisiasa katika utekelezaji wake. Tunaomba Kamisheni ya Umoja wa Afrika kuwezesha utekelezaji wa azimio hili."