Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Spence: Muislamu wa kwanza kuitwa England baada ya zaidi ya miongo 15
- Author, Tom Mallows
- Nafasi, BBC Sport journalist
- Author, Emma Smith
- Nafasi, BBC Sport journalist
- Muda wa kusoma: Dakika 3
Djed Spence anatarajia kuwa chanzo cha hamasa kwa vizazi vijavyo ikiwa atakuwa mchezaji wa kwanza wa Kiislamu kuichezea timu ya taifa ya wanaume wa England.
Mchezaji huyo wa Tottenham anayecheza upande wa kushoto, ambaye tayari ameshacheza michezo sita kwa timu ya vijana ya England chini ya miaka 21, amejukmuishwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya wakubwa kwa mara ya kwanza kwa mechi za kufuzu kombe la Dunia dhidi ya Andorra na Serbia.
Hii ni hatua kubwa ya mageuzi kwa Spence, ambaye ni mchezaji wa zamani wa Middlesbrough, aliyetolewa kwa mkopo mara tatu na timu yake ya Spurs, kwenda Rennes, Leeds na Genoa, kabla ya kufanikiwa kuwa kwenye kikosi cha kwanza msimu uliopita.
Ingawa chama cha mpira wa miguu la England (FA), halifungamani na masuala ya dini ya mchezaji, inaelezwa kuwa Spence anakuwa mchezaji wa kwanza wa Kiislamu kuichezea timu ya taifa ya England.
"Ni baraka, ni jambo la kushangaza sana. Sijui maneno yanayotosheleza kuelezea hisia zangu," alisema mchezaji huyo wa miaka 25.
"Ninaomba sana, namshukuru Mungu kila mara. Katika nyakati ngumu zaidi za maisha yangu, katika giza kubwa zaidi, nimekuwa nikiamini kwamba Mungu yupo karibu nami kila wakati. Hii ni jambo kubwa kwangu, ni imani yangu."
England itacheza dhidi ya Andorra katika uwanja wa Villa Park Jumamosi, kabla ya kusafiri kwenda Belgrade kuikabiliana na Serbia Jumanne.
Spence amesema haajihisi kubebaa mzigo wowote zaidi kutokana na dini yake, lakini ana matumaini kuwa hadithi yake inaweza kuwa chachu ya kuhamasisha wengine.
"Sijihisi nina shinikizo lolote kwa sababu fulani. Nacheza tu mpira kwa tabasamu usoni mwangu, kuwa na furaha, na yote mengine yatajitengeneza," aliongeza.
"Kama mimi nitaweza, nawe pia unaweza. Sio tu watoto wa Kiislamu, bali mtoto yeyote wa dini yoyote. Ukiweka akili yako kwenye kitu, unaweza kufanikisha."
Jinsi Spence alivyoitwa timu ya taifa ya wakubwa ya England
Kabla ya tarehe 15 Disemba mwaka jana, Spence alikuwa amecheza dakika 64 tu katika mechi za Ligi Kuu ya England msimu wa 2024-25.
Baada ya tarehe hiyo, alicheza dakika 90 katika michezo 19 kati ya michezo 22 ya ligi ya Spurs iliyofuata.
Mabadiliko yalikuwa makubwa. Spence alikuwa hayupo kabisa katika mipango ya kocha wa Spurs, Ange Postecoglou, kiasi kwamba hakuwa hata kwenye kikosi cha awali hatua ya makundi ya Europa League.
Aliwekwa baadaye katika hatua ya mtoano, lakini alicheza dakika 180 katika ushindi wa hatua ya 16 dhidi ya AZ Alkmaar.
Baadaye alitumika kama mchezaji wa akiba wakati Spurs walipoichapa Manchester United kwenye fainali, na kupata taji lao la kwanza kubwa baada ya miaka 17, jambo ambalo pia liliwapa nafasi ya kucheza Ligi ya mabingwa Ulaya.
Kukua kwa kiwango cha Spence msimu uliopita kulikuwa kwa kiwango cha juu kiasi kwamba kulikuwa na mazungumzo kuhusu uwezekano wake kujiunga na kikosi cha kwanza cha England kilichoitwa na Thomas Tuchel mwezi Machi.
Hata hivyo, Spence hakuchaguliwa, na badala yake kijana wa Arsenal, Myles Lewis-Skelly, aliitwa kama nyota mpya na sura mpya kwenye upande wa kushoto, licha ya Spence kuwa na takwimu nzuri zaidi katika Ligi Kuu hadi wakati huo.
Lakini Spence aliendelea kushikilia nafasi yake, na baada ya kucheza kila dakika ya michezo ya Spurs msimu mpya wa Ligi Kuu hadi sasa, alifanikiwa kuitwa kujiunga na kikosi cha timu ya taifa ya wakubwa.
"Ni jambo kubwa kweli kucheza kwa England, 100%," alisema Spence.
"Kocha amenifanya nijisikie vizuri, kila mtu hapa amenifanya nijisikie vizuri. Pia nilicheza kwenye timu ya vijana chini ya miaka 21, hivyo najua kidogo kuhusu viwango vya timu ya taifa. Lakini kwenye kikosi cha wakubwa, sijawahi kufanya hivyo kabla. Watu hapa wamenifanya nijisikie kama mtu niliyekamilika."
Spence alicheza mchezo wa kwanza na timu ya vijana chini ya miaka 21 ya England chini ya kocha Lee Carsley mnamo Machi 2022 dhidi ya Albania.
Carsley alitaka kumchukua Spence katika Kombe la Ulaya la vijana chini ya miaka 21 mwaka 2023, ambapo England ilishinda kwa kuichapa Hispania katika fainali, lakini majeraha yalimfanya mlinzi huyo asicheze katika mashindano.
Kwa Carsley, kupanda hadhi kwa Spence sio jambo la kushangaza.
"Nampenda Djed. Nadhani ni mchezaji mzuri sana," Carsley aliwaambia waandishi wa BBC mwanzoni mwa mwaka huu. "Ni jambo la kusisimua, ni mchezaji mwenye nguvu, mnyenyekevu na mtulivu. Ana sifa nyingi: jinsi anavyoweza kukokota mpira, kufunga, kutengeneza nafasi, kuzuia mashambulizi. Ni mchezaji ambaye hana kikomo cha kile anaweza kukifanya kwa ufanisi."