Mwanahabari amfanya muuaji sugu akiri mauaji aliyoyaficha kwa miaka 30

Chanzo cha picha, Roberto Candia
- Author, Fernanda Paul
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Makala hii ina maelezo ambayo baadhi ya wasomaji yanaweza kuwaumiza.
"Nina zawadi kwa ajili yako, kuhusu swali lako, andika Isabel Hinojosa na mtoto wake, Eduardo Páez."
Maneno hayo yanatoka kwa Hugo Bustamante, muuaji sugu, akimwambia mwandishi wa habari wa Chile, Ivonne Toro, Agosti 4, 2023.
Toro alimhoji Bustamante gerezani, alipokuwa akiandika kitabu kuhusu kifo cha msichana wa Chile, Ámbar Cornejo, ambaye Bustamante alimnyanyasa, kumbaka, kumuua na kumkata kata.
Historia ya mauaji

Chanzo cha picha, Yvonne Toro
Mauaji ya Ámbar Cornejo yaliitikisa Chile mwezi Agosti 2020. Baada ya kupotea kwa siku 8, mabaki ya binti huyo mwenye umri wa miaka 16 yalipatikana katika nyumba ya Hugo Bustamante - iliyoko katika jiji la Villa Alemana, katika mkoa wa Valparaiso, wakati huo Bustamante alikuwa mpenzi wa mama yake Ámbar, Denise Llanos.
Binti huyo ambaye tangu alipokuwa mdogo alikumbana na mazingira magumu na ukosefu wa ulinzi kutoka kwa familia yake iliyosambaratika - alikuwa amekwenda kwenye nyumba hiyo kuchukua pesa ambayo baba yake alikuwa akimtumia kila mwezi.
Ilipofahamika kwamba Ámbar ni muhanga wa mauaji ya kutisha yaliyofanywa na Bustamante na ambayo mama yake pia alishiriki, Chile yote ilikasirika.
Bustamante ana historia ya kutisha. Mwaka 2005 alipatikana na hatia ya mauaji ya mpenzi wake wa zamani, Verónica Vásquez, na mtoto wa mpenzi huyo mwenye miaka 9, Quenito. Alimkaba mama na akampiga kwenye fuvu la kichwa mtoto, na kuificha miili yao ndani ya tangi kubwa la chuma lenye chokaa, maji na plasta.
Ingawa alihukumiwa kifungo cha miaka 27 jela kwa makosa haya, miaka 11 tu baadaye - mwaka 2016 - aliachiliwa kutoka gerezani kwa msamaha na kurudi kuishi katika nyumba ya familia yake huko Villa Alemana.
Mengi yafichuka

Chanzo cha picha, Roberto Candia
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mwanahabari Ivonne Toro alifuatilia kesi ya Ámbar Cornejo. Anaamini serikali ya jimbo haikufanya kazi yake. Na ndio sababu ya mwandishi huyo kutumia miaka minne kufuatilia kesi hiyo.
Alipitia kurasa 8,000 za nyara za mahakama, ambazo kulingana na kitabu chake "The Amber Girl," “zilimzamisha kwenye giza tupu."
Pia alifanya mahojiano zaidi ya 100, baadhi yake yalimzamisha katika mambo ya kutisha ambayo hakuyajua.
Miongoni mwa waliohojiwa ni Hugo Bustamante mwenyewe, alikutana naye mara 6 - kati ya Juni 2023 na Januari 2024 - katika gereza la Rancagua, anakotumikia kifungo chake.
Mwanzoni alikataa mahojiano hayo na kufoka. Lakini baadaye alipokubali kuhojiwa, alimtaka mwandishi huyo, amletee vifaa vya usafi wa mwili na kitabu cha saikolojia huko gerezani.
Ivonne Toro alichagua kitabu cha "The Killer Across the Table" cha John Douglas na Mark Olshaker.
Lakini Bustamante akakirudisha na kumwita Toro ni mjinga na asiye na heshima. Kwa kiasi fulani Toro alijuta na baadaye akampelekea kitabu cha saikolojia na Sudoku.
Katika mkutano wao wa tatu, Agosti 2023, Bustamante alipatwa na hisia. Kabla hajawasha kinasa sauti, alimwambia Toro, anashukuru anavyomtendea utu. Mwandishi huyo alikuwa amempa Bustamante vitafunio na karanga, katika moja ya mahojiano yao.
Katika mazungumzo yao, mwanahabari alitaka kuelewa ni nini kilimpelekea kufanya uhalifu kwa Ámbar na pia kwa Verónica Vásquez na mwanawe Quenito.
Lakini alipata mengi zaidi. Wakati wa mkutano huu wa tatu ndipo Bustamante aliamua kumpa mwandishi wa habari "zawadi."
"Nina zawadi kwa ajili yako, kuhusu swali lako, andika: Isabel Hinojosa na mtoto wake, Eduardo Páez."
Majina hayo yanamaanisha nini? Ni akina nani? Wako wapi? Je, wana uhusiano wowote na kesi ya Ámbar? Ivonne Toro alitoka gerezani akijiuliza maswali yote hayo.
"Ilinibidi kutafuta ili nijue watu hawa wapo au la. Nilianza kupekua masijala kupata majina na maeneo. Mpaka nilifanikiwa kumpata jamaa wa watu hawa niliyemuuliza kama wako salama. Na jibu lilikuwa hapana, wamepotea kwa miaka 30,” anasema.
Safari ya kuwatafuta
Ivonne Toro alimtembelea tena Bustamante gerezani.
“Nikamwambia: niambie hawa watu wako wapi. Lakini akakataa na akajuta kunipa majina hayo,” anasema mwanahabari huyo.
Kilichofuata ni miezi ya kutafuta bila majibu. Familia ya watu waliopotea ilikuwa na kumbukumbu kidogo ya kile kilichotokea miaka 30 iliyopita. Pia ilikuwa ni kesi ambayo ilisahaulika katika mfumo wa mahakama wa Chile.
Januari mwaka huu, mwandishi wa habari huyo hatimaye alipata chanzo cha kifo cha Isabel Hinojosa na mtoto wake, Eduardo Páez.
Hugo Bustamante, alikiri watu hao wawili walikuwa katika nyumba yake mwaka 1996 - iliyoko katika Mtaa wa Covadonga, huko Villa Alemana - kabla ya kutoweka.
Páez na Bustamante walikutana katika miaka ya 90 gerezani na waliendelea kuonana hadi yeye na mama yake walipotoweka.
Kulingana na Toro katika kitabu chake, binti mwingine wa Isabel Hinojosa alisema Bustamante alikuwa mtu wa mwisho kuwaona wakiwa hai baada ya kuwapeleka nyumbani kwake.
“Nilianza kuchambua tabia ya Bustamante. Alimuua Ámbar nyumbani kwake na kuuacha mwili hapo. Aliichukua miili ya Verónica na Quenito pamoja naye alipohama nyumba. Nilihitimisha kuwa Bustamante hawezi kuwa mbali na watu anaowauwa, ilikuwa ni sehemu ya tabia yake, namna yake ya kutenda na kuua,” anasema Toro.
"Unawaweka watu unaowaua karibu nawe," mwandishi huyo alimwambia Hugo Bustamante alipomtembelea gerezani kwa mara ya mwisho, Januari mwaka huu.
“Nilimwambia: Uliwaua na kuwaweka kwako.' "Lakini alikwepa kutoa jibu, yalikuwa mazungumzo makali sana."
Juni mwaka huu, Bustamante alikiri kwa afisa wa jeshi la polisi kuhusu mazungumzo yake na mwandishi wa habari na ushiriki wake katika mauaji ya Isabel Hinojosa na Eduardo Páez mwaka 1996.
Pia alitoa taarifa juu ya miili hiyo ilipo. Maafisa wa uchunguzi wa Chile walifanya kazi yao na kupata miili miwili kwenye eneo la tukio.
Septemba 3, ofisi ya mwendesha mashtaka ilithibitisha, mabaki hayo ni ya Hinojosa na Páez. Hugo Bustamante, muuaji wa Ámbar, mpenzi wake wa zamani Verónica Vásquez na mwanawe Quenito, aliongeza idadi nyingine ya ya watu wawili aliowauwa.

Chanzo cha picha, Yvonne Toro
Katika uchunguzi wake, Toro alimhoji mama yake Ámbar, Denise Llanos, kama Bustamante, naye anatumikia kifungo kwa kuhusika kwake katika mauaji ya binti yake.
Lakini kazi ya Toro imemletea matokeo mabaya. "Siwezi kulala. Natumia chai ya kutafuta usingizi, kitu ambacho sikuwahi kukihitaji hapo awali.” Na anakiri kwamba anaendelea kuteseka kutokana na jinamizi la matukio hayo.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












