Jinsi Arsenal walivyoshinda usajili wa Eze na eneo atakalofaa kucheza

Chanzo cha picha, Getty Images
Usajili unaotarajiwa wa Eberechi Eze umebadilisha kabisa hisia za dirisha la uhamisho miongoni mwa mashabiki wa Arsenal.
The Gunners wamekuwa na shughuli nyingi katika dirisha hili, wakisajili wachezaji sita kwa takriban pauni milioni 190 kabla ya msimu wa Ligi Kuu kuanza.
Waliowasili ni pamoja na mshambuliaji wa £64m Viktor Gyokeres na kiungo Martin Zubimendi kwa takriban £60m, lakini ni dili la mchezaji wa kimataifa wa Uingereza Eze ambalo linawafanya mashabiki kuhisi kama wameshinda dirisha.
Sababu kubwa ni kuwavuruga wapinzani wao Tottenham Hotspur, ambao walikuwa wamekubaliana na Crystal Palace na mchezaji huyo saa chache kabla ya The Gunners kuwasilisha ofa yao ya pili.
Jinsi Arsenal ilishinda mbio za kumsajili Eze
Mapema Jumatano, ilionekana kana kwamba Eze mwenye umri wa miaka 27 angeelekea upande wa kaskazini mwa London.
Lakini mpango huo haukukamilika.
Na sababu ilikuwa mechi ya Palace ya Europa Conference ya mchujo na Fredrikstad siku ya Alhamisi.
The Eagles walitaka kumtumia Eze kwa mchezo wanaouona kuwa muhimu kwa msimu wao, na mchezo ambao hawakutaka kuukabili bila kuwa na mbadala.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Meneja wa Palace Oliver Glasner alikuwa na nguvu katika mkutano wake na waandishi wa habari kabla ya mechi aliposema kwamba Eze na Marc Guehi, ambaye pia amehusishwa na kuhamia klabu nyengine , "wamejitolea" kwa timu.
Katika uwanja wa Emirates Stadium, sehemu ndogo ilikuwa ikitayarishwa.
Arsenal walikuwa wakifanya mazoezi ya wazi katika uwanja wao ambayo hayakuwa na Kai Havertz. Baadaye ilibainika kuwa mchezaji huyo wa kimataifa wa Ujerumani alikuwa akifanyiwa tathmini ya jeraha la goti.
Licha ya ukubwa wa jeraha hilo kutofahamika, Arsenal walijua vya kutosha kufanya uhamisho.
Saa chache baadaye Jumatano alasiri, Arsenal ilitoa ofa kwa Eze, na kuamua kuchukua hatua kulingana na nia yao ya muda mrefu kwa mchezaji huyo.
Eze akiwa kijana na shabiki wa Arsenal ambaye alicheza katika akademi yao, ulikuwa uamuzi rahisi kwa mchezaji huyo.
Kufikia 19:30 BST, habari za uhamisho huo wa kushtukiza ziliibuka kwenye vyombo vya habari, huku vyanzo vikieleza kuwa hakuna kitu ambacho Spurs wangeweza kufanya ili uhamisho huo ufanyike kutokana na uhusiano huo wa kihisia.
Na kutokana na hatua yake ya kuikataa Tottenham - Eze hakika atakuwa kipenzi cha mashabiki wa Arsenal kwa haraka zaidi.
Lakini kwa nini walichukua uamuzi huo kwa kuchelewa?
Arsenal walikuwa wamemwona Eze kama nambari 10 zaidi na, huku Ethan Nwaneri akiweka mustakabali wake kwa klabu kwa mkataba wa muda mrefu, ilibidi wafikirie kwa makini jinsi mchezaji huyo wa kimataifa wa Uingereza atakavyofaa.
Lakini inaonekana jeraha la Havertz lilimaanisha waliamua kuwa anahitajika kwenye kikosi chao.
Eze hakucheza katika mechi ya mchujo ya Europa Conference kwa Palace siku ya Alhamisi, huku Glasner akisema mchezaji huyo alimpigia simu kumwambia alikuwa mgonjwa.
Ana uhakika wa kusaini Gunners siku chache zijazo, akikamilisha mkataba wa kujiunga tena na klabu ambayo ilimuachia akiwa na umri wa miaka 13.
Eze atafaa wapi Arsenal?

Chanzo cha picha, Getty Images
Swali kubwa kwa kocha wa Arsenal Mikel Arteta ni hili - Eze atacheza katika safu gani katika timu ya Arsenal?
Mshambuliaji huyo ni mmoja wa wachezaji wachache wa mwisho unaoweza kuwaelezea kuwa bora sana.
Hilo ndilo linalofanya usajili wake kuwa muhimu sana kwa Arsenal .
The Gunners wamepata matatizo ya kuvunja safu za ulinzi wa timu pinzani awali na sasa wanatumia mtindo mpya msimu huu ambao utawafanya kupeleka mpira mbele kwa kasi
Eze ni tofauti sana na washambuliaji wengine wote walio na Arsenal na atatoa chaguo tofauti.
Bila shaka, nahodha Martin Odegaard atakuwa mchezaji mgumu kuondoka katika nambari 10.
Lakini ununuzi wa Eze unaongeza chaguzi nyingi ambazo timu zinazotaka kushinda taji zinaweza kutamani.
Nafasi ya winga wa kushoto wa Arsenal pengine ndiyo inayopiganiwa zaidi.
Gabriel Martinelli hakuwa na msimu mzuri uliopita na jeraha alilopata lilizidisha hali hiyo.
Mwandishi wa BBC wa mbinu za soka Umir Irfan alisema: "Eze anaweza kucheza mara kwa mara kwenye wingi ya kushoto, kutokana na mchezo usioridhisha wa sasa wa Martinelli.
"Eze anaweza kustawi katika maeneo ya kati zaidi ikiwa beki wa kushoto wa Arsenal atapanda na mpira kuelekea mbele.
"Uwezo wa Eze kucheza vizuri na wachezaji wenzake wa karibu katika maeneo yenye msongamano unamfanya kuwa chaguo bora ikiwa itatumiwa kwa njia hii.
"Ubora wake wa juu wa kutamba na mpira akielekea mbele unamfanya Eze kuwa chaguo bora katika michezo ya mbele ambapo atakuwa akimpatia mipira Gyokeres .
"Kwa mechi ambayo mashambulizi yanahitajika, Odegaard na Eze wanaweza kucheza pamoja kama viungo washambuliaji.
"Kando ya mpira, anaingia kama kiungo wa kushoto huku Arsenal wakicheza mfumo wa 4-4-2. Hii inakuwa rahisi zaidi anapoanzia wingi ya kushoto."















