Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Aliyekuwa na matatizo ya akili akizunguka usiku kucha mchana kutwa, apata tena matumaini ya maisha
Na Asha Juma, BBC Swahili
Ushawahi kusikia msemo hujafa hujaumbika kwa maana kuwa chochote kinaweza kutokea maishani. Kijana wa makamo Hirima Mbilu kutoka Mazeras eneo la Mombasa, alizaliwa kama wengine akiwa hana shida yoyote, akafikia hatua ya kufanya kazi na kusaidia família yake lakini ghafla maisha yalianza kumbadilikia.
Kufumba na kufumbua akawa anatambulika kama mgonjwa mwenye matatizo ya akili.
Leo ikiwa ni siku ya watu wenye matatizo ya akili duniani, mwanahabari wa BBC Asha Juma amepata fursa ya kutembelea kituo cha Mombasa Women Empowerment Network kuangalia safari ya maisha ya wagonjwa wa aina hiyo huku Bwana Hirima akielezea aliyokumbana nayo maishani.
Hali yake ilikuwaje?
Hirima alikuwa ameanza kuishi maisha yake ya kujitegemea kama mtu mwingine yeyote, akiwa miongoni mwa watoto wanaosaidia familia yake.
Lakini kukatokea tukio ambalo si la kawaida, família inakumbuka kuna wakati ilipigiwa simu na kujulishwa kwamba kijana wao ameanguka .
Na walipofika eneo la tukio, walimkuta mpendwa wao akiwa tayari amepoteza fahamu wasijue kuwa, kinachofuata ni kukumbana na matatizo ya akili.
Miongoni mwa sababu ambazo Hirima amezitaja kuchangia kujikuta unakabiliana na ugonjwa wa akili ni pamoja na kufeli maishani.
‘’Kila mradi unaojaribu kufanya haufanikiwi, kazi unakosa, ndio kunafanya mtu avunjike moyo katika maisha yake,’’ Hirima amesema.
Hirima alikuwa mtu anayetembea mchana na usiku, jua na mvua yote yalikuwa yake, asiwe na cha kutia mdomoni zaidi ya kuchakura kwenye jaa au majalala. Na ingekuwa vigumu hata kwa familia kuishi naye karibu.
‘’Ilikuwa vita vyenyewe vya kupiga kelele, kutukana, alikuwa akizunguma peke yake na kurusha mawe,’’ mama yake amesema.
Kilichomfanya Hirima kukata tamaa ya maisha ni ‘’kuona kazi ni ngumu sana, kila ninalojaribu kwa kampuni nyingine sikubaliki, nikafikiria mambo mengi hadi nikasema sasa liwalo na liwe, nitaishi tu.’’
Safari hii hata kwa familia haikuwa rahisi. Walijaribu kila mbinu kumrejesha nyumbani lakini juhudi zao zilionekana kuambulia patu. Na kadiri siku zilivyosonga, ndivyo hali ilizidi kuwa zaidi. Alifikia kiwango cha kutoweka kabisa na kuanza kuishi msituni.
Siku iliyobadilisha maisha yake
Wakati akiwa anaendelea kupambana na ugonjwa wa matatizo ya akili, siku moja akakutana na wahudumu wa Shirika la Women Empowerment Network, na huo ukawa mwanzo mpya maishani mwake.
Hirima anasema waliomuokoa akiwa ameketi sehemu ambayo ni chafu ‘’walinipata kwenye jaa njiani, nilikuwa nafikiria mambo mengi kwasababu tayari nimejitenga’’.
Kinachotokea ni kwamba shirika hilo lenye kuwahudumia watu wenye matatizo ya akili huwa na siku zao za kwenda kutafuta wagonjwa kwenye majaa mbalimbali na sehemu wanazotembea sana kama vile barabarani.
Wanapomuokoa mgonjwa, humchukua moja kwa moja hadi kwenye kituo chao na kuanza utaratibu wa mchakato wa kubadilisha tabia na matibabu, kumfanyia usafi kwa sababu mara nyingi huwa hawajaoga kwa muda mrefu na kumpa chakula, akipumzishwa safari ya kutembea mwendo mrafu kutafuta donge la kutia mdomoni.
Lakini chimbuko la tatizo hasa huwa nini, Amina Abdhalla, mwanzilishi wa shirika la Mombasa Women Empowerment Network anasema, ‘’ Mara nyingi huwa wanatengwa kwasababu ya vile vituko wanavyofanya, hakuna anayetaka kuhusishwa naye’’.
Pia anaongeza kuwa bado jamii haijaku bali kuwa ugonjwa wa matatizo ya akili ni kama tu ugonjwa wa malaria, saratani na kadhalika kwa sababu hujumuishwa na dhana mbalimbali potofu.
‘’Kwanza watu wanawaita majina ambayo sio ya kibinadamu. Vile vile jicho linaweza kuuma, tumbo, hata akili inaweza kuuma kwa sababu ni kiungo kama viungo vingine lakini jamii bado haijaamini kuwa kiungo hicho cha mwili kinastahili kuugua pia,’’ Amina Abdhalla anasema.
Changamoto nyingine kubwa anasema kuna wakati amemtibu mgonjwa hadi amerudi kuwa kawaida lakini familia inapojulishwa watakuja na sababu zingine.
‘’ Huyo ana laana, alimpiga babangu kwahiyo hawezi kurudi sawa, limuibia mtu akasomewa, alirongwa na kadhalika, bado familia zinakataa kuwa kuna ugonjwa wa matatizo ya akili,’’ anasema Bi. Amina.
Safari ya uponyaji
Hirima alipopokelewa na Shirika la Mombasa Women Empowerment Network, mchakato wake wa kupata tiba ikiwemo ushauri nasaha ulianza. Baada ya miezi kama minane, Hirima alikuwa amerejea katika hali ya kawaida, na kuruhusiwa kurejea nyumbani. Sasa ameanza kuona mwangaza katika sehemu iliyokuwa na kiza kinene.
‘’Maisha yangu yamebadilika kwa sababu nina msimamo mpya wa maisha, nataka nianze kama kufuga kuku, mwanzo mpya, nimeachana na yale yaliyopita,’’ Hirima anasema.
Lakini nini kinachangia uponyaji wa haraka wanapofikishwa kwenye kituo cha kutoa huduma stahiki?
‘’Tunawapa upendo wa kutosha, wa kujisikia kumbe hapa ni nyumbani. Na baada ya hapo tunampa mapenzi ya mzazi. Akiwa na shida yoyote anasema, anabadilishwa nguo anazungumza chochote anachotaka’’.
Bila shaka safari yake hii ya kubadilisha maisha ya watu wenye matatizo ya akili sio kanda la usufi. Nini kinampa msukuko wa kusonga mbele kila kukicha?
‘’Ile kumuona mgonjwa, amepona, anafanyakazi, au hata ameniletea mjukuu, kitu ambacho hata sikufikiria kwa mtu kama yule. Hiyo inanipa nguvu kila siku.’’
Pia hufanya matangazo ya moja kwa moja wakati anamuokoa mgonjwa kwenye mtandao mmoja wa kifamii, na wakati huo hupokea maombi kutoka sehemu nyingi duniani zenye kuhitaji huduma yake.
Pengine hili linatokana na kuwa ni kituo cha pekee hadi kufikia sasa chenye kuwahudumia wagonjwa wa matatizo ya akili wakati wanaishi nao katika eneo la Afrika Kusini.
Tiba ya wenye matatizo ya akili
Mwanasaikolojia Yusuf Saad, anasema mgonjwa akipatikana barabarani, kwanza anafanyiwa uchunguzi kutathmini matatizo ambayo anakumbana nayo kila siku, anaishi vipi na mbinu ambayo inaweza kutumika katika matibabu yake.
‘’Kwanza angalia eneo analoishi kama linamuwezesha kupata utulivu wa akili. Kisha tunafuatilia kujua ugonjwa alionao, matibabu yake na saikolojia yake.
Haikuwa rahisi kwa Hirima Mbilu, kurejea katika hali yake ya kawaida lakini hatua kwa hatua afya yake ikaimarika. Kwa upendo aliopata, amekuwa tena na fursa ya kujumuika na familia yake, akifidia maisha aliyokosa siku za nyuma.