Tende: Mashambulizi ya Houthi yanavyotatiza upatikanaji kabla ya Ramadhan 2024

Peter Mwangangi
BBC Swahili
Awadh Omar ni mfanyabiashara katika soko la Marikiti mjini Mombasa Pwani ya Kenya ambapo anauza tende ambazo ameagizia kutoka Saudi Arabia, pamoja na asali kutoka Yemen na Ujerumani.
Amekuwa akijiandaa kwa kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhan ambapo biashara yake hufanya mauzo mengi zaidi. Lakini kuvurugika kwa usafiri wa meli katika bahari ya shamu kumempa wasiwasi.
Kwa hivyo aliamua kuagizia mzigo wake mapema ili kuwa na uhakika wa bidhaa kumfikia kwa wakati.
Lakini hatua hii imemfanya kukosa kufaidika na ruzuku iliyotolewa na serikali ambapo tende zinazoingizwa nchini Kenya kati ya tarehe 1 Machi na tarehe 20 Machi hazilipiwi kodi.
Usafirishaji wa bidhaa zinazoelekea eneo la Afrika Mashariki kupitia baharini umetatizika katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, kutokana na mashambulizi ya makundi ya Houthi kwa meli za mizigo zinazopitia katika Bahari ya Shamu.
Hali hii imeanza kuathiri gharama ya maisha katika eneo hili.
Meli zinalazimika kutumia njia mbadala ya kuzungukia Afrika Kusini, na hii inaongezea gharama za usafirishaji ambazo hatimaye zitalipiwa na wanunuzi wa bidhaa hizo.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Nchini Saudi Arabia “wanakuza tende za ubora wa hali ya juu ambazo zinapendwa na watu katika eneo hili. Mwaka huu, tunaona ongezeko la bei kwasababu tunalipishwa zaidi kwenye usafiri wa meli, na pia kutokana na kuongezeka kwa thamani ya dola,” anasema Awadh.
Shilingi ya Kenya imekuwa ikipoteza thamani yake ikilinganishwa na dola ya Marekani, na mwanzoni mwa Machi mwaka huu $1 ilikuwa na thamani ya Ksh 144, ikilinganishwa na Machi mwaka uliopita ambapo $1 ilikuwa Ksh 127.
Kuna hofu kuwa huenda watu wengi wakakosa kufikia bei za tende mwaka huu.
“Katoni moja ya tende sasa inauzwa kwa Ksh 2,700 ($17), ikilinganishwa na mwaka jana ambapo tulikuwa tunanunua kwa Ksh 1500 ($10). Unajua hatuwezi kununua ghali halafu tuuze rahisi,” anasema Fuad Omar, mfanyabiashara wa reja reja mjini Mombasa.
Tende ni aina ya chakula muhimu kwa jamii ya Waislamu duniani kote. Tunda hili huliwa mwaka mzima, lakini pia ni muhimu wakati wa Ramadhan kwasababu linampa nguvu mtu anayefunga. Aidha tende huliwa kama sehemu ya ibada (Sunna) wakati wa kufunga na kufungua.
Changamoto za usafirishaji wa bidhaa
Usafiri kupitia baharini unapendelewa na watu wengi wanaogiza au kutuma mizigo kwa wingi nje ya nchi, ikilinganishwa na usafiri wa ndege. Hii ni kwasababu ni nafuu kusafirisha bidhaa kama nafaka, tende, mbolea, mafuta ya petroli na bidhaa zingine kwa meli.
Lakini ukosefu wa usalama katika bahari ya shamu unamaanisha kuwa wafanyabiashara wamekabiliwa na gharama zaidi pamoja na kuchelewa kwa mizigo yao. Gharama hii ya ziada hatimaye italipiwa na wanunuzi.
Na iwapo hali hii itaendelea kwa muda mrefu itaathiri pakubwa uchumi wa nchi za eneo hili.
Ken Gichinga, mchambuzi wa uchumi aliye jijini Nairobi anatoa mfano wa ngano inayoagizwa kutoka Urusi ama Ukraine na kusafirishwa hadi Afrika. “Kama meli zinazobeba nafaka haziwezi kupitia bahari ya shamu, kiwango cha ngano katika masoko ya Afrika kitapungua," anasema.
"Wakati upatikanaji wa bidhaa sokoni ni finyu lakini hitaji lake ni kubwa, bei ya bidhaa hiyo itapanda. Na iwapo hali hii itajirudia kwa bidhaa zingine kama mafuta, magari, na kadhalika, itamaanisha kutakuwa na mfumuko wa bei kwa jumla.”
Iwapo hili litatokea, Bw Gichinga anasema benki kuu zitalazimika kuongeza viwango vya riba, hali itakayoongeza gharama ya mikopo, na hali kadhalika kupunguza shughuli za biashara pamoja na ukuaji wa uchumi.
Na hali hii haiathiri tu chakula, lakini pia bidhaa zingine ambazo kwa kawaida huonekana kama za kifahari kama vile magari.

Leonard Njiru, ambaye ni mfanyabiashara wa kugiza magari, aliambia BBC kwamba kuchelewa kufika kwa meli zinazotoka bara Uropa, Dubai, Singapore na Japan katika bandari ya Mombasa kunamaanisha kwamba wateja watapoteza pesa zao.
Bw Njiru anaeleza kuwa magari yaliyotumika (used cars) na ambayo yana zaidi ya miaka 8 tangu kutengenezwa hayaruhusiwi kuingia wala kusajiliwa Kenya.
“Kwa hivyo ilikuwa muhimu kwa waagizaji kuhakikisha kwamba magari yenye zaidi ya miaka 8 yamefika Kenya kabla ya tarehe 31 Disemba 2023,” anasema.
Muungano wa mawakala wa kupokea na kusafirisha bidhaa nchini Kenya (KIFWA) umeiambia BBC Swahili kuwa unazungumza na serikali ili kukubaliwa kusajili magari yaliyochelewa kutokana na changamoto hii.
Iwapo hawatapata ruhusa ya serikali, magari huenda yakavunjwa au kurejeshwa kwenye mataifa yaliyotoka na huenda hii ikawa ni kwa gharama ya mteja au mtu aliyeagiza.
“Na hata wakati tukisubiri kauli ya serikali, gharama zinaongezeka. Kama vile ada na kodi za kuhifadhi mizigo bandarini. Hii itakuwa na athari kwasababu iwapo mtu aliagiza magari ili auze, gharama ya ziada itaongezwa kwenye bei ya kuuza gari,’ anasema Njiru.
Idadi ya meli zinazoingia nchini Kenya imepungua kati ya Disemba 2023 na Februari 2024
BBC Swahili ilizungumza na Mamlaka ya Bandari Kenya (KPA) kuhusu ripoti kuwa , lakini KPA haijatoa kauli yoyote kuhusu hili hadi kufikia wakati wa kuchapisha taarifa hii.
Katika kipindi hicho, mawakala wanasema idadi ya makontena wanayoshughulikia imepungua.
“Nilikuwa nashughulikia makontena 30 kwa mwezi kwa niaba ya mteja mmoja, lakini sasa yamepungua. Baadhi ya meli zingefanya safari kila wiki kuelekea eneo hili, lakini sasa zinafanya kama moja tu kwa mwezi,” anasema Salim Mbarak, mmoja wa mawakala mjini Mombasa, akiongeza kuwa biashara haijakuwa nzuri.
“Hali hii imeathiri idadi ya bidhaa ambazo ningepokea katika bandari, na hali kadhalika mapato yangu kama ada za wakala,” anasema.
Meli zinazoelekea Afrika Mashariki kutoka maeneo mengine duniani hasa bara Uropa na Mashariki ya kati hutegemea sana njia ya Bahari ya Shamu.
Lakini kutokana na ukosefu wa usalama katika eneo hilo, sasa zinalazimika kuzunguka na kupitia Afrika Kusini, ambayo inaongeza maili 5,000 (8,000km) zaidi katika safari.
Kutumia njia hii ndefu kunamaanisha gharama zaidi za usafiri ambazo zinajumuisha bei za mafuta, kupanda kwa bima ya usafiri, pamoja na mishahara kwa wafanyakazi. Aidha kuchelewa kwa bidhaa kunamaanisha kuwa maduka yanakosa bidhaa za kuuza.
Changamoto hizo hazitakuwa tu kwa Kenya na Tanzania pekee, mbali pia kwa Jamhuri ya Kidemokaria ya Kongo, Uganda, Sudan Kusini, Rwanda na Burundi, mataifa ambayo pia hutegemea kwa kiasi kikubwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje.
Haya yanajiri wakati wanunuzi wengi wanakabiliwa na kuongezeka kwa gharama ya maisha miongoni mwa changamoto zingine za kiuchumi.
Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) hivi karibuni ilionya kwamba kuongezwa kwa bei za mafuta na bidhaa kutokana na kushuka kwa thamani ya sarafu kunaweza kuchangia katika mizozo ya ndani kwa ndani ya mataifa husika mwaka 2024.
Unakumbuka meli ya Ever Given?
Hata hivyo, Juma Tella, Afisa Mkuu Mtendaji wa Muungano wa Mawakala wa meli nchini Kenya (KSAA) anasema kwamba hii sio mara ya kwanza kushuhudia changamoto katika njia hiyo ya bahari ya shamu.
Anatoa mfano wa mwaka 2021 ambapo meli kubwa kwa jina Ever Given ilikwama katika mlango wa mrefeji wa Suez na kuzuia meli zingine kupita.
“Kulikuwa na mlolongo mkubwa wa meli katika eneo hilo. Wakati huo, hali haikuwa mbaya kama hii ya sasa, kwasababu wakati huo changamoto ilikuwa kuiondoa meli hiyo hapo. Lakini sasa haijulikani hali itakuwa hivi hadi lini,” anasema Bw Tella.
Kwa sasa, wafanyabiashara kama Awadh wanatumai kuwa usalama katika bahari ya shamu utaimarika ili kuhakikisha kuwa biashara zinaendelea bila hitilafu.
"Ramadhan haiwezi kuwa bila tende," anasema. "Tumefundishwa katika dini yetu kuwa wakati tunafungua, tunapendekezwa tule tende, kama si moja hata tatu. Kwa hivyo ni muhimu mzigo utufikie."














