Imran Khan ni nani na Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Pakistani anatuhumiwa kwa kosa gani?

    • Author, Ahmen Khawaja and Asad Ali Chaudhry
    • Nafasi, BBC World Service

Imran Khan ni nani?

Yeye ni nyota wa zamani wa kimataifa wa kriketi aliyegeuka kuwa mwanasiasa ambaye aliiongoza Pakistan kupata ushindi katika Kombe la Dunia la 1992.

Mzaliwa huyo wa Lahore baadaye alistaafu kucheza kriketi na akaendelea kuchangisha mamilioni ya dola kufadhili hospitali ya saratani katika kumbukumbu ya mama yake.

Kuingia huko kwa uhisani kulizaa taaluma ya siasa ambapo aliwka kando sura yake ya ujana.

Bw Khan alihudumu kama waziri mkuu wa Pakistan kuanzia Julai 2018 hadi Aprili 2022, kama mkuu wa chama cha Pakistan Tehreek-e-Insaf (PTI).

Ni Kesi ipi ya ufisadi dhidi yake?

Imran Khan alikamatwa tarehe 9 Mei 2023 baada ya shirika la kupambana na ufisadi la Pakistan, Ofisi ya Kitaifa ya Uwajibikaji, kumshtaki kwa ufisadi.

Maafisa wa serikali wanadai kuwa Bw Khan na mkewe walipokea ardhi yenye thamani ya mamilioni ya dola kama hongo kutoka kwa tajiri anayemiliki majumba kupitia shirika la uhisani.

Inajulikana kama kesi ya Al-Qadir Trust. Bw Khan na wasaidizi wake wamekana kufanya makosa yoyote.

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 70 anasema mashtaka hayo yanachochewa kisiasa. Anashutumu vyama vya siasa kwa kuunganisha nguvu na jeshi lenye nguvu la nchi hiyo ili kumuondoa mamlakani.

Wakfu wa Al-Qadir ni nini?

Wakfu wa Al-Qadir ni shirika lisilo la kiserikali la ustawi wa jamii.

Waziri mkuu wa zamani na mke wake wa tatu, Bushra Wattoo, ambaye pia anaitwa Bushra Bibi, walikaa kwenye bodi yake ya wadhamini.

Bw Khan aliahidi kuanzisha Chuo Kikuu cha Al-Qadir huko Punjab, jimbo lenye watu wengi zaidi nchini Pakistan.

Makao rasmi ya chuo kikuu ni shamba la ekari 60 katika wilaya ya Jhelum ya Punjab, lakini machache sana yaliyofanywa katika ardhi hiyo.

Uingereza ina uhusiano gani na kesi hiyo?

Mnamo tarehe 3 Desemba 2019, Shirika la Kitaifa la Uhalifu la Uingereza (NCA) lilitangaza suluhu yenye thamani ya pauni milioni 190 na Malik Riaz Hussain, mmoja wa wafanyabiashara tajiri na hodari zaidi wa Pakistan.

Ilisema pesa zilizofungiwa katika akaunti yake ya Uingereza "zilishukiwa kuwa zimetokana na hongo na ufisadi katika taifa la ng'ambo". Taarifa hiyo ilisema pesa hizo zitarejeshwa kwa jimbo la Pakistani.

Bwana Hussain alitoa majibu kupitia ujumbe wa Twitter siku hiyo hiyo.

"Niliuza mali yetu halali na niliyotangaza nchini Uingereza ili kulipa £190M kwa Mahakama ya Juu Pakistan dhidi ya Bahria Town Karachi," aliandika kwenye Twitter.

"Taarifa ya NCA kwa vyombo vya habari inasema suluhu hiyo ni suala la kiraia na haiwakilishi kupatikana na hatia.

Je, rushwa hiyo inadaiwa kutolewa vipi?

Serikali ya sasa inadai kuwa badala ya kuweka £190m ($240m) kwenye hazina ya Pakistan, serikali ya Imran Khan iliitumia kulipa faini iliyotozwa na mahakama ya Pakistani dhidi ya Bw Hussain kwa kunyakua ardhi ya serikali kinyume cha sheria kwa thamani ya chini ya soko nchini Pakistani katika mji wa Karachi.

Waziri wa mambo ya ndani anadai kuwa Bw Hussain alitoa ardhi ya Jhelum kwa Al-Qadir Trust ili kufanyiwa mapendeleo hayo.

Nini kinafuata kwa Pakistan?

Tangu kuondolewa madarakani kama waziri mkuu, Bw Khan amekuwa akifanya kampeni za uchaguzi wa mapema. Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.

Wasaidizi wa Bw Khan wanasema kuna zaidi ya kesi 100 za kisheria dhidi yake.

Licha ya machafuko yanayoendelea, Imran Khan bado ni maarufu sana nchini Pakistan, nchi yenye watu milioni 230.

Wengi wanasema matatizo yake ya kisheria yatamfanya kuwa maarufu zaidi miongoni mwa wafuasi wake.