Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ni kidonda ambacho hakitapona katika nafsi yangu-Baba yake Clemence
- Author, Alfred Lasteck
- Nafasi, BBC, Dar es Salaam
Mamia ya watanzania wakiwemo ndugu na jamaa wamejitokeza kwenye maziko ya Marehemu Clemence Mtenga, mtanzania aliyekuwa akiishi nchini Israel, alimezikwa leo Jumanne, nyumbani kwao mkoani Kilimanjaro, Kaskazini mwa Tanzania.
Mwili huo umepumzishwa masaa kadhaa baada ya kuwasili nchini Tanzania ukitokea nchini Israeli.
Mamlaka zilidhibitisha kifo chake wiki moja iliyopita na kueleza kuwa kilitokana na mapiganyo yaliyokuwa yakiendelea kati ya Majeshi ya Israeli na Kikundi cha Kipalestina cha Hamas.
Vilio vyatawala
Vilio, uchungu na huzuni vilitawala nyumbani kwa marehemu Clemence Mtenga huku wengi wakisema kuwa Clemence aliyekuwa na miaka 22 sio tu alitegemewa kuisaidia familia yake bali alikuwa mtu wa kujitolea kwa jamii.
Careen Mtenga, mdogo wa marehemu alisema, “Clemence alikuwa Zaidi ya kaka kwangu, alikuwa mwalimu wangu. Alinisaidia na kuniwezesha mimi kufika elimu ya juu ya sekondari. Kiukweli aligusa Maisha yangu na vjana wengine hapa mtaani kwetu Kirwa- Rombo.
Aacha maumivu makali kwa familia
Baba mzazi wa Clemence, Felix Mtenga anasema kifo cha kijana wake kilimpa masikitiko makubwa mno, na inaacha maumivu kwa familia yake.
Anasema, “Ni kidonda kisichopona kwenye roho yangu, alikuwa ndio tazamia langu na tegemeo langu. Nilijitahidi kwa hali na mali kuhakikisha kijana wangu anasonga mbele. Sina pa kuangalia na sijui nitafanya nini.”
Elimu na stadi
Juma moja lililopita marehemu Clemence Mtenga, alitajwa kuwa miongoni mwa wahitimu katika mahafali ya 42 ya Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, SUA cha nchini Tanzania akiwa na Shahada ya Sayansi ya Kilimo cha Bustani yaani Bachelor of Science in Horticulture.
Familia inasema, Clemence alipenda sana kilimo na hakujali pale alipoulizwa kwanini kilimo.
Baba mzazi wa Clemnce anasema, “Hata tulipo (mbele ya nyumba yao) ilikuwa ni sehemu ya kufanyia shughuli za bustani yake, alikuwa akija nyumbani anahakikisha kuna mboga tena alipenda kuotesha spinach,mchicha na wakati wote tulikuwa tuna chakula.
Kuhusu mahafali yake ya kuhitimu shahada ya Kilimo, Mtenga anasema alipewa tarifa hiyo lakini familia tayari iliondokewa na Clemence. “Niliambiwa aligraduate, sikuelewa lakini pia sikutaka kuisikia kwasababu ya msiba isipokuwa niliambiwa alifanya vizuri kwenye masomo yake.
Mwenye msimamo, mshauri
Mtenga anasema kuna wakati alikuwa hamuelewi mwanae.”Nilikuwa simuelewi, sikuelewa analenga nini kwenye masomo ya kilimo. Nilimweleza kuwa huku kwetu wengi ni makenika na mafundi, yeye alienda kwenye kilimo. Alikuwa ananiambia baba niachee najua ninachokifuata, sikujua nia na malengo yake mbele yalikuwa nini.
Mtenga anasema inaniwia ngumu kusema, kwasababu alikuwa kijana mwenye bidi. ya tofauti. “Nikifikiria napata machungu makali sana kwasababu hata mshauri, ulikuwa ukifanya kitu anakuuliza unafanya kitu gani, kile ana kuja kukuambia unakuta kina faida. Kwakweli nimeondokewa na mtu niliyemtegemea, sina namna tena.”
Vijana wenzake wamlilia
Mmoja wa wanafunzi wenzake waliohudhuria sherehe za kuhitimu, Cleopatra Mluge, aliambia BBC kwamba Clemence alikuwa kama kiongozi kwa sababu alikuwa mnyenyekevu na tayari kusaidia na kuwashauri marafik.
Mwanafunzi mwingine, Irene Chaboma, alimkumbuka kuwa "mchapakazi darasani na mmoja wa wanafunzi waliofanya vizuri. Roho yake ipumzike kwa amani."
Kifo cha Clemence Mtenga
Inakadiriwa kuwa karibu watu 1,200 waliuawa wakati wa shambulio la Hamas huku watu wenye silaha wakiwachukua mateka zaidi ya watu 200, miongoni mwao watu kadhaa kutoka mataifa ya kigeni.
Awali Israel ilisema kuwa Clemence na Mtanzania mwenzake Joshua Loitu Mollel walikuwa miongoni mwa mateka hao.
Hata hivyo baada ya taarifa za mamlaka za Tanzania, ni kuwa Clemence si mmoja wa mateka wawili ambao miili yao imeopolewa kutoka Gaza, kwa hivyo bado haijafahamika alifia wapi na jinsi gani.
Hata hivyo mamlaka ilieleza kuwa inafuatilia kwa karibu Mtanzania Joshua Mollel ambaye anadaiwa kushikiliwa mateka.
Watanzania hao wawili walikuwa wakiishi Israel kama sehemu ya programu ya mafunzo ya kilimo. Walitarajiwa kukaa nchini kwa miezi 11 zaidi. Takribani Watanzania 260 wanasomea kilimo nchini Israel.
Serikali za Tanzania, Israel zazungumza
Katika ibada ya mazishi iliyofanyika katika kanisa la Mt Joseph lililopo Mashati Rombo, viongozi mbalimbali ndugu na jamaa walitoa salamu za pole.
Katika salamu za serikali ya Israel, Balozi Mdogo wa Israel nchini Kenya, Dvora Yarkoni alisema Clemence ni kijana aliyekuwa na ndoto nyingi lakini ndoto zake zilikatishwa na hali inayoendelea.
Kwa upande wa Tanzania, Mkuu wilaya ya Rombo, Hamisi Maiga ambaye pia aliiwakilisha serikali ya Mkoa,Tunasikitika kuondokewa na kijana huyu. Tuliupokea mwili wa marehemu na kuukabidhi kwa familia. Kijana huyu alikuwa wa mfano na alienda Israel kwaajili ya kujiendeleza na kurudi kutumikia taifa.
Nayo Wizara ya mambo ya nje ya Tanzania, ilieleza kuwa itaendelea kuhakikisha kuwa watanzania wote walio nje ya nchi wako salama.
Imeandikwa na Alfred Lasteck na kuhaririwa na Lizzy Masinga