Lilipofikia soko la pamoja EAC si haba japo linahitaji ‘mganga’

Yusuf Mazimu

BBC Swahili

Bendera za Africa Mashariki

Chanzo cha picha, EACJ

Maelezo ya picha, Bendera za Africa Mashariki

Wakuu wa nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) mwishoni mwa juma walihitimisha mkutano wao wa siku mbili wa Jumuiya hiyo uliokuwa unafanyika jijini Arusha, Tanzania.

Kikao hicho kiliwaleta pamoja marais wa nchi za Kenya, Tanzania, Uganda na Burundi. Rai wa Somalia alishiriki kama nchi mwalikwa, na nchi zingine wanachama; Sudan Kusini, Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, na Rwanda wakituma wawakilishi.

Mbali na viongozi hao, kikao hicho kiliwajumuisha pia viongozi wengine wakiwemo mawaziri kutoka nchi hizo na wageni zaidi ya 300.

Ni mkutano wa kawaida wa 22 ambapo pamoja na mambo mengine ajenda kubwa na muhimu ilikuwa kuhusu utekelezaji wa itifaki ya soko la pamoja la bidhaa na huduma. Utekelezaji wa soko hili umeanza miaka 12 iliyopita, hoja ni mwamba kuna hatua imepigwa? Kuna lolote lakujivunia? Na kwa kiasi gani changamato zake zinapunguza kasi utekelezaji wake?

Lilipotoka Soko la Pamoja la EAC na msingi wake

Wazo la kuwa na soko la pamoja la Afrika Mashariki, halikuwa geni sana wakati likianzishwa, lilikuwepo huko nyuma tangu Afrika Mashariki ikiundwa na nchi tatu tu wanachama; Kenya, Uganda na Tanzania, ingawa lilitumika kwa misingi na taratibu tofauti na za sasa.

Wengi wanasema ni kama mfano wa soko la pamoja la Ulaya, ambalo ni kongwe linaloruhusu uhuru wa bishara, bidhaa, watu na fedha miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ulaya (EU).

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Julai 2010, nchi wanachama wa EAC; Burudi, Kenya, Rwanda, Uganda na Tanzania zilianza rasmi kutekeleza makubaliano soko la pamoja kwa mkataba uliolenga kujenga misingi ya kuruhusu uhuru wa mitaji, uhuru wa bidhaa na uhuru wa watu kuvuka kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine za Afrika Mashariki.

Katika mkataba huo kulikuwepo pia makubaliano mengine madogo madogo lukuki ambayo nchi wanachama zilipaswa kurekebisha ili kufikia malengo.

Makubaliano hayo mengine ya kufanyiwa marekebisho ni pamoja na sheria, mifumo na utaratibu kwa lengo la kusaidia kukuza biashara na utengamano kwa nchi za afrika mashariki.

Leo ni miaka 12 imetimia tangu kuanzishwa kwa utekelezaji wa soko hilo la Pamoha, huku wanachama wapya wawili wakiongezeka, mataifa ya DRC na Sudan Kusini.

Hatua ya soko la pamoja haihusu tu bidhaa bali pia kulegezwa kwa masharti kwa usafiri wa watu na upatikanaji wa ajira na huduma katika mataifa wanachama, jambo linaloendelea kuzua mijadala.

Kwanini Soko hili ni muhimu kwa Afrika Mashariki?

Kwa tafsiri ya kawaida isiyo rasmi, Soko la Pamoja maana yake ni makubaliano ya pamoja ya nchi kwenye vikwazo vinavyoingiliana ili kuruhusu uhuru wa biashara, nguvu kazi au watu, na mitaji baina ya nchi hizo.

Uhuru huu unawekwa ili kusaidia kuinua uchumi utakaonufaisha nchi zote wanachama wa makubaliano hayo.

Faida kubwa kwa wananchi wa Afrika Mashariki kwa makubaliano ya kuwa na soko la pamoja ni pamoja na wananchi wa nchi wanachama kuwa na uhuru wa kufanya biashara bila kuingiliwa na Mamlaka na vikwazo vikubwa vya kiushuru.

Uhuru wa kuwekeza waonapo fursa ya uwekezaji. Kuweka mitaji katika masoko ya hisa ni jambo linalotazamwa kama faida kubwa kwa wananchi wa nchi hizo, ukiachilia uhuru wao wa kusafiri na kuchangamana.

Kiuchumi, kuwa na soko la aina hii ni kusaidia kuboresha uzalishaji wa bidhaa, kwa sabababu ya ushindani wa kimahitaji na kupanuka kwa soko la bidhaa na huduma miongoni mwa wanachama.

Ingawa nchi ambazo hazina uchumi imara na uzalishaji bora wa bidhaa na huduma bora zitajiona kuweweseka kwenye soko hili na kuziacha nchi imara kunufaika zaidi.

Majivuno ya mashaka ya soko la pamoja EAC

Wakati wa majadiliano ya mkutano wa 22 wa wakuu wa nchi za Afrika Mashariki, mafanikio ya utekelezaji wa soko la Pamoja, ilikuwa ajenda kubwa. Wakuu hawa walitaja mafaniko kadhaa ya kujivunia yaliyofikiwa tangu kuanzishwa kwa soko hilo.

Mwenyekiti wa EAC ambaye ni Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta alinukuliwa akisema moja ya mambo ambayo yamekuwa na manufaa ni uboreshwaji wa miundombinu katika nchi wanachama akieleza nchi wananchi wa Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Sudani Kusini hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanaunganishwa na barabara na miradi mingine ikiwepo ya umeme.

Bila shaka, miundo mbinu ni eneo la msingi kwa kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na watu baina ya nchi hizi za jumuiya hii, hakuna shaka katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, miundombinu katika nchi hizi imeimarika na kuboreshwa kwa kiasi kikubwa.

Suala la watu kusaifiri baina ya nchi wanachama wa Afrika Mashariki limerahishishwa zaidi tofauti na miaka 15 iliyopita, jambo ambalo hata Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye amelisifia.

Hakuna vikwavo vikubwa kama zamani. Vivyo hivyo pia kwenye eneo la usafirishaji wa bidhaaa, vikwazo visivyo vya ushuru vimepunguzwa kwa kiasi kikubwa ikiwemo utitiri wa vituo va ukaguzi wa magari na bidhaa zinazosafrishwa baina ya nchi wanachama.

Kwa kauli za viongozi wa mataifa haya, unaweza kuona wanajivunia kilichofanyika mpaka sasa kwenye utekelezaji wa soko hilo la pamoja, licha ya jitihada kubwa kuendelea kuhitajika.

‘Wanajivunia, na sio mbaya kwa hatua zilizopigwa, lakini wajivune kwa mashaka, kwani kuna mengi ya kufanywa, sheria, sera na dhamira ya kisiasa ndiyo mtaji pekee wa kuwa na soko la pamoja lisilo la mashaka na la dhati Afrika Mashariki’, anasema Beatrice Kimaro, Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Ushirika, Moshi, Tanzania.

Lilipofikia soko la Pamoja EAC si haba ila linahitaji ‘mganga’

Viongozi wa Afrika Mashariki

Chanzo cha picha, EAC

Maelezo ya picha, Viongozi wa Afrika Mashariki

Kwa kipimo cha lilipotoka na lilipo sasa, bila shaka soko la Pamoja la Afrika Mashariki, lina hatua limepiga.

Awali Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, Dkt. Peter Mathuki akizungumza katika mkutano huo wa 22 wa EAC huko Arusha alieleza mafanikio ya soko la pamoja kuwa ni pamoja na kukuza uchumi, biashara, ajira na kukuza mitaji baina ya nchi wanachama, akiipongeza sekta binafsi kwa mchango wake katika hilo.

Pamoja na mafanikio haya, bado kuna maswali mengi kwenye utekelezaji wake ukirejea misingi ya kuanzisha kwa mkataba wa soko la pamoja: Uhuru wa mitaji, uhuru wa bidhaa na uhuru wa watu.

Kwenye soko la fedha (uhuru wa mitaji), Tanzania inaonekana imepiga hatua ikiruhusu zaidi wageni kuwekeza kwenye soko lake la hisa la Dar es Salaam, hoja iliyopo, kwa kiwango gani nchi zingine zinaruhusu kwa ukubwa huo wageni kuwekeza mitaji yao kwa nchi hizo?

‘Shirika la ndege la Kenya (Kenya Airways) limeweza kufika Tanzania kwa kuingia kwenye soko la hisa. Lakini je Rwanda inaruhusu? Burundi inaruhusu? Aliwahi kuuliza Lousi Accaro, mkurugenzi wa huduma kwa wanchama, TPST.

Alihoji pia katika eneo la bima na hata sekta ya madini.

‘Masuala ya bima, kuwekeza Tanzania, Mtanzania lazima awe na hisa asilimi 35, lakini nchi nyingine kama Kenya ili kuwekeza kwenye soko la bima, mkenya lazima awe na asilimia 60. Kwenye suala la madini, Kenya wamesema kwamba ili kuwekeza Kenya, kwa mtu ambaye sio mkenya, mkenya lazima awe na asilimi 60, sisi bado hatujafikia huko’.

Katika kipindi cha miaka 12 ya utekelezaji wa soko hili, tumeshuhudia na kusikia mengi yanayoleta ukakasi na mashaka licha ya uwepo wa mkataba huu; malori yakizuiwa mipakani, bidhaa zikizuiwa, ushuru kwa bidhaa, mifugo ikichomwa moto. Kwa ujumla vimekuwepo vikwazo vingi vya kisheria na kisera.

‘Bado kuna mengi ya kufanywa, na muda unaruhusu, muhimu ni dhamira ya wazi na utashi wa kisiasa kwa viongozi wa mataifa haya’. Lazima mkataba utekelezwe ulivyo na uboreshwe kwa usawa, kwa kuzingatia uwezo wa kila taifa mwanachama’, anasema Beatrice Kimaro, mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, Tanzania.

Mambo haya makubwa mawili anayoyataja mhadhiri huyu ndiyo ‘mganga’ mkubwa wa kufikia malengo ya kuwa na soko la pamoja madhubuti kwa Afrika Mashariki, vinginevyo kutakuwa na soko la pamoja lakini lisilo pamoja kwa utekelezaji.