Kwanini daktari huyu alituhumiwa kuwafunga kizazi maelfu ya wanawake?

Chanzo cha picha, Mohammed Shafi
Je, kuna kidonge kinachoweza kuwafanya watu wasizae? na Je, umewahi kusikia kuhusu visa vya daktari kuwafunga uzazi wanawake kisiri wakati wa kujifungua kwa upasuaji?
Hizi zote ni nadharia za njama zinazosambaa miongoni mwa wafuasi wa dini ya Kibudha wanaopinga Uislamu nchini Sri Lanka.
Madai yameibuka kwamba Waislamu walio wachache nchini humo wanajaribu kisiri kuongeza idadi ya watu wao kwa kuwafunga kizazi wanawake wa jamii ya Wabuddha walio wengi.
Mwanamume mmoja, daktari kutoka mji wa kaskazini-magharibi wa Kurunegala, alikuwa mlengwa wa tuhuma isiyowezekana.
"Mimi ni Muislamu, na nilishutumiwa kwa kuwafunga kizazi wanawake 4,000 wa Kibudha," Mohamed Shafi, daktari wa upasuaji aliiambia BBC.
Dk Shafi alishtakiwa kwa uwongo kwa kubana mirija ya uzazi ya wagonjwa wa Kibudha hasa wakati wa upasuaji, hivyo kuwazuia kupata watoto zaidi.
Alikamatwa tarehe 24 Mei 2019 na kushtakiwa chini ya sheria za ugaidi.
"Niliwekwa kwenye seli pamoja na wahalifu. Nilijiuliza, kwa nini wananifanyia hivi? Ilibidi nivumilie kwa ajili ya mke wangu na watoto wangu," Dk Shafi alisema.
Baba wa watoto watatu alizuiliwa gerezani kwa siku 60.
Mnamo Julai 2019, mahakama ilikubali dhamana, lakini alipewa likizo ya lazima kwa sababu uchunguzi dhidi yake ulikuwa unaendelea.
Miaka minne baada ya kukamatwa, Mohamed Shafi alirejeshwa kazini na Wizara ya Afya ya Sri Lanka mnamo Mei 2023 kutokana na ukosefu wa ushahidi unaounga mkono shutuma dhidi yake.
Shambulio la bomu la Jumapili ya Pasaka

Chanzo cha picha, AFP
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Waumini wa Kibudha wanajumuisha asilimia 70 ya wakazi milioni 22 wa Sri Lanka, Waislamu karibu asilimia 10. Pia kuna Wahindu (karibu asilimia12) na Wakristo (asilimia 7).
Kabla ya shutuma hizo, Dk Shafi alikuwa akiwatibu wagonjwa kutoka katika jumuiya zote hizi za kidini.
Lakini tarehe 21 Aprili 2019 - Jumapili ya Pasaka - msururu wa mashambulio ya mabomu ulilenga makanisa na hoteli za kitalii, na kuua zaidi ya watu 250. Tukio hilo lilibadilisha maisha ya Dk Shafi milele.
Licha ya kwamba mashambulizi hayo yalitekelezwa na kundi la watu wenye msimamo mkali wa kidini wanaohusishwa na kundi la Islamic State (IS), mashambulizi hayo yalikuwa mabaya zaidi tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo dhidi ya wanaotaka kujitenga wa Tamil Tiger kumalizika mwaka 2009.
Mashambulio hayo ya mabomu yalizua wimbi la chuki dhidi ya Waislamu kote Sri Lanka.
Katika hatua ya kulipiza kisasi, misikiti, nyumba na maduka yanayomilikiwa na Waislamu yalichomwa moto, na mwanamume mmoja Mwislamu kuawa kwa kukatwakatwa na kundi la watu.
Tuhuma za uwongo

Chanzo cha picha, Divaina
Mnamo tarehe 23 Mei 2019, mwezi mmoja baada ya shambulio la mabomu ya Jumapili ya Pasaka, gazeti kuu la 'Divaina' lilichapisha makala katika ukurasa wake wa mbele ikidai "Daktari wa Thawheed Jamath amewafunga kizazi wanawake 4,000 wa Kibudha wa Kisinhali. Maelezo yalifichuliwa baada kuthibitisha yaliyojiri. Uchunguzi mkubwa uliofanywa ili kumkamata daktari huyo ."
National Thawheed Jamath lilikuwa mojawapo ya makundi mawili ya Kiislamu ya eneo hilo yaliyotuhumiwa kuhusika na mashambulizi ya Jumapili ya Pasaka.
Gazeti hilo halikutoa vyanzo vyovyote vya kuunga mkono madai hayo wala kufichua utambulisho wa Dk Shafi, lakini shutuma za kuwafunga kizazi wanawake wa Kibudha zikimhusisha Dk Shafi pamoja na picha yake na eneo aliko ziliibuka kwenye mtandao wa Facebook.
"Hiyo ndiyo mara yangu ya kwanza kuhusishwa hadharani na madai hayo," aliambia BBC.
Dk Shafi anasema kuwa yeye, mshauri wa wadi na maafisa wenzake wakuu walimtembelea mkurugenzi wa Hospitali ya Kurunegala, Dk Sarath Weerabandara, kuripoti tuhuma za uwongo dhidi yake kwenye mitandao ya kijamii na kuelezea wasiwasi wake juu ya hatari inayoweza kumkabili.
Hata hivyo, Dk Weerabandara alijibu kuwa anaweza kushughulikia masuala ya ndani ya hospitali pekee na si nje.
Siku mbili baadaye, Dk Shafi alikamatwa.
“Nilipelekwa polisi bila kibali na kufungwa jela ili kuepusha fujo za wananchi,” alisema.
''Vyombo vya habari vya uchochezi''

Chanzo cha picha, AFP
Suala hilo lilizingatiwa zaidi wakati vituo vya televisheni vilipoangazia taarifa hiyo, na shutuma za uwongo zilizoenea kwenye mitandao ya kijamii.
"Nilitengenezewa mazingira. Nikavi kwa taji la ugaidi hadharani. Vituo vyote vya televisheni vilivyoangazia habari ghushi kwenye mitandao ya kijamii kimsingi ziliharibu maisha yangu," Dkt Shafi alisema.
Watawa wa Kibudha walianza kuandamana nje ya hospitali ambako mke wa Dk Shafi, Fathima Imara, pia alifanya kazi.
"Mke wangu alipokea vitisho vya kuuawa. Alihofia maisha ya watoto wetu," Dkt Shafi alisema, akiongeza kuwa pia alikuwa karibu kupoteza kazi yake.
"Binti yangu mkubwa alikuwa akijiandaa kwa mitihani yake na alitaka kwenda shule. Lakini hatukuweza kufanya hivyo kwa sababu ya hasira ya umma dhidi yetu. Alikuwa amevunjika moyo - ilitubidi tutafute shule mpya kwa ajili ya watoto wetu," aliongeza.

Chanzo cha picha, Anadolu Agency/Getty Images
Baada ya kukamatwa kwake, mkewe na watoto wao watatu walihamia Colombo. Tangu wakati huo, watoto wake wamesoma shule tatu tofauti.
"Mke wangu na watoto walilazimika kutoroka kutoka sehemu moja hadi nyingine. Na hawakuwa na pesa kwani akaunti zangu zilifungiwa," Dk Shafi alisema.
Ingawa takriban wanawake 800 walitoa taarifa kuhusu Mohamed Shafi - ambayo viongozi wa hospitali walitaja kama "malalamiko" - mnamo 27 Juni 2019, Idara ya Upelelezi wa Jinai ya Sri Lanka (CID) iliiambia mahakama kwamba hakuna ushahidi uliopatikana dhidi ya Dk Shafi kuhusu taratibu za siri za kufunga uzazi.
Zaidi ya hayo, ripoti kutoka kwa mashirika mbalimbali ya sheria na kijasusi nchini Sri Lanka, ikiwa ni pamoja na Huduma ya Ujasusi ya Serikali, zilisema hakuna ushahidi unaomhusisha Shafi na shughuli zozote za kigaidi.














