Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Mwanangu anajua sauti ya mabomu kuliko anavyojua sauti za wanasesere'
- Author, Lara El Gibaly and Haya Al Badarneh
- Nafasi, BBC Eye Investigations
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Ndani ya siku chache baada ya Israel kuanzisha vita huko Gaza, Oktoba iliyopita, Wapalestina wawili walianza kurekodi maisha yao ya kila siku kwa ajili ya BBC.
Aseel alikimbilia kusini mwa Gaza ili kupata hifadhi, Khalid alichagua kubaki kaskazini. Wote wawili, wanashuhudia milipuko, kuhamishwa mara nyingi, vifo na kiwewe kinachowapata watoto waliojikuta katikati vita.
Khalid na watoto wake
Kwenye sebule ya nyumba ya ghorofa iliyopigwa bomu kaskazini mwa Gaza, mtoto Hamoud mwenye umri wa miaka sita na Halloum mwenye umri wa miaka minne wanaigiza kama wahudumu wa afya na mwanasesere mdogo wakiigiza kama wanamshona.
"Amejeruhiwa," Hamoud anasema. "Kifusi kingi kilimwangukia."
Mtu mmoja kati ya watu watatu waliouwawa katika vita vilivyoanza Oktoba 2023 ni mtoto, kulingana na wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas.
Vita vinavyoendelea vilianza baada ya takribani watu 1,200 kuuawa katika mashambulizi ya Hamas ya tarehe 7 Oktoba.
Khalid, baba wa watoto hao, anatazama kwa mbali akiwa na wasiwasi juu ya namna wanavyocheza.
"Hii si michezo ambayo watoto wanapaswa kucheza," anasema Khalid. "Ninapowaona hivi, moyo wangu unavunjika."
Hospitali za kaskazini mwa Gaza zilipoacha kufanya kazi mwezi Disemba, miezi michache tangu kuanza kwa vita, Khalid alikwenda kinyume na maagizo ya Israel ya kuhama kusini na kuamua kukaa katika kitongoji chake cha Jabalia, kaskazini mwa Gaza, ili kutoa huduma za matibabu kwa jamii yake.
Khalid si daktari, lakini ana mafunzo ya tibamaungo, na alifanya kazi ya usambazaji madawa katika kampuni ya vifaa vya matibabu.
“Kila mtu katika eneo langu anajua mimi ni mtaalamu wa tibamaungo, si daktari. Lakini kutokana na hali ngumu, niliwaambia naweza kubadili bandeji na kushona majeraha, hasa kwa watoto. Nikiondoka, wale ninaowahudumia wanaweza kupoteza maisha, kwa sababu hakuna hospitali wala zahanati.”
Akiwa na ujuzi mdogo wa upasuaji na uwezo wa kupata madawa - baadhi yao zikiwa zimeshaisha muda wake - alifungua kliniki nyumbani kwake, ambapo alilenga kutibu watoto. Watoto wake walianza kuiga walichokiona.
"Ambulensi, mpeleke kwenye gari la wagonjwa!" Hamoud alisema, wakati yeye na dadake wakicheza kama watoa huduma za dharura, moja ya mchezo mpya ambao umeibuka wakati wa vita.
Khalid anamsikia mwanawe akijaribu kuuliza aina ya jeraha. Je, ni jeraha la risasi, makombora, au kuporomoka kwa jengo?
“Hamoud anafahamu zaidi sauti za mabomu kuliko sauti za vidude vyake vya kuchezea. Na Halloum amepitia mengi kwa umri wake,” anasema Khalid. "Ninaogopa athari za muda mrefu za kisaikolojia za vita hivi kwao."
Kamati ya Kimataifa ya uokoaji inasema kuhama, kiwewe, na kukosa kwenda shule yanaweza kuwa na athari ya muda mrefu katika maisha ya watoto wa Gaza.
Wakiwa wamekwama kaskazini, watoto wa Khalid wamepata sio tu athari za kisaikolojia, lakini pia kiwango cha njaa ambacho hakijawahi kushuhudiwa. Mwezi Juni, Umoja wa Mataifa ulikadiria kuwa 96% ya watu wa Gaza wanakabiliwa na "uhaba mkubwa wa chakula."
Huku Hamoud akiwa ameweka bendera juu ya paa la nyumba, akiashiria kuomba msaada kwa ndege ya msaada kurusha vifurushi vya mahitaji karibu na nyumba yake, kishindo cha kutisha kinatikisa ardhi. Ndege ya Israel ilikuwa imedondosha bomu kwenye jengo la karibu, moshi mwingi uliokuwa ukiongezeka ulionekana umbali wa mita chache.
"Sipendi ndege zinazorusha mabomu," anasema Hamoud kwa huzuni. "Badala yake nataka watuachie chakula."
Aseel, mume na watoto wake
Kusini mwa Gaza, mama mwenye umri wa miaka 24 aliyejifungua hivi karibuni mtoto wake wa pili - Aseel, anatafakari jinsi atakavyo mlisha binti yake mchanga, Hayat.
"Hakuna chakula sokoni ili niweze kula ipasavyo na kumnyonyesha, kwa hivyo lazima nimpe maziwa ya unga," anasema Aseel.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) limeonya mwezi huu kwamba wanawake 17,000 wajawazito huko Gaza sasa wako kwenye ukingo wa njaa.
"Maziwa, nepi, kila kitu ambacho watoto wanahitaji kimekuwa ghali sana wakati wa vita," anasema mume wa Aseel, Ibrahim. “Hata kuviona tu ni changamoto,” anaongeza.
Aseel, mume wake, na mtoto wao mdogo wa miezi 14 aitwaye Rose, walilazimika kuondoka nyumbani kwao na kuelekea kusini katika wiki za kwanza ya vita, kutii maagizo ya Israel ya kuhama.
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa Wapalestina tisa kati ya 10 huko Gaza wamelazimika kuyahama makazi yao angalau mara moja tangu kuanza kwa vita Oktoba 2023.
Aseel akiwa na ujauzito wa miezi minane, ilimbidi atembee maili nyingi kwenda kusini - kupitia njia salama iliyochaguliwa.
“Hatukuwa na maji ya kutosha, na nilikuwa nikisumbuliwa na upungufu wa damu. Kulikuwa na miili imetapakaa mitaani. Nilichoweza kufikiria ni binti yangu Rose, na mtoto anayekua tumboni.”
Aseel na mume wake waliingia makubaliano, “ikiwa lolote litampata (mumewe), niendelee na safari peke yangu na kumtunza binti yetu Rose na mtoto. Na ikiwa ningezimia kwa sababu ya uchovu, anapaswa kuendelea na safari na binti yetu na kuniacha nyuma.
Mara tu walipofika eneo salama la Deir al-Balah upande wa kusini, tatizo jipya lilijitokeza; hapakuwa na hospitali zinazofanya kazi ambapo angeweza kujifungua mtoto wake. Hospitali ya Al Awda huko Nuseirat ilikuwa kituo pekee cha karibu ambacho kingeweza kushughulikia uzazi.
Binti wa Aseel, Hayat, alizaliwa katika hospital hiyo tarehe 13 Desemba. Jina lake, ni neno la Kiarabu lenye maana ya ‘maisha,’ lilichaguliwa kama ukumbusho wa maisha kamili, yenye furaha wanayotarajia kuanza tena mara tu vita vitakapoisha.
"Ni kama amenirudishia uhai, katikati ya uharibifu huu wote. Ananikumbusha kwamba maisha yanaweza kuendelea hata katika hali ngumu.”
Ibrahim, mpiga picha, alilazimika kumwacha mke wake, binti yake Rose, na mtoto wake mchanga ili kwenda shambani na kufanya kazi, akiyaweka maisha yake hatarini ili kuwahudumia.
Katika tukio moja alijikuta katikati ya mapigano na akaponea chupuchupu, anasema “haya yote ninayafanya ili kuwapa mambo ya msingi maishani, nepi, maziwa na nguo.”
"Ninahisi uzito wote wa Gaza uko kwenye mabega yangu, nina wasiwasi sana kuhusu binti zangu, na ninahisi siwezi kumtunza mtoto wangu mchanga."
Mwezi Mei, Ibrahim na Aseel wanakutana tena huko Deir al-Balah, na kuwachukua watoto wao kwa matembezi katika gari.
"Hayat hajapitikiwa na siku hata moja bila vita," Ibrahim anasema. "Alizaliwa katikati ya matukio haya ya vita, huku kukiwa na sauti ya mabomu na taarifa za habari."
Hayat mwenye umri wa miezi sita amekaa kwenye mapaja ya mama yake kwenye kiti cha mbele. Gari linapita katika majengo yaliyobomolewa, katika Barabara zenye mchanga na vifusi.
"Licha ya hayo yote," Ibrahim anasema, "anaendelea kutabasamu."
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah