Jinsi kichungi cha sigara kilivyofichua siri ya uhalifu wa miaka 30

Chanzo cha picha, Getty Images
Zaidi ya miaka 30 baada ya Mary McLachlan kuuawa, kichungi cha sigara kilichopatikana katika nyumba yake kilitoa muelekeo wa kwanza kuhusu utambulisho wa muuaji.
Sampuli za DNA zilizopatikana kwenye mkanda uliotumika kumnyonga Mary, mama wa watoto kumi na moja, zililingana na zile zilizopatikana kwenye kichungi cha sigara.
Ugunduzi huo uliwavunja moyo wachunguzi wa kesi hiyo ya muda mrefu, kwani mshukiwa mkuu alikuwa gerezani mjini Edinburgh wakati mwili wa Mary McLachlan mwenye umri wa miaka 58 ulipopatikana magharibi mwa jiji la Glasgow.
Lakini ofisi ya msimamizi wa gereza ilithibitisha kuwa Graham McGill, alikuwa amehukumiwa na alikuwa nje kwa dhamana wakati wa mauaji ya Mary McLachlan.
Rekodi zilionyesha kuwa alirudi kwenye selo yake ya gerezani saa chache baada ya kutoka nyumbani kwa Mary majira ya alfajiri mnamo Septemba 27, 1984.

Makala ya BBC, iliyohusua kumtafuta aliyemuua Mary McLachlan", inasimulia uchunguzi wa kesi hii ya muda mrefu na athari mbaya ya mauaji haya kwa familia yake na wapendwa wake.
"Kuna mauaji mengine yanayorejea akilini kwa miaka mingi," anasema mtaalamu mwandamizi wa uchunguzi wa vifo Joanna Cochrane. "Mauaji ya Mary yalikuwa miongoni mwa kesi za zamani zenye maumivu sana nilizowahi kuchunguza."
Mary alitumia usiku wake wa mwisho akinywa na kucheza dominó kwenye Mgahawa wa Hindland, ambao sasa unaitwa Dock Club unaotazama Mansfield Park.
Aliondoka mgahawani kati ya saa 11:15 na 11:30 alfajiri na kutembea kwa miguu karibu kilomita mbili hadi nyumbani kwake.
Njiani, alisimama kwenye Duka kubwa la Armando's katika Mtaa wa Dumbarton, akafanya utani na wafanyakazi na kununua vinywaji pamoja na sigara.
Dereva wa teksi aliyemfahamu Mary alisema alimuona mwanaume mmoja akimfuata kwa nyuma Mary alfajiri hiyo wakati alikuwa akitembea pekupeku , akiwa ameshika viatu vyake mkononi.

Chanzo cha picha, FIRECREST
Mfulululizo wa matukio na jinsi McGill alivyofika kwenye ghorofa ya tatu ya nyumba ya Mary katika jengo la Creighton Court haujulikani wazi, lakini hakuna dalili kuwa mlango wa nyumba hiyo ulivunjwa.
Alipoingia, muuaji alimshambulia kwa ukatili mwanamke huyo aliyekuwa na umri mara mbili ya wake.
Hakukuwa na simu za mkononi wakati huo, hivyo Mary hakuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na familia yake waliokuwa wakiishi Glasgow, Lanarkshire na Ayrshire.
Mwanawe mmoja, Martin Cullen, alikuwa akimtembelea mara moja kwa wiki.
Alipofika nyumbani kwa Mary mnamo Oktoba 2, 1984, aligonga mlango lakini hapakuwa na jibu, na kulikuwa na harufu kali ya kuchukiza.
Alimkuta Mary akiwa amelala kifudifudi juu ya godoro.
Alikuwa na fizi na meno bandia, yaliyonekana kando, na gauni lake jipya la kijani alilovaa alipokwenda mgahawani lilikuwa limevaliwa kwa kupinduliwa, nje ndani ndani nje.

Chanzo cha picha, Getty Images
Afisa wa zamani Ian Wishart anaeleza eneo la tukio la mauaji kama "ukatili wa kushangaza."
"Jambo la kuhuzunisha ni kwamba Mary alikuwa akimtazama usoni muuaji wake alipokuwa anauawa," anasema.
Uchunguzi wa baada ya kifo ulionyesha kuwa Mary alifariki siku tano kabla kutokana na kunyongwa.
Wapelelezi walikusanya zaidi ya taarifa 1,000 miezi ya mwanzo baada ya mauaji, lakini upelelezi haukufika popote kumpata muuaji.
Mwaka mmoja baada ya mauaji, familia iliambiwa uchunguzi umefungwa, lakini daktari wa uchunguzi alimwambia binti wa Mary, Gina McGavin, "usikate tamaa."

Mary alikuwa na watoto kumi na mmoja kutoka kwa wanaume wawili tofauti na alikuwa anajulikana sana katika jamii yake.
Binti yake Gina anasema kwenye makala ya BBC kwamba kulikuwa na migogoro wakati Mary alipoondoka na watoto sita na kuishi na watoto wake wengine watano kutoka kwa mpenzi aliyempata baadaye.
"Niliwaza kwamba muuaji alikuwa mtu wa familia," anasema.
Gina, ambaye ameandika kitabu kuhusu mauaji ya mama yake, anasema aliwahi kushirikiana na polisi kuhusu hisia hizo.
"Ndugu zangu na dada zangu walidhani hivyo pia mwaka 1984," anasema.
"Moja ya watoto wake huenda alihusika au alikuwa na taarifa zaidi kuhusu tukio hilo, lakini hatuwezi kuthibitisha jambo lolote."

Chanzo cha picha, CROWN OFFICE
Mpaka kufikia mwaka 2008, uchunguzi wa mara ya nne ulikuwa umeshindwa kumbaini mshukiwa wa mauaji hayo.
Uchunguzi wa tano ulianza mwaka 2014, na hatimaye mafanikio yalitokea kupitia kituo kipya cha utambuzi wa DNA katika Scottish Crime Campus huko Garthcash, North Lanarkshire.
Awali, wataalamu waliweza kuchunguza sifa 11 za DNA pekee, lakini teknolojia mpya iliruhusu kuchunguza hadi sifa 24.
Hii ilisaidia pakubwa kupata taarifa hata kutoka kwenye sampuli ndogo au zenye ubora wa chini.
Tom Nelson, mkurugenzi wa uchunguzi wa kisayansi Police Scotland, alisema mwaka 2015 kuwa teknolojia imewezesha "kurudi nyuma na kuleta haki kwa wale waliokuwa wamekata tamaa."

Chanzo cha picha, FIRECREST
Sampuli na ushahidi uliokusanywa mwaka 1984 ulijumuisha nywele chache, sampuli za tishu kutoka chini ya kucha, na vichungi vya sigara.
Mtaalamu mwandamizi Joanna Cochrane aliombwa kuchunguza ushahidi kutoka eneo la mauaji ambao ulikuwa umehifadhiwa kwenye mifuko ya karatasi kwa zaidi ya miaka 30.
"Hawakuwa na ujuzi wowote kuhusu upimaji wa DNA wakati huo," anasema.
"Hawakuwa na wazo kuwa ushahidi huo ungeweza kuwa na thamani kubwa siku moja."

Chanzo cha picha, FIRECREST
Mafanikio muhimu ya uchunguzi yalianza na kichungu cha sigara ya aina ya "Embassy" kilichopatikana kwenye kidude cha kuwekea vichungi na majivu ya sigara kilichokuwa sebuleni kwenye meza.
Kwa kuwa sigara aliyopenda Mary ilikuwa Woodbine, jambo hili liliibua wasiwasi kwa timu ya uchunguzi wa kesi hii ya zamani.
Joanna Cochrane anasema alitumaini maendeleo ya kiteknolojia kumwezesha kufuatilia viwango tofauti vya DNA.
"Tulipofikia wakati wa mafanikio makubwa," alisema kwenye makala ya BBC, "ni wakati kichungi cha sigara ambacho hapo awali hakikutoa DNA sasa kilitupatia taarifa zote kamili za mtuhuyo. Hii ilikuwa fursa ambayo hatukuwahi kuwa nayo kabla."

Chanzo cha picha, FIRECREST
Sampuli hiyo ilipelekwa kwenye kanzidata ya DNA ya Scotland ili kulinganishwa na maelfu ya taarifa za wahalifu waliokwisha hukumiwa.
Matokeo yalitumwa kwa Bi. Cochrane kupitia barua pepe kwa njia ya fomu.
Aliteremka haraka hadi sehemu ya chini ya fomu hiyo na kuona alama ya tiki pembeni mwa kisanduku cha "Inashabihiana."
Mtaalamu huyo alisema, "Ilikuwa ni wakati ambapo nywele za mwili wangu zilisimama."
Aliongeza: "Matokeo yalimtambua mtu aitwaye Graham McGill na niliweza kuona kwenye fomu kuwa alikuwa na rekodi kubwa ya makosa ya kingono."
"Baada ya zaidi ya miaka 30, hatimaye tulimpata mtu aliyelingana na DNA hiyo."

Chanzo cha picha, Google
Lakini mafanikio haya yaliyosubiriwa kwa muda mrefu katika uchunguzi yalikutana na fumbo tata baada ya kugundulika kuwa McGill alikuwa gerezani kwa kosa la ubakaji na jaribio la ubakaji wakati wa mauaji ya Mary.
Rekodi zilionyesha kuwa hakutolewa hadi Oktoba 5, 1984, siku tisa baada ya Mary McLachlin kuonekana hai mara ya mwisho.
Mpelelezi mstaafu Kenny McCubbin aliteuliwa kutatua fumbo hili lisiloeleweka.
Bi Cochrane pia aliambiwa ushahidi zaidi wa kimaabara unahitajika ili kujenga kesi thabiti.

Chanzo cha picha, FIRECREST
Utafutaji wake wa ushahidi thabiti ulimpeleka kwenye hifadhi ya DNA" nyingine: mkanda wa pajama uliotumika kumnyonga Mary.
Bi Cochrane aliamini kulikuwa na uwezekano mkubwa kwamba mtu aliyefunga fundo alikuwa amegusa kipande cha kitambaa ambacho sasa kilikuwa kimejificha ndani.
Chini ya mwangaza mkali wa taa za maabara yake, alifungua mkanda huo polepole, fundo baada ya fundo, na kufichua kipande cha kitambaa kilichokuwa kimejifichwa kwa zaidi ya miongo mitatu.
"Tulipata kipande hicho muhimu cha ushahidi, kilikuwa na DNA iliyolingana na ya Graham McGill, kwenye mafundo ya kamba hiyo," alisema.
Aliongeza: "Alikuwa amefunga kamba hiyo shingoni mwa Mary na kuvuta mafundo hayo hadi kumnyonga."

Chanzo cha picha, FIRECREST
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Aidha, mabaki ya shahawa ya muuaji yalipatikana kwenye gauni la kijani alilokuwa amevaa Mary.
Lakini Bw. McCubbin, ambaye sasa amestaafu, alisema katika makala ya BBC kwamba ushahidi wa kimaabara pekee haukutosha kwa ajili ya hukumu.
"Haijalishi tulikuwa na DNA ya aina gani," alisema. "Mshukiwa alikuwa na udhuru mzito. Inawezekanaje mtu kufanya mauaji akiwa gerezani?"
Kupata rekodi hizo kulikuwa kugumu kwa sababu Gereza la HMP Edinburgh lilikuwa likikarabatiwa wakati wa mauaji hayo na kwa kuwa ilikuwa ni enzi za kabla ya kidijitali, nyaraka za karatasi kadhaa zilikuwa zimepotea.
Uchunguzi wa McCubbin hatimaye ulimfikisha kwenye Maktaba ya Taifa ya Scotland katikati mwa jiji la Edinburgh, ambako aliweza kupata ofisi ya msimamizi wa gereza.
Na rekodi moja tu iliibadilisha kila kitu.
Kando ya nambari ya mfungwa, jina Jay McGill na kifupisho TFF vilikuwa vimeandikwa.
"Hii ilimaanisha 'Training for Freedom' (mafunzo kwa ajili ya kuachiliwa huyu), yaani alipewa ruhusa ya kutoka gerezani kwa siku kadhaa," alieleza mpelelezi McCubbin.
Timu ya uchunguzi iligundua kuwa McGill alipata ruhusa ya kutoka kwa wikiendi mbili, ikiwa ni pamoja na siku tatu kabla ya kuachiwa rasmi, na alirudi gerezani Septemba 27, 1984.
"Hii ndiyo ilikuwa sehemu ya dhahabu ya ushahidi tuliokuwa tukitafuta," alisema Mark Henderson, aliyekuwa mkuu wa uchunguzi.

Chanzo cha picha, FIRECREST
McGill alikamatwa hatimaye tarehe 4 Desemba 2019.
Wakati huo bado alikuwa chini ya usimamizi kama mhalifu wa kingono lakini alikuwa akifanya kazi Linwood katika eneo la Glasgow.
Gina alisema habari hizo zilikuwa mkombozi kwake, na kuongeza, "Sikuwahi kufikiria ningeuona wakati huu katika maisha yangu."
McGill alipatikana na hatia baada ya kesi ya siku nne mnamo Aprili 2021 na kuhukumiwa kifungo cha chini cha miaka 14 gerezani.
Jaji Lord Burns katika Mahakama Kuu ya Glasgow alisema kuwa McGill alikuwa na umri wa miaka 22 alipomuua Mary lakini sasa ana umri wa miaka 59 anaposimama kizimbani.
"Familia yake imekuwa ikisubiri muda wote huu ili ukweli ujulikane, wakijua kwamba mtu aliyehusika na uhalifu huu huenda anaishi kwa uhuru katika jamii," aliongeza.
"Hawakuwahi kukata tamaa kwamba siku moja wangepata ukweli juu ya kilichompata."
Imetafsiriwa na Yusuph Mazimu












