Viatu vya wahalifu vilivyozua gumzo mtandaoni Kenya

Ng'ombe

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Peter Mwai
    • Nafasi, Reality Check

Serikali ya Kenya inapoendelea kukabiliana na wahalifu na wezi wa mifugo katika kaunti za kaskazini magharibi mwa nchi hiyo, Wakenya mtandaoni wamekuwa kwenye mvutano - hili sana likichochewa na habari za kupotosha.

Video na picha zisizohusiana kamwe na operesheni hiyo inayoendeshwa na polisi na wanajeshi zimekuwa zikisambazwa.

Kuna jaribio la baadhi ya watu kuwaonesha majangili hao kama waliowazidi akili maafisa wa usalama nao wengine wakijaribu kuwaonesha maafisa wa usalama, na hasa Majeshi ya Ulinzi ya Kenya (KDF) kama wenye nguvu na uwezo zaidi.

Tumeangazia baadhi ya picha na video hizi za kupotosha.

Viatu vyenye kwato si vya Kenya wala Nigeria

Picha zinazoonyesha viatu vilivyoongezwa kwato kwenye soli ili mtu anapotembea viache nyayo za mnyama ardhini zimesambazwa pia sana mtandaoni.

Miongoni mwa waliosambaza ni gavana wa zamani wa kaunti ya Nairobi Mike Sonko aliyeandika kwamba viatu kama hivyo hutumiwa na wahalifu kaskazini mwa Bonde la Ufa.

Alisema hilo huifanya vigumu kuwafuata wahalifu hao kwani utafikiria nyayo walizoacha ni za ng’ombe.

Sonko

Chanzo cha picha, Twitter/Sonko

Waliosambaza picha hizo wamekusudia kuonyesha uvumbuzi wa wahalifu na wezi wa mifugo na jinsi wanavyotumia ubunifu wao kuwakwepa maafisa wa usalama.

Lakini picha hizo hazina uhusiano wowote na Kenya, na si mara ya kwanza kusambaa mitandaoni.

Mapema Julai 2021, zilisambaa mtandaoni Kenya na Nigeria.

Uchunguzi wa BBC umebaini chanzo cha picha hizo ni Afrika Kusini.

Miongoni mwa watu wa kwanza kabisa kuchapisha picha hizo mtandaoni alikuwa ni Kevin Pietersen kwenye Twitter mnamo 3 Julai, 2021, ingawa mwishoni mwa mwaka jana alifuta ujumbe wake wa awali.

Alikuwa ameandika kuwa picha hizo zinaonyesha “viatu vilivyovaliwa na wawindaji haramu waliokamatwa katika [mbuga ya taifa ya] Kruger jana.”

Wezi wa mifugo

Chanzo cha picha, TWITTER

Msemaji wa Mbuga ya Taifa ya Kruger nchini Afrika Kusini ameiambia BBC kwamba ni kweli picha hizo zilipigwa katika mbuga hiyo.

“Picha hizo zilipigwa baada ya kukamatwa kwa majangili waliodhani wanaweza kuwapotosha askari wetu wenye ujuzi ambao mwishowe walifanikiwa kuwakamata licha ya juhudi zao hizo,” msemaji huyo Isaac Phaahla alisema.

“Hatuwezi kudhibiti kusambaa kwa picha hizo katika mitandao ya kijamii lakini matumaini yetu ni kuwa wenzetu watajifunza kutoka kwa tuliyoyapitia na wasidanganyike na wahalifu hawa.”

Mamlaka ya hifadhi za wanyama nchini Afrika Kusini ilikuwa imeripoti kuhusu kisa cha kilichowahusisha wawindaji haramu mnamo 2 Julai katika hifadhi hiyo.

Mmoja aliuawa katika ufyatulianaji risasi na walinzi na wengine wawili wakatoroka ingawa walikuwa wakiandamwa. Haijabainika iwapo kisa kilichorejelewa ndicho kilichohusisha viatu vilivyo pichani.

Video zinawaonyesha vijana kutoka Sudan Kusini

Kumekuwepo na video kadha zinazosambaa zikiwaonyesha vijana, baadhi wakiwa na silaha na sare za kijeshi, wakidaiwa kuwa wapiganajii kutoka jamii ya Pokot wakijiandaa kwa vita dhidi ya wanajeshi wa Kenya.

Moja ya hizo, ambayo imesambazwa pia na Bw Sonko, imetokana na video ndefu ambayo tulifanikiwa kuipata kwenye YouTube. Video hiyo ilipakiwa kwenye mtandao huo miaka miwili iliyopita na inadaiwa kuwaonyesha watu wa jamii ya Murle, Sudan Kusini wakijiandaa kwa vita dhidi ya makabila jirani.

Sonko

Chanzo cha picha, Twitter/Sonko

Video nyingine inaonyesha mkusanyiko mwingine wa watu, lakini inapokaribia kuisha unaweza kuiona bendera ya Sudan Kusini katika sare ya mmoja wa wanaume kwenye video hiyo.

Picha

Chanzo cha picha, Twitter

Picha hizi ni za wahalifu kutoka Nigeria

Picha nyingine imekuwa ikisambaa ikidaiwa kuwaonyesha wahalifu waliokuwa wamekamatwa na wanajeshi wa Kenya.

Mmoja wa walioisambaza alikuwa ameandika: “Ripoti: Majangili watatu wamekamatwa katika milima ya Lotelemoi na maafisa wa usalama kutoka idara mbalimbali. Wamepelekwa kambi ya jeshi iliyo karibu ambapo watapewa hotuba ya uhamasisho na wanajeshi.”

Hotuba hapo ni kejeli.

Wahalifu

Chanzo cha picha, Twiiter

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Ukitafuta picha hiyo kwenye Google inachipuza taarifa kuhusu wahalifu waliokuwa wamekamatwa na kuzuiliwa baada ya ufyatulianaji risasi na wanajeshi wa Nigeria katika jimbo la Kaduna, kaskazini magharibi mwa Nigeria.

Walikuwa wamewateka nyara watu takriban 30 ambao waliokolewa.

Ipo picha nyingine inayowaonyesha watu hao wakiwa na wanaume wengine wenye mavazi ya kiraia na wanajeshi watatu na mwanamume mmoja mwenye mavazi meusi wakiwa na silaha.

Ukizitazama sare za wanajeshi hao, utagundua kwamba rangi imekolea zaidi ya ilivyo kwenye sare zinazovaliwa na wanajeshi wa Kenya.

Video ni ya mapigano Afghanistan

Kuna video nyingine inayowaonyesha wanaume wakiwa kwenye eneo kame lenye milima na mabonde wakiwa wanafyatuliwa risasi kwa wingi.

Imekuwa ikidaiwa kuwaonyesha wahalifu wakiwa wanafyatuliwa risasi na wanajeshi wa Kenya.

Mmoja wa walioichapisha ameandika: “Wanajeshi wetu wa KDF wamefyatua risasi za kuwaonya majangili Pokot, Turkana na Bonde la Kerio. Majangili huelewa lugha moja tu; Kifo. Watakufa bila huruma.”