Wasiwasi huku Rwanda ikijiandaa kuwasili kwa wahamiaji wa Uingereza

Na Barbara Plett Usher

Mwandishi wa BBC Africa, Rwanda

Makazi ya Hope Hostel nchini Rwanda yako tayari kupokea wahamiaji wasiotakiwa kutoka Uingereza kwa siku 664.

Sasa, baada ya Bunge la Uingereza kuidhinisha sheria hiyo, serikali ya Rwanda inataka kujaza vyumba na kumbi hizi ambazo kwa sasa zina mwangwi ndani ya kipindi cha wiki chache.

Rwanda kwa kiasi kikubwa imekuwa ikifuatilia tu mabishano ya kisheria nchini Uingereza kuhusu mpango tata wa kuwapeleka wanaotafuta hifadhi katika nchi hii ya Afrika Mashariki.

Mahakama za Uingereza zimeweka rekodi ya haki za binadamu ya Kigali katika kipaumbele kwa kudai ulinzi zaidi kwa wale wanaoletwa hapa.

Wakati huo huo, Rwanda imejiandaa vilivyo kwa ajili ya kuwasili kwao tangu Juni 2022, miezi miwili baada ya makubaliano hayo.

Nilipata fursa ya kutembezwa katika makazi ya Hostel Hope yaliyopo katika mji mkuu, Kigali ya meneja, Ismael Bakina. Vyumba vyake vya kulala vimepangwa kwa umakini, vikiwa na huduma muhimu kama vile mazulia ya kusalia na vyoo.

Wafanyakazi wa bustani hukata ukingo wa maua unaopakana na uwanja wa mpira wa miguu na uwanja wa mpira wa kikapu kuuweka katika hali ya unadhifu, huku wapishi na wafanyakazi wa usafi wakitekeleza majukumu yao kwa ufanisi wa hali ya juu.

Pia kuna hema lenye safu za viti vinavyosubiri kutumika kuwapokea wahamiaji hao baada ya kupata hifadhi nchini Rwanda. Iwapo hawatastahiki bado watapata vibali vya kuishi. Au wanaweza kujaribu kwenda nchi nyingine, lakini si kurudi Uingereza.

Bw.Bakina ananiambia hosteli iko tayari kuanza shughuli iwapo itapewa taarifa kwa muda mfupi kuwapokea wanaotafuta hifadhi.

“Hata wangefika sasa, leo si kesho, tuna uwezo wa kuwapokea,” anasema. "Tunaweka utayari wetu kwa 100%.

Kupitia madirisha ya mabweni unaweza kuona vilima vya vitongoji nadhifu vya Kigali. Ni jiji zuri lenye mitaa yenye utaratibu na salama dhidi ya uhalifu. "Rwanda inafanya kazi" ndiyo kauli mbiu ya nchi hiyo inavyosema.

Baadhi ya waliowasili wanaweza kutafuta kazi hapa, lakini kuna maoni tofauti kuhusu iwapo Rwanda inahitaji wafanyakazi wapya.

"Nadhani itakuwa vizuri kiuchumi kwa taifa," anasema Emmanuel Kanimba, mmiliki wa mgahawa mjini Kigali.

"Najua watatoa mtaji wa watu, pia watazalisha bidhaa na huduma na pia kutumia. (Kisha kuna) mawazo mapya ambayo wanaweza kuleta katika uchumi wetu."

"Lakini utapata wapi kazi za watu hawa?" anauliza mwanaume mwingine. "Sisi wenyewe tumehitimu lakini bado hatujapata ajira. Tuko huko nje kutafuta kazi."

Hakutaka kutambulika akizungumzia mtazamo unaopinga sera ya serikali, unaoakisi hali ya hofu nchini.

Kuna madai mengi kwamba mamlaka hukandamiza upinzani. Ukosoaji ni pamoja na kutoka mashirika ya haki za binadamu, upinzani wa kisiasa, hata tathimini zilizofanywa na Ofisi ya Mambo ya Nje ya Uingereza wa hivi karibuni katika mwaka 2021.

Victoire Ingabire, kiongozi mkuu wa upinzani aliyewahi kufungwa jela kwa tuhuma za kutishia usalama wa taifa, ametumia kesi yake kudai kuwa wanaotafuta hifadhi wanapata mpango mbaya.

"Ni watu walioikimbia nchi yao, kwa sababu ya umaskini, kwa sababu ya vita, kwa sababu ya udikteta walio nao katika nchi yao," aliiambia BBC.

"Na watakuja katika nchi ambayo watakabiliwa na matatizo sawa, ambapo hawawezi kuwa na uhuru wa kujieleza , ambapo hawatakuwa na ustawi wanaotafuta nchini Uingereza.

"Sielewi kwa nini serikali ya Uingereza inataka kabisa kuwapeleka watu hawa Rwanda." Serikali ya Rwanda inakanusha vikali madai haya.

Na bunge lake limepitisha sheria ya kushughulikia maswala ya Mahakama ya Juu ya Uingereza. Hii ilihusisha kuidhinishwa kwa mkataba wa hivi majuzi na Uingereza wa kuimarisha ulinzi kwa wanaotafuta hifadhi, ikiwa ni pamoja na hakikisho kwamba hawatarejeshwa katika nchi walizokimbia.

Nilimuuliza afisa mkuu anayesimamia mpango huo wa Uingereza, Doris Uwiceza Picard, kuhusu ikiwa wahamiaji wataweza kuikosoa serikali na kufanya maandamano kama watataka.

"Sheria zetu za kitaifa ziko wazi sana kuhusu haki ya kuandamana, inalindwa chini ya mazingira maalumu," alisema.

"Ikiwa wanataka kuandamana kwa amani ndani ya mipaka ya kisheria, wanakaribishwa."

Lakini, aliongeza kuwa, "lazima ukumbuke kwamba wakimbizi kwa ujumla, na kuhusiana na shughuli za kisiasa za wakimbizi, wamewekewa vikwazo na Mkataba wa Wakimbizi".

Rwanda imekaribisha watu wengine wanaotafuta hifadhi, na mara nyingi huonesha kituo cha muda cha hifadhi cha muda cha wakimbizi kilichopo kusini mwa Kigali kama uthibitisho kwamba inaweza kuwatunza vizuri sana.

Hii ni kambi ambayo inawahifadhi Waafrika waliokuwa wamekwama nchini Libya, wakijaribu kufika Ulaya, na inasimamiwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi.

Ni kimbilio la muda kwa watu walio katika mazingira magumu huku wakipanga hatua zinazofuata. Wangeweza kuchagua kuishi Rwanda. Hakuna, anasema meneja wa kambi hiyo, Fares Ruyumbu.

'Siwezi kupata kazi hapa'

Daniel Diew anashukuru kuwa hapa baada ya matukio ya kuhuzunisha. Ni kijana mrefu mwembamba kutoka Sudan Kusini akiwa na kaka na dada 11, na aliondoka kijijini kwao kutafuta kazi ili asaidie kutunza familia.

Bw Diew alijaribu mara saba kuvuka bahari kutoka Libya hadi Italia, na anasema aliwekwa gerezani kila mara aliporudishwa.

Ana malengo yake kuu la kwenda Amerika Kaskazini sasa.

"Sina uwezo wa kupata kazi hapa," anasema.

"Hakuna kazi nyingi kama ninavyoona kwa sababu nimekaa miezi mitano hapa. Lakini kila mara huwa naomba sana kupata nafasi ya kuondoka Rwanda."

Nilimuuliza angehisi vipi kama angeletwa huku baada ya kufika Ulaya, alishusha pumzi nzito na kusema ni matumaini yangu Mungu atamlinda na hilo.

Kwa wahamiaji katika kituo cha muda cha wanaoomba hifadhi, na kwa wale ambao bado wanakuja, nia yao ni kutafuta maisha bora ya baadaye. Je, Rwanda itakuwa njia ya mzunguko wa safari ndefu kwao, mwisho au makazi mapya?