Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Quds: Jinsi kikosi hiki cha Iran kinachoogopwa kinavyofanya kazi
Shambulio dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus Jumatatu hii, ambalo serikali kadhaa zinadai kuwa linafanywa na Israel, limesababisha vifo vya watu saba, akiwemo mwanajeshi muhimu katika utawala wa Ayatollah.
Huyu ni Mohamed Reza Zahedi, Brigedia Jenerali mwenye umri wa miaka 63 na historia ndefu ya utumishi katika IRGC (Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu), jeshi lenye nguvu sambamba la Iran na kubwa zaidi ndani ya vikosi vyake vya kijeshi.
Zahedi alikuwa kamanda mkuu wa Kikosi cha Quds, kikosi cha askari Walinzi wa Mapinduzi kinachosimamia uhusiano na serikali na vikundi vinavyofungamana na Tehran.
Alikufa pamoja na naibu wake, Jenerali Mohamed Hadi Haji-Rahimi, katika shambulio la kushtukiza ambalo ndege za Israel kutoka Miinuko ya Golan, kulingana na Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria, zilifanya shambulizi kwenye ubalozi mdogo wa Iran katika wilaya ya Mezzeh huko Damascus.
Shambulio hilo liliharibu jengo la ghorofa nyingi karibu na ubalozi wa Iran, ambo haukuharibiwa.
Jenerali aliyeuawa alikuwa kamanda wa Kikosi cha Quds huko Syria na Lebanon, ambapo alichukua nafasi muhimu katika kutoa msaada wa kijeshi kwa utawala wa Bashar al Assad na shirika la kisiasa na kijeshi la Hezbollah.
Tunachambua jinsi shirika hili linaloogopwa linavyofanya kazi na jukumu la Zahedi lilikuwa nini.
Sera muhimu ya mambo ya nje ya Iran
Kikosi cha Quds ni chombo muhimu cha sera za kigeni za Iran ambacho wataalamu wengi wanakielezea kuwa ni mchanganyiko wa vikosi maalum vya operesheni na Shirika la Kijasusi la CIA.
Iliibuka kama tawi la mambo ya nje wakati wa upanuzi wa IRGC.
Jina lake linamaanisha Yerusalemu kwa Kiajemi na Kiarabu, jiji ambalo wapiganaji wake waliahidi "kukomboa."
Shirika linafanya kazi kwa siri na wakati mwingine kwa uwazi katika sehemu mbalimbali za dunia.
Inahusishwa na kundi la Hezbollah nchini Lebanon na wanamgambo wa Kishia nchini Iraq na Afghanistan.
Kikosi cha Quds kimesifiwa kwa kusimamia mashambulio kadhaa mabaya, kama vile shambulio katika kambi ya kijeshi ya Beirut mwaka 1983 ambapo wanajeshi 241 wa Marekani, wanajeshi 58 wa Ufaransa na raia 6 wa Lebanon waliuawa.
Marekani na Umoja wa Ulaya (EU) zimeishutumu kwa kusambaza silaha nchini Syria kusaidia utawala wa Bashar al Assad kuwakandamiza waasi katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Washington pia imewataja kuwa na jukumu la kuwapa silaha na kuwafunza Taliban katika Mashariki ya Kati.
Shirika hili linalenga katika kusaidia na kushauri badala ya kushiriki moja kwa moja katika uvamizi wa kijeshi.
Hii inaruhusu Iran kukataa kuhusika katika shughuli za kijeshi na waasi, kuepuka migogoro ya moja kwa moja na Marekani.
Kati ya wanajeshi 5,000 na 10,000
Kwa sababu ya jinsi inavyofanya kazi, haiwezekani kupata idadi kamili ya idadi ya wanajeshi wake. Hata hivyo, kuna makadirio ya kuanzia wanajeshi 5,000 hadi zaidi ya 10,000.
Wanaajiriwa kulingana na ujuzi wao na kwa kiwango cha uaminifu wao kwa Jamhuri ya Kiislamu.
Lakini kwa vile kazi kuu ya Kikosi cha Quds ni kusaidia kuanzisha wanamgambo washirika na vikosi vya kupambana katika nchi nyingine, idadi ya wanajeshi hao haiakisi uwezo wake mkubwa wa ushawishi.
Tangu mwaka 1979, lengo lake limekuwa ni kupambana na maadui wa Iran na kupanua ushawishi wa nchi katika eneo.
Ili kujaribu kukabiliana na nguvu yake inayokua, utawala wa Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump uliteua kitengo hiki cha kijeshi kama Shirika la Kigeni la Kigaidi (FTO).
Serikali ya Iran kwa upande wake imekanusha mara kadhaa kuunga mkono mashirika ya kihalifu na kuishutumu Marekani kwa kuhusika na machafuko yanayoitikisa Mashariki ya Kati hivi sasa.
Mnamo Januari 2020, Merekani ilimuua kamanda mkuu wa Kikosi cha Quds, Meja Jenerali wa Irani Qasem Soleimani, katika shambulio lililolengwa la ndege isiyo na rubani.
Mauaji ya Soleimani yalikuwa ni pigo kubwa kwa utawala wa Ayatullah Ali Khamenei, ambao ulijibu mashambulizi dhidi ya kambi za Marekani katika nchi jirani ya Iraq, na hivyo kuibua mvutano wa kijeshi kati ya nchi hizo mbili.
Nafasi ya Soleimani ilichukuliwa na Brigedia Jenerali Esmail Qaani, 66, ambaye ni kiongozi wa sasa wa Kikosi cha Quds.
Mohamed Reza Zahedi
Mauaji ya Zahedi ni ya juu kabisa katika Kikosi cha Quds na Walinzi wa Mapinduzi tangu yale ya Soleimani mnamo 2020.
Jenerali huyo mwenye umri wa miaka 63 alichukua nafasi muhimu katika kuwa mpatanishi mkuu kati ya Iran na Hezbollah, shirika la kisiasa na kijeshi la Lebanon lililochukuliwa kuwa la kigaidi na Umoja wa Ulaya, Marekani na sehemu ya jumuiya ya kimataifa.
Alizaliwa Novemba 2, 1960, alijiunga na Walinzi wa Mapinduzi mwaka 1980 wakati wa vita vya Iran-Iraq (1980-88), ambako alishiriki kikamilifu.
Aliongoza Kitengo cha 44 cha Qamar Bani Hashem kati ya 1983 na 1986, na Kitengo cha 14 cha Imam Hussein hadi 1991.
Kati ya 1998 na 2002 aliongoza Kikosi cha Quds kwa Lebanon kwa mara ya kwanza, ambapo alitoa kila aina ya misaada kwa Hizbullah.
Baadaye, kati ya 2005 na 2008, aliongoza vikosi vya ardhini vya IRGC na aliwajibika kwenye kituo cha Thar-Allah huko Tehran, akisimamia usalama katika mji mkuu wa Iran.
Mnamo 2008, Zahedi alijiunga tena na Kikosi cha Quds na, hadi alipouawa Jumatatu hii, alikuwa msimamizi wa shirika hili la Syria na Lebanon.
Kulingana na wataalamu, alikuwa na jukumu muhimu katika kuipatia Hezbollah silaha na utaalamu wa kiufundi, pamoja na kuratibu operesheni dhidi ya vikosi vya Israel kusini mwa Lebanon.
Aidha, aliratibu usaidizi wa kijeshi ambao mkono wa kigeni wa jeshi la Iran hutoa kwa utawala wa Bashar al Assad na akaongoza IRGC Unit 18000, ambayo inafanya kazi nchini Syria kwa ushirikiano na jeshi la ndani kusafirisha silaha, risasi na zana za kijeshi.
Tangu 2010, Zahedi alikuwa kwenye orodha ya magaidi na wafadhili wao waliowekewa vikwazo na Idara ya Hazina ya Marekani kwa kufanya kazi kama "uhusiano na Hezbollah na huduma za ujasusi za Syria" na "kuhakikisha usafirishaji wa silaha" kwa shirika la Kiislamu lenye itikadi kali nchini Lebanon. .