Uchunguzi wa kufichua mbinu zinazotumiwa na walanguzi wa binadamu

A BBC undercover reporter speaks to a people smuggler
    • Author, Na Reha Kansara, Samrah Fatima & Jasmin Dyer
    • Nafasi, BBC Trending, BBC Urdu & BBC Newsnight

"Usiwe na wasi wasi. Iwe wana umri wa miaka 12 au 18, tunachukua watu wa umri huu pia."

Mlanguzi wa watu huko Quetta, ambaye hupanga njia haramu kutoka Pakistan, anaelezea mtindo wake wa biashara kwa mwandishi wa habari wa BBC. Kwa rupia za Pakistani milioni 2.5 ($9000; £7,500), kijana anaweza kufika Ulaya "salama na mzima" katika takriban wiki tatu, anasema, kwa kuvuka mpaka na kuingia Iran kwa miguu na kisha kusafiri kwa barabara kupitia Uturuki hadi Italia. Sauti yake inatoa taswira ya uhakika.

"Anapaswa kubeba vitafunio. Kwa hakika anapaswa kubeba viatu vilivyo bora , na seti mbili au tatu za nguo. Ndivyo hivyo. Anaweza kununua maji kutoka Quetta. Atapiga simu akifika Quetta na kuna mtu atakayekuja kumpokea '

Msafirishaji haramu wa watu - Azam - anadai mamia ya wahamiaji huvuka mpaka wa Pakistan na kuingia Iran kila siku. Anapuuza hatari iliyopo kwa ripota wetu, ambaye anajifanya kama mtu anayetaka kumleta kaka yake nchini Uingereza.

Huku mfumuko wa bei ukiongezeka nchini na Rupia ya Pakistani ikishuka thamani, watu wengi wanatazamia kuhama. Mamlaka ya Pakistani imeiambia BBC karibu watu 13,000 waliondoka Pakistani kwenda Libya au Misri katika miezi sita ya kwanza ya 2023, ikilinganishwa na karibu 7,000 katika mwaka mzima wa 2022.

Mara nyingi, safari wanazofanya ni hatari. Mnamo Juni, mamia ya wahamiaji walikufa baada ya meli iliyojaa ya watu ya uvuvi kuzama katika pwani ya Ugiriki. Takriban Wapakistani 350 walidhaniwa kuwa ndani ya meli hiyo.

"Hata akikamatwa [njiani], ataishia tu nyumbani. Hakuna mtu wa kumteka na kuomba fidia," Azam inasema.

Lakini wahamiaji wanaojaribu kusafiri kupitia Libya wanaweza kuwa mateka wa wanamgambo na magenge ya wahalifu. Mwanamume mmoja wa Pakistani tuliyezungumza naye, ambaye alitumia mlanguzi wa watu kusafiri hadi Italia, anasema alitekwa nyara na kufungwa kwa miezi mitatu nchini Libya.

Saeed (sio jina lake halisi) anasema aliachiliwa tu baada ya familia yake kulipa fidia ya $2,500 (£2,000).

Saeed says his family paid a ransom for his release in Libya
Maelezo ya picha, Saeed anasema alikamatwa nchini Libya alipokuwa akijaribu kuelekea Ulaya

'Nitumie ujumbe kwa mchezo'

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Walanguzi wengi wa watu wanafanya kazi bila kuonekana kwenye majukwaa ya kawaida ya mitandao ya kijamii kama vile Facebook na Tik Tok - kupitia akaunti ambazo zina makumi ya maelfu ya wafuasi.

Tangu Mei, BBC imekuwa ikifuatilia akaunti za mitandao ya kijamii zinazotangaza njia haramu za uhamiaji. Tuligundua kuwa mbinu za wasafirishaji haramu zimefichwa na mtandao wa maneno fiche ambayo huwawezesha kukwepa udhibiti wa maudhui na utekelezaji wa sheria. Wanapanga safari na malipo kwa faragha kupitia ujumbe wa moja kwa moja na WhatsApp.

Maneno ya msimbo kama vile "dunki" na "mchezo" hutumiwa kukuza njia haramu za kwenda Uropa. "Dunki" inamaanisha kuvuka kwa mashua na "mchezo" unaelezea safari ambazo wahamiaji watachukua kuanzia mwanzo hadi mwisho.

Njia tatu za kawaida kutoka Pakistani hupitia Uturuki, Iran au Libya kabla ya kufika mwisho wa mwisho wa Ulaya.

Baada ya maafa ya boti ya wahamiaji wa Ugiriki, wasafirishaji haramu wa watu tuliowafuatilia wamekuwa wakitangaza zaidi "michezo ya teksi" - njia fupi ya njia za barabara kupitia Ulaya Mashariki - kama njia inayopendekezwa ya magendo.

Akaunti za mitandao ya kijamii za wasafirishaji haramu huchapisha video za vikundi vya wahamiaji waliojificha msituni na kukimbilia kwenye gari dogo, huku majina ya mawakala na nambari za simu za rununu zikiwa juu. Kwenye WhatsApp, wateja na "mawakala" hubadilishana ujumbe kuhusu "mchezo" unaofuata katika gumzo la kikundi na mamia ya wanachama.

Azam amebobea katika "michezo ya teksi", akidai ni salama kuliko njia za baharini. Lakini kuna hatari kwa njia hizo za ardhini pia.

UNHCR inasema hali ya baridi kali wakati wa baridi huku wahamiaji wakijaribu kuvuka mipaka kwa miguu, pamoja na ajali za barabarani, zimesababisha vifo.

Safari ya Saeed kwenda Italia

TH

Wasafirishaji wengine watano tuliozungumza nao pia walipendekeza "njia za teksi". Mmoja alisema angeweza kumfikisha mtu Uingereza kutoka Ufaransa kwa £1,000 ($1,228).

Tuliwasilisha ushahidi wetu kwa Meta, ambayo inamiliki Facebook na Whatsapp, na TikTok - kwamba majukwaa yao yanatumiwa kusafirisha watu kwa njia haramu .

Meta iliondoa viungo vyote vya vikundi vya Facebook na kurasa tulizowapa , lakini haikushusha wasifu ulioambatishwa kwao. Haikuondoa vikundi vya WhatsApp, kwa sababu sera yake ya usimbaji fiche kutoka mwisho hadi mwisho inalinda faragha na hairuhusu udhibiti.

TikTok iliondoa viungo vya akaunti tulizowaarifu. Inasema kampuni "haina uvumilivu kabisa kwa maudhui ambayo yanawezesha ulanguzi wa binadamu" na "kuondoa akaunti na maudhui ambayo yanakiuka sera zao".

Saeed is now in Italy
Maelezo ya picha, Sasa Saeed yuko Italia

'Safari ya mauti'

TH

Saeed aliondoka katika mji wake katika Kashmir inayotawaliwa na Pakistan karibu mwaka mmoja uliopita kwa sababu ya ukosefu wa fursa za ajira kwa vijana wa kiume katika eneo lake - na mapigano kwenye mpaka na Kashmir inayotawaliwa na India. Aliishi karibu sana na Mstari wa Udhibiti - mpaka wa ukweli kati ya India na Pakistan katika eneo linalozozaniwa - lakini amekuwa Italia kwa miezi 10.

Anasema alishawishiwa kuja Ulaya na mseto wa video za TikTok alizoziona mtandaoni na rafiki yake ambaye aliondoka Pakistan miezi michache kabla yake.

"Nilisikia kwamba ni rahisi sana kuja hapa na ingechukua takriban siku 15-20. Lakini yote yalikuwa uongo. Ilinichukua zaidi ya miezi saba," anasema.

Saeed anasubiri matokeo ya madai yake ya hifadhi nchini Italia na anasema sasa anajuta kufanya safari h hiyo haramu, akiiita "safari ya kifo". Lakini mara kwa mara anachapisha video kwenye TikTok za maisha yake mapya nchini Italia.

Klipu chache huonyesja njia yake kutoka Pakistani, nyingi zikimuonyesha kijana mwenye furaha katika safari yake. Video hizi za kusisimua zinafuata mtindo wa TikTok ambao vijana wengi wa Pakistani kama yeye, wanaofika Ulaya, wameshiriki.

Katika video moja iliyoitwa "Pakistan hadi Libya", rafiki ambaye alisafiri nao anawapiga picha wote wawili, mtindo wa selfie, akiwa ameketi kwenye ndege, akitabasamu.

Anasema kwamba "ni aina tu ya sanaa" kuchapisha video kama hii na anasema "sio uhalisia wa kinachofanyika katika jamii".

Wiki mbili baada ya mwanahabari wetu wa siri kuwasiliana kwa mara ya kwanza na mlanguzi huyo, tunampigia tena simu - wakati huu tukifichua kuwa sisi ni waandishi wa BBC.

Tunapomhoji Azam kuhusu hatari ya njia haramu anazozitangaza, anakata simu.