Mwanaume aliyekaa miaka 38 gerezani Marekani na kufa kwa kosa ambalo hakufanya

“Mimi sina hatia.”
Kwa miaka 38, Mwingereza Krishna Maharaj alisema kauli hiyo mahakamani, kwa vyombo vya habari na kwa mawakili wake.
Muda wote huo alikuwa gerezani katika jimbo la Florida, nchini Marekani, baada ya kukutwa na hatia ya mauaji ya wanaume wawili yaliyotokea Miami mwaka 1986.
Ingawa hakimu alikubali kwamba hana hatia, kwa uhalifu uliofanywa na wanachama wa genge la Medellín linaloongozwa na Pablo Escobar, lakini Maharaj hakuweza kupata uhuru wake.
Tarehe 5 Agosti, akiwa na umri wa miaka 85, Maharaj aliaga dunia katika hospitali ya gereza alikokuwa amelazwa.
“Waliponihukumu kifo, hiyo ndio ilikuwa hukumu yangu ya kwanza, nilianguka kwenye sakafu ya chumba cha mahakama. Sikuamini kuwa nimehukumiwa kwa uhalifu ambao sikuujua, ambao sikuwahi kuufanya," anasema Maharaj katika mahojiano ya BBC ya mwaka 2019.
Wakili wa Maharaj, Clive Stafford Smith, aliweza kubadilisha hukumu ya kifo kuwa kifungo cha maisha, na kisha alifanikiwa kuifanya mahakama iamue Maharaj hahusiki na vifo ambavyo alihukumiwa kwavyo.
Hata hivyo, hakuweza kabisa kumtoa jela.
"Mahakama ilisema kuna ushahidi wa kutosha unaoonyesha Maharaj hana hatia, lakini haukutosha kumwachia huru," Stafford aliliambia gazeti la Uingereza la The Guardian.
Kwa sasa mke wa Maharaj, Bi Marita na Stafford wanafanya maandalizi ya mwili wake kurejea katika nchi yake ya asili.
Mauaji huko Miami

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Oktoba 16, 1986, raia wa Jamaica Derrick Moo Young na mwanawe Duane walikutwa wamefariki katika chumba katika Hoteli ya DuPont Plaza huko Miami.
Miili yote ilikuwa na majeraha ya risasi. Uchunguzi ulianza ambao ulipelekea Kris Maharaj kufunguliwa mashitaka.
Maharaj, Muingereza mwenye asili ya India, aliyekuwa milionea kutokana na biashara ya kuagiza ndizi, alikuwa na mzozo wa kibiashara na Moo Young.
Kulingana na taarifa za polisi, Maharaj alipanga kukutana na Moo Young katika moja ya vyumba vya hoteli. Kwa mujibu wa shuhuda mmoja, wakiwa ndani ya chumba, Maharaj alimpiga risasi Moo Young na mwanawe.
Sababu inashukiwa kuwa ni mabishano juu ya pesa ambazo Moo Young alikuwa amechukua kwa njia ya ulaghai kutoka kwa baadhi ya jamaa wa Maharaj katika kisiwa cha Trinidad na Maharaj alitaka azirudishe.
Maharaj alikamatwa, akashtakiwa kwa mauaji ya watu wawili, na chini ya mwaka mmoja tu, alihukumiwa kifo kwa mauaji hayo.
“Sikuwepo kwenye hoteli. Na watu sita walisema siku hiyo nilikuwa mahali pengine zaidi ya kilomita 30 kutoka hotelini. Sikuamini kuwa walinitia hatiani," Maharaj aliiambia BBC 2019.
Kwa miaka sita, licha ya majaribio ya mfungwa huyo kuthibitisha kutokuwa na hatia na kuepuka hukumu ya kifo, hakuna kilichobadilika. Hadi 1993, Stafford, mwanasheria wa haki za binadamu, aliamua kuchukua kesi hiyo.
Nani waliohusika?

Chanzo cha picha, Reuters
Jambo la kwanza alilofanya Stafford ni kukata rufaa ili hukumu ya kifo ibadilishwe na kuwa kifungo cha maisha, jambo ambalo alifanikiwa mwaka 2002. Kisha alijikita katika kuthibitisha kutokuwa na hatia kwa Maharaj.
Uhalifu huo ulitokea katika miaka ya 1980, wakati ulanguzi wa madawa ya kulevya umeshamiri huko Miami; ndani ya mfumo wa vita vya siri kati ya makampuni ya Colombia na wafanyabiashara wa madawa ya kulevya wa Cuba.
Stafford alipata ushahidi kwamba Moo Young alikuwa anahusika na ulanguzi wa dawa za kulevya na mauaji yake akaelezwa yalitekelezwa na wanachama wa genge la Medellín.
Kimsingi, mauaji hayo yaliagizwa na Pablo Escobar na wafuasi wake walitekeleza hilo.
"Nilisafiri hadi Medellín kuwatafuta wanachama wa zamani wa genge ambao walikuwa bado hai, kutoa ushahidi katika kesi hiyo na walisema Maharaj hakuwa na uhusiano wowote na uhalifu huo," Stafford aliiambia BBC.
Kwa miaka kadhaa, wakili huyo alitafuta njia ya kufungua kesi mpya ya Maharaj, akitumia ushahidi wote uliokusanywa ambao ulionyesha kulikuwa na watu wengine waliokuwa na nia ya kumuua Moo Young na zaidi ya yote, mashahidi sita ambao walithibitisha alikuwa mbali sana na sehemu yalipotokea mauaji.
Lakini ombi lolote la kuhurumiwa au kujaribu kukata rufaa, lilkataliwa.
"Serikali ya shirikisho haikuwa tayari kusikiliza ushahidi na kushindwa kumwachilia mtu asiye na hatia ni jambo la kusikitisha," Stafford aliiambia BBC.
Ushuhuda

Chanzo cha picha, Getty Images
Novemba 2017, wakala wa zamani Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya (DEA), aliiambia mahakama, watu wanaohusishwa na Pablo Escobar walikaa katika moja ya vyumba kwenye Hoteli ya DuPont Plaza siku ya mauaji.
Kulingana na taarifa ya wakala huyo wa zamani, Escobar aliamuru Moo Young auawe kwa sababu alikuwa na pesa za shirika hilo na alizihalalisha kwa njia ya utakatishaji fedha.
Alisema habari hii aliipata kutoka kwa Jhon Jairo Velásquez, anayejulikana zaidi kwa jina la Popeye, ambaye aliachiliwa uhuru Agosti 2014 baada ya kutumikia kifungo cha miaka 23 jela.
Popeye alikuwa mmoja wa manaibu wakuu wa Escobar, na kwa mujibu wa ushahidi wa wakala huyo wa zamani, wazo lilikuwa ni kusafisha maadili yake na kufichua kwamba Maharaj alifungwa kimakosa.
Kwa ushahidi huo mpya, wenye nguvu zaidi kuliko ule aliokuwa ameupata hapo awali, mwaka 2019 baada ya miaka 33 tangu uhalifu huo kutendwa, wakili wake alipambana ili kesi ya Maharaj ipitiwe upya, ili kuthibitisha kutokuwa na hatia na kurudi nyumbani.
Mwaka huo huo, Jaji kutoka Mahakama ya Rufaa ya Marekani, alionyesha kwamba kulikuwa na vipengele vilivyothibitisha kutokuwa na hatia kwa Maharaj.
Hata hivyo, kesi ilipopelekwa katika Mahakama ya Rufaa ya Shirikisho, mahakama ya juu zaidi kwa ajili ya mchakato wa aina hii, iliamua uamuzi wa jaji haukutosha kumwachilia huru Maharaj.
Mkewe Marita Maharaj, hakuacha kumtembelea kwa miaka 38, alihamia Uingereza miaka michache iliyopita akiwa na wazo kwamba mumewe angehamishiwa katika gereza la Uingereza.
Lakini Agosti 5, baada ya matatizo kadhaa ya kiafya, Maharaj alifariki katika hospitali ya gereza alikokuwa amelazwa.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla












