Waridi wa BBC: Kifungo gerezani kilimsaidia kujiendeleza kimaisha

Chanzo cha picha, Emma Atieno
- Author, Anne Ngugi
- Nafasi, BBC Swahili
Sote tunajua kuwa maisha yanaweza kuwa magumu wakati mwingine, simulizi ya Emma Atieno ni mfano mzuri.
Mwanadada huyu alikulia katika mazingira ya umasikini na alipokuwa na umri wa kutosha kujitafutia riziki, haikuwa rahisi, ilibidi apambane kwa njia zote kujikimu kimaisha.
Mapambano yake pia yaliimarishwa na majukumu ya kuwa mama wa watoto wawili ambao anasema ndio ramani yake maishani.
Nini kilichomsukuma kuwa mchuuzi?

Chanzo cha picha, Emma Atieno
Kutokana na ugumu wa maisha na pia kuhakikisha kwamba anatosheleza mahitaji ya familia yake , Emma aliamua kuanza kuuza peremende mitaani katika hali ya kupiga jeki maisha yake. Alifanya kazi za uchuuzi katika mitaa mbalimbali jijini Nairobi nchini Kenya, lakini kwa bahati mbaya, biashara yake ndogo ilidumu kwa muda mfupi alipokamatwa kwa kosa la kuwa mchuuzi bila kibali au leseni ya uchuuzi .
Alifungwa katika Gereza la Wanawake la Lang'ata baada ya kuambiwa alipe faini ya dola 100 au asalie rumande kwa miezi mitatu.
Haikuwa rahisi anasema , japo alikaa gerezani kwa muda wa wiki moja na siku 3, hatua iliyotosha kumfungua macho na anasema kwamba kamwe hawezi kusahau .
Baadhi ya mambo ambayo yalimtia hofu ni kile anachotaja kutokuwa na ruhusa ya kuvaa nguo za ndani, ni sare za jela tu na si kitu kingine. Wakati ambao waliruhusiwa kuvaa ni wakati wa hedhi.
Kazi ngumu gerezani

Chanzo cha picha, Emma Atieno
Kazi ya mikono ya kila siku ilikuwa ngumu sana kwake kwani hakuizoea. Hapo ndipo madhara ya kufungwa gerezani yalipoanza kumuingia.
Kwa bahati nzuri, rafiki yake aliweza kupata faini yake ya Ksh 10,000 au dolla mia moja , ambayo ilimnusuru kutumikia kifungo cha miezi 3. Ijapokuwa hatimaye Emma aliunganishwa tena na watoto wake, bado alikuwa akihangaika kutafuta riziki na aliogopa kurudi kwenye uchuuzi na pengine kukamatwa na kuishia gerezani tena
Japo hakukaa gerezani kwa muda mrefu kama wafungwa wanawake wengi , anasema kwamba muda huo mfupi ulijaa mafunzo tele , na ulimpa fursa ya kujitathmini alipokuwa maishani na kufikiria njia nyingine ambazo zingemsaidia kuweka chakula mezani pindi atakapotoka jela .
Afueni yake ilijiri baada ya kutoka jela ,alifahamishwa kuhusu shirika la Clean Start Africa kutoka kwa rafiki yake mmoja , ambaye urafiki wake ulianzishwa wakiwa gerezani pamoja. Bado alikuwa akihangaika kutafuta riziki . Emma anasema kwamba ushirikiano wa shirika hilo ulizalisha ndoto na ari mpya ya maisha yake baada ya jela .
Alichojifunza gerezani

Chanzo cha picha, Emma Atieno
Alijiandikisha katika darasa la mafunzo ya useremala , moja wapo wa kazi ambazo wanawake wengi hawasikiki wala kuhusika kutokana na kwamba ni wanaume ambao wanafahamika sana kuwa fundi wa mbao .
Sasa yeye ni seremala mwenye fahari na anajivunia sana kwa kuweza kubadilisha maisha yake kwa fursa aliyopewa.
Fahari yake ya kuwa na mahali pa kufanyia kazi kila siku, akiwa na zana zake za biashara ni moja ambayo anajivunia kila siku
Ujuzi wake umeboresha maisha yake mapya . Tabasamu lake ni lile la mwanamke jasiri anayejenga mustakabali wake na asiyefungwa tena na umaskini.












