Vita vya Ukraine: Urusi kufunga bomba muhimu la gesi kwenda EU

Bomba la gesi la kutoka Urusi hadi Ujerumani halitafunguliwa tena kama ilivyopangwa Jumamosi, kampuni ya nishati ya serikali ya Gazprom imesema.

Kampuni hiyo ilisema imepata uvujaji wa mafuta kwenye bomba la Nord Stream 1, kumaanisha kuwa litafungwa kwa muda usiojulikana.

Bomba hilo limefungwa kwa muda wa siku tatu zilizopita kwa kile kampuni ya Gazprom ilielezea kama kuwezesha kufanyika kwa marekebisho.

Habari hizo zinawadia huku kukiwa na hofu kwamba familia katika Umoja wa Ulaya hazitaweza kumudu gharama ya kupasha joto msimu huu wa baridi.

Bei ya nishati imepanda tangu Urusi ilipovamia Ukraine na uhaba wa vifaa unaweza kuongeza gharama hata zaidi.

Ulaya inajaribu kujiondoa kutoka kwa utegemezi wa nishati ya Urusi katika juhudi za kupunguza uwezo wa Urusi kufadhili vita, lakini hali hiyo inawezekana isifikiwe kwa haraka.

Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel alisema hatua hiyo ya Urusi ‘’haijashangaza’’ kwa maana kwamba ni jambo ambalo lilitarajiwa.

‘’Matumizi ya gesi kama silaha hayatabadilisha azimio la EU. Tutaharakisha njia yetu kuelekea uhuru wa nishati. Wajibu wetu ni kulinda raia wetu na kuunga mkono uhuru wa Ukraine,’’ aliweka ujumbe kwenye Twitter.

Moscow inakanusha kutumia nishati kama silaha ya kiuchumi kulipiza kisasi vikwazo vya Magharibi vilivyowekwa kufuatia uvamizi wa Urusi.

Imelaumu vikwazo hivyo kwa kusimamisha matengenezo ya kawaida ya bomba la Nord Stream 1, lakini EU inasema hiki ni kisingizio.

Mdhibiti wa mtandao huo huko Ujerumani, Bundesnetzagentur, alisema nchi hiyo sasa imejiandaa vyema kwa usambazaji wa gesi ya Urusi kukoma lakini imewataka raia na kampuni kupunguza matumizi.

Tangazo la kampuni ya Gazprom linawadia muda mfupi baada ya mataifa ya G7 kukubaliana kupunguza bei ya mafuta ya Urusi ili kuunga mkono Ukraine.

Kundi la G7 linajumuisha Uingereza, Marekani, Kanada, Ufaransa, Ujerumani, Italia na Japan.

Kuanzisha kwao kwa ukomo wa bei kunamaanisha kuwa nchi zinazojiandikisha kwenye sera hiyo zitaruhusiwa kununua tu mafuta ya Urusi na bidhaa za petroli zinazosafirishwa kupitia bahari ambazo zinauzwa kwa bei ya chini au chini ya bei iliyowekwa.

Hata hivyo, Urusi inasema haitauza kwa nchi ambazo zitashiriki katika ukomo huo wa bei.

Bomba la gesi linaanzia pwani ya Urusi karibu na St Petersburg hadi kaskazini-mashariki mwa Ujerumani na linaweza kubeba hadi mita za ujazo milioni 170 za gesi kwa siku.

Inamilikiwa na kuendeshwa na kampuni ya Nord Stream AG, ambayo inahisa zake nyingi katika kampuni ya Gazprom.

Ujerumani pia hapo awali iliunga mkono ujenzi wa bomba sambamba – la Nord Stream 2 - lakini mradi huo ulisitishwa baada ya Urusi kuivamia Ukraine.

Kampuni ya Gazprom pia ilisema kuwa hitilafu hiyo iligunduliwa katika kituo cha kubana umeme cha Portovaya, na ukaguzi ulifanywa na wafanyakazi kutoka Siemens, kampuni ya Ujerumani inayodumisha mabomba.

Ilisema kuwa kurekebisha uvujaji wa mafuta katika injini muhimu kuliwezekana tu katika warsha maalum, ambazo zilizuiliwa na vikwazo vya Magharibi.

Hata hivyo, kampuni ya Siemens yenyewe ilisema: ‘’Uvujaji huo hauathiri kwa kawaida uendeshaji wa mabomba na unaweza kufungwa kwenye eneo. Ni utaratibu wa kawaida ndani ya upeo wa kazi ya marekebisho.’’

Hii si mara ya kwanza tangu uvamizi wa bomba la Nord Stream 1 kufungwa.

Mnamo mwezi Julai, kampuni ya Gazprom ilikata vifaa kabisa kwa siku 10, ikisema kuwa ni ‘’mapumziko ya kufanya marekebisho.’’

Ilianza tena usambazaji siku 10 baadaye, lakini kwa kiwango kilichopunguzwa sana.

Akizungumza na BBC kutoka mji mkuu wa Uswizi Bern, mwanauchumi na mchambuzi wa masuala ya nishati, Cornelia Meyer, alisema kuzimwa kwa gesi kutakuwa na athari kubwa katika ajira na bei.

‘’Hiyo kwa kweli ina madhara makubwa kwa gesi barani Ulaya ambayo ni ghali mara nne zaidi kuliko ilivyokuwa mwaka mmoja uliopita na gharama hii ya maisha itapanda sana kwa sababu sio gesi pekee,’’ alisema.

‘’Gesi inakuwa mbolea na inatumika katika michakato mingi ya viwanda, hivyo itaathiri ajira, na itaathiri gharama.’’