Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Muhoozi Kainerugaba: Kutoka ‘kumposa’ Waziri Mkuu wa Italia hadi kutishia kuivamia Kenya
Na Seif Abdalla
BBC Swahili
Mtoto mkubwa wa rais wa Uganda Yoweri Museveni ambaye pia ni kamanda wa jeshi la ardhini nchini humo Luteni Jenerali Muhoozi Kainerugaba, amekuwa akizua hisia kali kupitia machapisho yake katika mtandao wa Twitter. Kupitia machapisho yake ya kisiasa na yale ya kijamii, amevutia ufuasi mkubwa sana.
Kamanda huyo wa jeshi anadaiwa kuandaliwa kwa lengo la kumrithi baba yake atakapondoka uongozini na amekuwa akiishi chini ya kivuli cha rais huyo wa taifa hilo la Afrika Mashariki.
Muhoozi hatahivyo amekuwa maarufu miongoni mwa wafuasi wake 600,000 wa matandao wake wa Twitter kwa namna anavyoutumia. Ijapokuwa haijulikani iwapo ana msimamizi wa ukurasa wake au anausimamia mwenyewe, kitu kimoja ni kwamba takriban kila wiki chapisho lake litazua hisia.
Ni kutokana na hilo tunayaangazia machapisho ya kamanda huyo ambayo yamezua utata.
‘Kuiteka Nairobi kwa wiki mbili’
Tarehe tatu mwezi wa kumi mwaka 2022, ni siku ambayo bwana Muhoozi aliamua ‘kuwachokoza’ majirani zake wa Kenya kwa kudai kwamba jeshi lake lingeweza ‘kuiteka Nairobi baada ya wiki mbili tu’ huku akiwauliza wafuasi wake iwapo wangependelea “aishi katika eneo la Riverside au Westland.”
Kauli yake ilizua hisia mseto miongoni mwa wafuasi wa mtandao wa twitter nchini Kenya maarufu kama KOT ambao wengi walilitaka jeshi lake kwanza kumkamata kiongozi wa waasi na mbabe wa kivita Joseph Kony kabla ya kuiteka Kenya huku wengine wakimuunga mkono na kudai kwamba jeshi la Uganda lipo imara zaidi ya majeshi yote Afrika Mashariki.
Hatahivyo serikali ya Uganda baadaye ilitoa taarifa ikikana machapisho ya jenerali Muhoozi ikisema kuwa yalikuwa ya kibinafsi
Hatahivyo Muhozi baadaye alirudi katika akaunti yake na kusema hivi:
‘Kumposa’ waziri mkuu wa Itali
Siku cha tu kabla ya kuwachokoza Wakenya kuhusu kuuteka mji wao mkuu wa Nairobi, Muhoozi Kainerugaba aligonga vichwa vya habari baada ya kuuliza katika mtandao wake wa Twitter ni ng’ombe wangapi Waganda wangempatia waziri mkuu mpya wa Italia kama mahari huku akichapisha picha ya kiongozi huyo.
Kawaida kulingana na tamaduni za Kiganda na baadhi ya makabila ya Afrika, mwanamume anayemposa mchumba wake anapaswa kutoa ng’ombe kwa wazazi wake.
Chapisho hilo lilizua hisia miongoni mwa wapenzi wa mtandao wa Twitter
Baadaye Muhoozi alirudi na kusema kwamba angempatia ngombe 100 za Nkore kwa kuwa jasiri na mtu mkweli.
Kuliunga mkono jeshi la Tigray la TPLF
Machapisho ya Twitter ya kamanda wa jeshi la ardhini nchini Uganda Luteni jenerali Mohoozi Kainerugaba yaliounga mkono waasi wa Tigray huku akiishutumu serikali ya Ethiopia kwa ukiukaji wa haki za kibinadamu mwezi Julai mwaka huu yalizua mzozo wa kidiplomasia kati ya Uganda na serikali ya Ethiopia.
Hali hiyo iliilazimu serikali ya Uganda kupitia msemaji wake wa jeshi kusema kwamba kauli iliyotolewa na kamanda huyo wa jeshi yalikuwa yake ya binafsi na sio msimamo wa jeshi la Uganda.
Katika mahaojiano na BBC Focus on Africa TV, msemaji wa jeshi Brigedia Felix Kulagigye alisema kwamba: “Nina ufahamu wa kila kitu kinachofanyika katika jeshi, na kama umegundua, ujumbe huo wa Twitter haukutoka kutoka kwa kamanda mkuu wa jeshi la Uganda UPDF wala msemaji wa wizara ya Ulinzi. Hivyobasi hauwezi kuwa msimamo wetu rasmi.”
Wakati huo kulikuwa na uvumi ulionea kwamba Uganda ilikuwa ikiwafunza wapiganaji wa TPLF.
Kustaafu katika Jeshi
Ilikuwa tarehe nane mwezi Machi mwaka huu wakati Jenerali Kainerugaba alipoangusha ‘bomu’ jingine katika mtandao wa Twitter.
Aliandiaka katika ujumbe wake wa twitter: ''Baada ya kuhudumu kwa miaka 28 katika jeshi letu , jeshi bora zaidi duniani , nafurahia kutangaza kwamba ninastaafu.
Mimi na wanajeshi wangu tumefanikiwa pakubwa , ninawapenda na kuwaheshimu maafisa wote waliofanikiwa kila siku '', alisema mtoto huyo wa rais wa Uganda Yoweri Museveni katika mtandao wake wa twitter.
Chapisho lake lilizua hisia kali miongoni mwa wapenzi wa Twitter
Hatahivyo licha ya chapisho hilo Muhoozi Kainerugaba ameendelea kuwa kamanda wa jeshi la ardhini nchini Uganda hadi leo.
'Kutishia usalama wa kikanda
Machapisho ya bwana Muhoozi hatahivyo hayakuisha hapo.
Mnamo tarehe 14 Juni, 2022 spika wa Bunge la DRC, Christophe Mboso, alifichua kuwa wajumbe walikataa kuridhia mkataba ambao serikali ilitia saini na Uganda kwa ajili ya ujenzi wa barabara za mpakani kulingana na jarida la Afrika Report. Mboso alisema Muhoozi ameisaliti DRC kwa kusaini mkataba na Kagame.
"Tulisema kwamba kufuatia mkataba aliosaini na Rwanda, hatutaruhusu mkataba huu upite," Mboso alisema. "Ametusaliti tu."
Lakini hakukuwa na mkataba wowote ambao Muhoozi alikuwa ametia saini na Kagame kwa niaba ya Uganda.
Alichokuwa akisisitiza Mboso ni msururu wa jumbe za twitter kutoka kwa Muhoozi akiahidi kuwa atampigania ‘mjomba’ wake Kagame wakati ambapo Kinshasa ilikuwa ikitoa kauli za hasira ikiishutumu Kigali kwa kuiyumbisha kwa kuunga mkono M23. Rwanda imekana kuunga mkono kijeshi waasi hao wa M23.
Hata hivyo baadaye wizara ya mambo ya nje ya Uganda ilijitenga na kauli za mtoto huyo wa rais.