Tunajua kuhusu tetemeko la ardhi Morocco kufikia sasa

tt

Chanzo cha picha, Getty Images

Tetemeko la ardhi limeikumba Morocco, na kusababisha mamia ya vifo na majeruhi. Katika taarifa hii tunaangazia kile tunachojua kufikia sasa.

Nini kimetokea Morocco?

Tetemeko la ardhi lilikumba eneo la katikati mwa Morocco na kuua zaidi ya watu 800, na zaidi ya 650 kujeruhiwa. Inahofiwa idadi vijiji vya mbali vimeathiriwa vibaya na ni kubaini ukubwa wa maafa

Tetemeko hilo, lililotokea saa tano na dakika kumi na moja usiku wa Ijumaa (22:11 GMT), lilikuwa cha kipimo cha 6.8. Mitetemeko ya ukubwa wa 4.9 ulifuatia dakika 19 baadaye.

Tetemeko la ardhi lilipiga wapi?

Kitovu hicho kilikuwa katika eneo lenye watu wachache la Milima ya Juu ya Atlas, 71km (maili 44) kusini-magharibi mwa Marrakesh, kivutio kikuu cha watalii.

Baadhi ya waathiriwa wanadhaniwa walikuwa katika maeneo ya mbali, na vifo vimethibitishwa katika majimbo na manispaa ya Marrakesh, al-Haous, Ouarzazate, Azilal, Chichaoua na Taroudant.

Watu pia wanahofiwa kunanaswa chini ya vifusi huko, huku familia moja ikisemekana kuwa chini vifusi vya nyumba yao katika mji wa Al-Haous, karibu na kitovu hicho.

Pia kuna ripoti za watu kufukiwa chini ya vifusi katika mji wa kihistoria wa Marrakesh na uharibifu wa sehemu za Madina, eneo la Urithi wa Dunia wa Unesco.

Ramani

Walionusurika walisema nini?

Michael Bizet, ambaye alikuwa katika mji wa kale wa Marrakesh, alisema alifikiri kitanda chake "kingeruka". "Ilikuwa vurugu kamili, janga la kweli, wazimu," aliambia shirika la habari la AFP.

Fayssal Badour, anayeishi katika jiji hilo, alikuwa akiendesha gari wakati tetemeko hilo lilipotokea. "Nilisimama nikaanza kuwaza itakuaje," aliambia shirika la habari. "Sikujua nipige mayowe na kulia au nifanyeje."

Mina Metioui aliiambia BBC kelele hizo zilisikika kama "ndege ya kivita", ikiwa karibu na zaidi.

"Ilichukua sekunde ambayo ilionekana kama dakika," aliambia BBC News. "Kisha nikasikia watu wakipiga kelele, wakitoka nje ya nyumba zao ... ilikuwa mbaya sana

Je, Morocco imewahi kuwa na matetemeko mengi ya ardhi hapo awali?

Tetemeko kubwa la mwisho la ardhi katika nchi hiyo lilipiga mji wa kaskazini-mashariki wa Al Hoceima mnamo 2004, na kuua watu wasiopungua 628.

Na lililokuwa mbaya zaidi lilitokea huko Agadir kwenye pwani ya kusini ya Atlantiki, mwaka wa 1960. Tetemeko hilo la kipimo cha 6.7 lilisababisha vifo vya watu 12,000.

Ni nini kinachofanyika kwa sasa?

Juhudi za kutafuta manusura zinaendelea. Huenda ikuchukua muda kubainisha majeruhi katika vijiji vya mbali vya milimani karibu na kitovu cha tetemeko hilo.

Kuna uwezekano idadi ya vifo ikaongezeka huku juhudi za uokoaji zikiendelea.

Mamlaka imetoa wito kwa wakazi kuchangia damu kusaidia waliojeruhiwa.

Jamii ya kimataifa imesema nini

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza James Cleverly alisema: "Tuko tayari kusaidia marafiki zetu wa Morocco kwa njia yoyote tunayoweza." Alisema Uingereza inawasaidia raia wa Uingereza katika eneo hilo.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema "amesikitishwa" na nchi yake iko tayari kusaidia katika huduma ya kwanza.

Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sánchez alisema: "Tuko tayari kutoa na msaada kwa watu wa Morocco kutokana na tetemeko hili baya."

Narendra Modi wa India, akizungumza katika mkutano wa G20 mjini Delhi, alisema jumuiya ya kimataifa itaungana kusaidia Morocco.

Vladimir Putin alisema Urusi inasimama "na watu wa Morocco wakati huu mgumu".

Volodymyr Zelensky wa Ukraine alituma "rambi rambi" zake kwataifa la Morocco.