Wachezaji maarufu duniani waliokufa kwa ajali

    • Author, Abdalla Seif Dzungu
    • Nafasi, BBC Swahili
    • Akiripoti kutoka, Nairobi Kenya
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Ulimwengu wa kandanda umekumbwa na ajali nyingi mbaya za magari kwa miaka mingi, zikigharimu maisha ya vipaji vinavyoinuka na wataalamu waliobobea.

Hivi karibuni zaidi ni nyota wa kimataifa wa Ureno na Liverpool, Diogo Jota, ambaye alikufa pamoja na kaka yake katika ajali ya gari huko Uhispania, siku chache baada ya harusi yake.

Vifo hivi, mara nyingi huwa vya ghafla na vya kuhuzunisha, huacha athari ya kudumu kwa vilabu, mashabiki na mataifa.

Ifuatayo ni orodha ya wanasoka mashuhuri waliopoteza maisha katika ajali za barabarani na angani.

1.Emiliano Sala (Argentina, 2019)

Labda janga la kusikitisha zaidi la ajali ya anga katika soka ya kisasa lilikuwa la kifo cha mchezaji huyu aliyekuwa amejiunga na Cardiff City wakati ndege nyepesi iliyokuwa ikimbeba kutoka Ufaransa ilipoanguka.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 alikuwa anasafiri kwa kutumia ndege ya Piper Malibu ikiruka kutoka Nantes nchini Ufaransa kwenda Wales jioni ya Januari 21 2019 wakati ilipoanguka katika Mkondo wa bahari wa Uingereza karibu na Guernsey, pia na kumuua rubani David Ibbotson, 59, ambaye mwili wake haujawahi kupatikana.

Sala alikuwa akijiunga na klabu ya wakati huo ya Ligi ya Premia Cardiff City kwa uhamisho wa pauni milioni 15 kutoka Nantes ya Ligi Kuu ya Ufaransa, ambayo ilimhusisha wakala wa soka Willie McKay.

Kulingana na uchunguzi Sala alikuwa bado yuko hai wakati wa ajali hiyo na alikufa kutokana na majeraha mabaya ya kichwa na kifua.

2. Patrick Mutesa Mafisango {Rwanda 2012}

Patrick Mutesa Mafiosango alikuwa akiichezea klabu ya Simba Sports na timu ya taifa ya Rwanda.

Mchezaji huyo maarufu alifariki mwezi Mei tarehe 17 2012 kwa ajali ya gari iliotokea eneo la keko mjini Dar es Salaam ikiwa ni siku chache baada ya msimu wa ligi kuu Tanzania bara 2011/2012 ambapo Simba walitwaa ubingwa.

Hadi wakati mauti yake yamfike Mafisango alikuwa na umri wa miaka 32 na kabla ya kuitumikia Simba aliichezea timu za TP Mazembe , APR , Atraco na Azaam.

3. Antonio Reyes (Uhispania, 2019)

Winga huyo wa zamani wa Arsenal na Sevilla alifariki katika ajali ya gari la mwendo wa kasi katika mji aliozaliwa wa Utrera.

Ripoti zilisema kuwa gari lake aina ya Mercedes lilikuwa likiendeshwa kwa kasi ya 237 km/h (147 mph) kabla ya kukosa mwelekeo.

Reyes alikuwa na umri wa miaka 35 na alikuwa akisafiri na binamu wawili; mmoja wao pia alikufa.

4. Lesley Manyathela – Afrika Kusini, 2003

Mshambulizi nyota anayechipuka wa Orlando Pirates na Bafana, Manyathela alifariki akiwa na umri wa miaka 21 tu baada ya kufunga mabao 48 katika mechi 73 akiichezea klabu ya Buccaneers.

Manyathela alikuwa amerejea tu kutoka kwa majaribio barani Ulaya na kuifungia Pirates katika kichapo cha 2-1 kutoka kwa Jomo Cosmos kwenye Uwanja wa Rand Stadium, alipopata ajali akiwa njiani kuelekea mji wa Musina kutumia muda na mamake.

Akiwa mshindi wa Kiatu cha Dhahabu cha Premier Soccer League (PSL) akiisaidia kuiongoza Bucs kutwaa taji la 2002-03, alikuwa kwenye harakati ya kusaini na klabu ya Dynamo Kiev ya Ukraine. Tuzo ya mfungaji bora wa PSL ilipewa jina la Manyathela.

5. Laurie Cunningham

Winga huyo Mwingereza, ambaye aliweka historia ya kuwa mmoja wa wachezaji wa kwanza weusi kuiwakilisha Uingereza katika ngazi ya juu na pia alichezea Real Madrid na Manchester United, alifariki katika ajali ya gari nchini Uhispania Julai 1989.

Maisha yake ya soka yalikatizwa kwa huzuni akiwa na umri wa miaka 33 pekee.