Wanasiasa maarufu Tanzania walioaga dunia 2025

S

Chanzo cha picha, URT

Muda wa kusoma: Dakika 6

Mwaka 2025 umeacha pengo kubwa katika historia ya Tanzania kufuatia vifo vya wanasiasa wakubwa waliowahi kushika nyadhifa za juu serikalini na kuwa na ushawishi mkubwa katika taifa hilo.

Baadhi yao walikuwa sehemu ya kizazi cha waanzilishi wa sera za kiuchumi na kisiasa, huku wengine wakiwa viongozi wa kizazi cha sasa waliotoa mchango wao katika kipindi cha mageuzi ya kisiasa na kiutawala.

Viongozi hawa walihudumu katika nafasi mbalimbali ikiwemo uwaziri mkuu, usimamizi wa Bunge, diplomasia, usalama wa taifa na wizara muhimu za kijamii na kiuchumi.

Vifo vyao vimegusa siasa za Tanzania na kuibua mazungumzo mapya kuhusu urithi wao wa kisiasa na mchango wao katika kujenga taifa.

Cleopa Msuya - Waziri Mkuu wa zamani

S

Chanzo cha picha, URT

Cleopa David Msuya mmoja wa wanasiasa wakongwe na waheshimika zaidi katika historia ya Tanzania. Aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania mara mbili, (1980 -1983 na 1994 -1995, pamoja na kushika wizara nyeti kama Fedha, Viwanda na Biashara. Zamani cheo chake cha Waziri Mkuu kilenda sambamba na kuwa Makamu wa kwanza wa rais.

Alikuwa miongoni mwa wachumi waliounda sera za mageuzi ya kiuchumi kuanzia miaka ya 1980, wakati Tanzania ilipokuwa ikipitia mabadiliko makubwa ya mfumo wa uchumi.

Msuya alijulikana kwa unyenyekevu, busara na uwezo wa kufanya kazi na viongozi wa vizazi tofauti. Alikuwa mshauri muhimu wa marais kadhaa hata baada ya kustaafu siasa za moja kwa moja, na aliheshimika ndani na nje ya nchi.

Alifariki dunia mwaka 2025 nchini Tanzania baada ya kuugua kwa muda. Kifo chake kilionekana kama kufungwa kwa ukurasa muhimu wa kizazi cha viongozi wa mwanzo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Job Ndugai – Spika wa zamani wa Bunge

S

Chanzo cha picha, URT

Job Ndugai alikuwa Spika wa Bunge la Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Kongwa. Akiwa Spika, alisimamia vikao vya Bunge katika kipindi ambacho mijadala ya kisiasa ilikuwa mikali na yenye mgawanyiko mkubwa wa maoni.

Ndugai alitambulika kwa mtindo wake wa uendeshaji wa Bunge uliokuwa wa nidhamu na msimamo mkali. Kabla ya siasa, alikuwa mhandisi na mtumishi wa umma, jambo lililompa taswira ya kiongozi mwenye mtazamo wa kiutendaji.

Alifariki dunia Agosti mwaka 2025 baada ya kuugua kwa muda. Kifo chake kilizua mjadala mpana kuhusu urithi wake katika taasisi ya Bunge na demokrasia ya Tanzania.

Ndugai alihudumu katika nafasi ya Spika wa Bunge la Tanzania kwa miaka 6, kuanzia mwishoni mwa 2015 hadi alipojiuzulu Januari, 2022, muda mfupi baada ya kutofautiana kuhusu masuala ya mikopo ya nchi na Rais Samia Suluhu Hassan.

Jenista Mhagama – Waziri wa zamani

S

Chanzo cha picha, URT

Jenista Mhagama alikuwa mwanasiasa mkongwe na mmoja wa wanawake wachache waliowahi kushika nafasi ya uwazi katika wizara mbalimbali serikalini. Aliwahi kuwa Mbunge wa Peramiho na Waziri wa Afya, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, na Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Aliwahi pia kuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi katika utawala wa Rais Jakaya Kikwete kati ya Januari 2014 na Januari 2015.

Alijulikana kwa msimamo wake mkali kuhusu chama, lugha ya moja kwa moja na uaminifu wake kwa Chama cha Mapinduzi. Mhagama alikuwa kielelezo cha wanawake waliopambana kuvunja vikwazo katika siasa za ngazi ya juu.

Alifariki dunia Disemba mwaka 2025 nchini Tanzania baada ya kuugua kwa muda mfupi. Kifo chake kiliombolezwa sana na wanawake na wanachama wa CCM waliomchukulia kama mlezi na mfano wa uongozi.

Profesa Philemon Sarungi – Waziri na msomi

S

Chanzo cha picha, FB

Maelezo ya picha, Prof. Sarungi alikuwa mnazi mkubwa wa Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam

Profesa Philemon Sarungi alikuwa daktari bingwa wa upasuaji na mifupa na msomi aliyewahi kuwa Waziri wa Afya na baadaye Waziri wa Elimu. Alitoa mchango mkubwa katika kuboresha sera za afya na elimu, akitumia maarifa yake ya kitaaluma katika siasa.

Sarungi aliheshimika kwa utulivu, weledi na uwezo wa kuunganisha taaluma na siasa. Kabla ya siasa, alikuwa mhadhiri wa chuo kikuu na mshauri wa masuala ya afya ndani na nje ya nchi.

Alifariki dunia mwezi Machi mwaka 2025 baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Juma Mwapachu – Mwanadiplomasia na kiongozi wa kikanda

S

Chanzo cha picha, EAC

Juma Mwapachu alikuwa mwanasiasa, mwanadiplomasia na mtumishi wa umma aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Alikuwa mstari wa mbele katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda na sera za maendeleo ya Afrika Mashariki.

Ndani ya Tanzania, Mwapachu alihudumu katika bodi na taasisi mbalimbali za kitaifa, akijulikana kama msomi na mpatanishi mwenye heshima kubwa.

Alifariki dunia mwezi Machi mwaka 2025 kwa maradhi akiwa nje ya nchi. Kifo chake kiligusa sana sekta ya diplomasia na ushirikiano wa kikanda.

Hassy Kitime – Mbunge na Usalama wa taifa

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Hassy Kitime alikuwa mwana CCM mtiifu

Hassy Kitime alikuwa mmoja wa viongozi waliowahi kushika nyadhifa nzito serikalini. Aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) na Mbunge wa Makete.

Alijulikana kwa ukimya, uthabiti na uzoefu mkubwa katika masuala ya usalama na nishati. Alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa na ushawishi mkubwa ndani ya mifumo ya dola.

Mtoto wake, Ibra Kitine, alinukuliwa akisema baba yake alifariki dunia akiwa usingizini usiku wa kuamkia Julai 25, 2025 akiwa nyumbani kwake Oysterbay, Dar es Salaam.

Watu wengine maarufu walioaga dunia 2025

s

Chanzo cha picha, MC Pilipili

Maelezo ya picha, MC Pilipili alifariki kwa kushambuliwa huko Dodoma
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mbali na wanasiasa, mwaka 2025 pia uliwapoteza watu maarufu kutoka sekta za sanaa, burudani, mawasiliano na jamii. Vifo vyao viligusa moja kwa moja maisha ya watu wa kawaida kupitia muziki, maigizo, redio, na mchango wao katika utamaduni wa kisasa wa Tanzania.

Emmanuel Mathias maarufu kama MC Pilipili alikuwa mtangazaji na mchekeshaji aliyepata umaarufu mkubwa kupitia redio, runinga na majukwaa ya burudani. Alijulikana kwa ucheshi wa asili na uwezo wa kuunganisha watu wa rika zote. Alifariki dunia Novemba, 2025 huko Dodoma kutokana na kushambuliwa.

Mwigizaji Raidanus Vitalis aliyefahamika zaidi kama Kitundu katika tamthilia ya Jua Kali alikuwa sura pendwa ya televisheni, akiwakilisha maisha ya watu wa kawaida kwa uhalisia na ucheshi. Alifariki Juni, 2025, dunia baada ya kuugua kwa muda kifua na tumbo, na kifo chake kiliombolezwa na mashabiki wa maigizo.

Godson Rutta (G-Son), mmoja wa waanzilishi wa kundi la X Plastaz, alifariki dunia akiwa Marekani. Alikuwa balozi wa muziki wa Bongo Flava kimataifa na alitambulika kwa kuenzi lugha za asili na ujumbe wa kijamii kupitia muziki.

s
Maelezo ya picha, Charles Hillary, katikati mwenye suti, aliwahi kufanya kazi BBC, hapa alikuwa na baadhi ya wafanyakazi wa BBC walipomtembelea Ikulu Zanzibar

Charles Hillary, aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano Ikulu Zanzibar, alifariki dunia Mwezi Mei, 2025 baada ya maradhi. Alijulikana kwa taaluma na mchango wake katika mawasiliano ya serikali na vyombo vya habari. Ni mchezi na mtani kwa wanaomjua na wasiomjua.

Mwkaa 2025 pia imepoteza Hashim Lundenga, Mratibu wa zamani wa mashindano ya Miss Tanzania, Hashim Lundenga aliyefariki Jumamosi ya Aprili 19, 2025 katika hospitali ya Kitengule, Tegeta, Dar es Salaam alikokuw akipatiwa matibabu.

Wengine walioaga dunia mwaka 2025 ni pamoja na Master Tindwa Mtopa, mwandishi wa habari na mchambuzi wa michezo aliyekuwa akifanya kazi na Clouds media. Alifariki katika matukio ya Oktoba 29, 2025.

Gissima Nyamo-Hama, aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la umeme (Tanesco), aliyefariki mwezi April kwa ajali ya gari huko Bunda, Mara; pamoja na watu wengine waliokuwa na mchango mkubwa katika maeneo yao.