Ziara ya Trump Uingereza: Anakwenda na nini?

Donald Trump atawasili nchini Uingereza wiki hii kwa ziara yake ya pili ya kiserikali kama rais wa Marekani, atafuatana na makumi ya wafanyakazi na vifaa vya usalama.
Hatua zinazohitajika kumweka rais salama wakati wa kukaa kwake zinagharimu mamilioni ya pauni - zinazohusisha Idara ya Usalama (Secret Service) pamoja na maelfu ya maafisa wa polisi wa nchi husika.
Ziara yake ya kwanza ya serikali Juni 2019 - ilitumia zaidi ya maafisa 6,000 wa Polisi wa Metropolitan wakitumwa kwa gharama inayokadiriwa kuwa ni pauni milioni 3.4.
Usalama wa rais umeimarishwa katika siku za hivi karibuni kufuatia kupigwa risasi mwanaharakati wa kihafidhina Charlie Kirk katika chuo kikuu huko Utah.
Ronald Kessler, mwandishi aliye na ujuzi wa Idara ya Usalama, anasema, maandalizi ya ziara ya serikali huanza "wiki nyingi" kabla ya rais kuwasili na inajumuisha majadiliano na polisi wa nchi husika pamoja na ufuatiliaji wa vitisho vyovyote vinavyoweza kutokea.
Takriban maafisa 60 wa Idara ya Usalama wa rais kwa kawaida hupewa jukumu la kumlinda rais moja kwa moja, pamoja na polisi wa nchi husika ambao hutumika kuweka vizuizi kuzuia trafiki na usalama wa anga.
Ndege ya Rais

Chanzo cha picha, FLIKT
Trump, ambaye ataandamana na mkewe Melania, atawasili nchini Uingereza kwa ndege yake maalum aina ya Boeing 747-200B inayojulikana kama Air Force One.
Air Force One kwa hakika si ndege moja, bali ni mojawapo ya ndege mbili maalum za Boeing 747-200B, ambazo zina nambari 28000 na 29000.
Licha ya kuonekana kama ndege za kawaida za abiria kwa nje, Air Force One imeorodheshwa kama ndege ya kijeshi kutokana na vifaa vyake vya hali ya juu vya kielektroniki na mifumo ya ulinzi.
Imeundwa kupambana na shambulio la angani kwa kuvuruga rada ya adui na kutoa miale ya moshi ili kujikinga na makombora. Pia ina uwezo wa kuongeza mafuta katikati ya anga, ikiiruhusu kuruka kwa muda usio na kikomo - jambo muhimu wakati wa dharura.
Ndani ina futi za mraba 4,000 katika sakafu tatu za juu na chini, ikiwa ni pamoja na chumba kikubwa cha rais, chumba cha matibabu kilicho na meza ya upasuaji, na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya waandishi wa habari, wageni maalumu, usalama na wafanyakazi wa makatibu.
Gari la Rais

Chanzo cha picha, US Secret Service
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mara baada ya kutua, rais anasafiri katika gari la Cadillac One - ambalo limeboreshwa na kupewa jina la "Beast."
Matoleo mawili yanayofanana ya gari la rais, pamoja na magari mengine kadhaa ya Secret Service, yanasafirishwa hadi Uingereza kwa ndege za mizigo za kijeshi kabla ya Trump kuwasili.
Wakati rais anasafiri katika moja ya The Beast, lingine huandamana nalo na hutumia nambari zile zile za leseni za Washington DC - 800-002.
Gari hilo limejaa silaha na madirisha ya kuzuia risasi, ambayo huchangia uzito wake mkubwa wa takriban tani tisa (lb 20,000). Inaripotiwa kuwa na vifaa vya kurushia mabomu ya machozi, kamera za kuona usiku na simu ya satelaiti.
Matoleo ya hivi karibuni ya gari hilo pia yanaripotiwa kujumuisha mfumo wa oksijeni na friji ambalo lina damu inayolingana na aina ya damu ya rais itakayotumika katika dharura.
The Beast husafiri kama sehemu ya msafara wa rais, ambao unaweza kujumuisha zaidi ya magari kumi na mbili ikiwa ni pamoja na askari, timu za kukabiliana na mashambulizi na gari la mawasiliano la kivita la SUV, linalojulikana kama Roadrunner, madaktari na waandishi wa habari.
Kwa kawaida huwa haijulikani kwa watazamaji wa kawaida au washambuliaji ni gari gani hasa linamsafirisha rais.
Maafisa wa Idara ya Usalama wa Rais wanaweza hata kwenda katika barabara za chini ya ardhi na kumbadilisha Trump kutoka gari moja hadi gari lingine, "kulingana na Bw Kessler.
Helikopta

Chanzo cha picha, US Secret Service
Trump atafanya safari fupi kwa kutumia gari, lakini anatarajiwa kufanya safari zake nyingi angani - kama ilivyokuwa wakati wa safari yake ya Scotland Julai mwaka huu.
Rais ana uwezekano wa kuleta helikopta pamoja naye hadi Uingereza na miongoni mwao kutakuwa na Marine One ambayo, kama Air Force One, si ndege maalum bali ni helikopta yoyote ya Kikosi cha Wanamaji cha Marekani inayombeba rais.
Helikopta zilizoboreshwa zimefungwa mifumo ya ulinzi wa makombora na mifumo ya kuvuruga rada ya adui pamoja na vifaa vya kielektroniki vilivyoundwa kustahimili mapigo ya sumakuumeme ya mlipuko wa nyuklia.
Kama hatua ya usalama, Marine One mara nyingi huruka pamoja na kundi la helikopta zinazofanana zikifanya kazi ya kumpoteza adui.
Pia kawaida huambatana na helikopta mbili au tatu za Osprey MV-22s, ambazo hujulikana kwa uwezo mzuri wa kutua na kasi ya kuruka na ufanisi kama ndege.
Ospreys hubeba wafanyakazi wa usaidizi, vikosi maalum na maafisa wa idara ya usalama, ambao wana jukumu la kushughulikia dharura yoyote ya ndege.
Wafanyakazi wengine wa rais pia husafirishwa kwa anga, ikimaanisha kuwa msafara wa angani mara nyingi huwa na helikopta kadhaa.
Tishio la Droni

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Mfalme Charles III na Malkia Camilla watamkaribisha Trump na mkewe kwenye Jumba la Windsor Castle wakati wa ziara ya rais badala ya Jumba la Buckingham, ambalo linafanyiwa ukarabati.
Polisi wa Thames Valley wamesema ndege - ikiwa ni pamoja na droni - zitakuwa chini ya "vizuizi muhimu vya anga" karibu na Windsor Castle wakati wa ziara ya serikali, marufuku itakayote kelezwa na Idara ya Taifa ya Polisi wa Anga.
Tishio kutoka kwa ndege zisizo na rubani ni jambo muhimu kwa Idara ya Usalama wa Rais, kulingana na Kessler, ambaye anasema udhaifu katika uwezo wa kupambana na ndege zisizo na rubani ulionekana wakati wa jaribio la mauaji ya rais Julai 2024.
Kiongozi huyo wa Marekani atakuwa nchini Uingereza kwa siku mbili lakini hajaratibiwa kushiriki katika mazungumzo yoyote ya umma wakati wa kukaa kwake.
Maelfu ya watu wanatarajiwa kushiriki katika maandamano ya kumpinga Trump, yakiwemo maandamano huko Windsor na katikati mwa London.















